Kuacha kalamu na kushika silaha
中国国际广播电台

Katika karne ya kwanza, China ilipokuwa katika Enzi ya Han alikuweko msomi mmoja mashuhuri, anaitwa Ban Chao. Kwa ajili ya kulinda mipaka ya nchi aliacha kalamu na kushika silaha, na akawa bingwa wa kivita na mwanadiplomasia.

Mwaka 32 Ban Chao alizaliwa katika ukoo wa maofisa wa kuandikia historia, baba yake mdogo na ndugu yake mdogo wa kike wote walikuwa watu mashuhuri wa kuandikia historia katika historia ya China. Baba yake Ban Biao aliendelea kuandika mfululizo wa kitabu cha “Rikodi za Historia”, kaka yake Ban Gu alihariri na kuandika kitabu cha Historia ya Han na ndugu yake mdogo wa kike aliendelea kuandika kitabu hicho baada ya kaka yake kufariki. Ban Chao alisoma vitabu vingi toka utotoni mwake. Alikuwa mtu mwenye akili nyepesi, ujasiri mkubwa na uhodari wa kuongea kiada.

kwa sababu ya umasikini wa ukoo wake, ilimpasa Ban Chao kunukulu nyaraka serikalini ili kupata kijungu jiko. Lakini Ban Chao alikuwa mtu mwenye matumaini makubwa, haridhiki na kazi yake hiyo iliyokuwa ikirudia rudia kila siku.Wakati huo dola yake Han ilikuwa imepata tu utulivu baada machafuko ya muda mrefu wa vita, nguvu za taifa zilikuwa bado dhaifu, mpaka wa kaskazini mara kwa mara ulishambuliwa na dola ya Xiong Nu. Siku moja mkono wake ulimkaza kwa ajili ya kuandika sana, akifikiri kuwa kazi kama hii ina maana gani kwa taifa linalosumbuliwa mpakani! Akaitupilia mbali kalamu yake huku akipiga kite na kusema, “Mimi dume halisi laizima nitoe michango mpakani, bali sio kuishi na kalamu kila siku!” Basi akaacha kazi yake ya ukatibu akajiandikisha kujiunga na jeshi.

Baada ya kujiunga na jeshi, Ban Chao alipigana na vita kwa ushupavu na ujanja, akapata sifa nyingi nzuri. Werevu na ushupavu wake vilimvutia mfalme, hivyo akatumwa kwenye sehemu ya magharibi ya China, yaani mkoa wa Xin Jiang wa leo ili kuweka uhusiano mzuri na madola mengine ya huko.

Ban Chao aliondoka na wafuasi wake 36. Kwanza alifika Dola ya Shan Shan. Mwanzoni mfalme alimhehimu na kumkaribisha kwa ukarimu. Lakini baada ya siku kadha kupita mfalme akawa baridi. Kuona jinsi mfalme alivyo akawaambia wafuasi wake, “Mabadiliko ya msimamo wa mfalme panengine yatokana na kuja kwa wajumbe wa Xiong Nu ambao wanajaribu kuharibu uhusiano wetu na mfalme, nendeni mkafanye uchunguzi.” Baada ya kufanya upelelezi akaambiwa kwamba hali ilivyo ndivyo alivyokadiria. Basi Ban Chao aliwakusanya wafuasi wake pamoja akasema: “Tuko mbali na nchi yetu, na tumekuwa hatarini sasa, maana ikiwa mfalme wa Shan Shan akifuata ushawishi wa Xiong Nu sote tutauawa. Niambieni basi tufanyeje sasa?” Mara wafuasi wakamjibu, “Tutakusikiliza tu kufa au kupona.” Ban Chao akawaambia kwa uthabiti, “Hatuna njia nyingine ila tu kuwafyeka kabisa maadui wetu pangoni!”

Usiku huo huo aliwaongoza wafuasi wake kujificha nje ya mahema ya wajumbe wa Xion Nu. Kwa kusaidiwa na upepo waliwasha moto, na moto ukawaka ripuripu. Maadui walibumburuka na kukhangaika ovyo, kwa kutumia fursa hii wakatoma mahemani wakawaua wajumbe wote wa Xio Nu. Siku ya pili, Ban Chao alipomwona mfalme alifichua njama za Xion Nu na kumfariji vema mfalme. Mfalme akakata shauri kuweka uhusiano na Dola ya Han.

Kisha baadaye akiwa na wafuasi wake 36, Ban Chao alifika Dola ya Shu Le. Mfalme wa Dola ya Shu Le alikuwa ni mfalme wa kupandikizwa tu kutoka nje, kwa hivyo wananchi walikuwa wakimchukia, Ban Chao aliwasaidia kumwondoa na akamsimamisha mfalme wao wenyewe. Jambo hili liliungwa mkono na wananchi. Ban Chao licha ya kuweza kutumia ujanja wake kuwafyeka maadui, bali pia alikuwa hodari wa kuwashawishi wafalme waungane pamoja kupigana na maadui. Sha Che ilikuwa dola yenye nguvu, wakati huo mara kwa mara ilishambulia mataifa mengine ya magharibi. Ban Chao aliunganisha madola hayo kuishinda dola hiyo. Tokea hapo jina la Ban Chao lilikuwa likivuma sana katika sehemu ya magharibi ya China.

Katika muda wote wa miaka 31 alipokuwa katika sehemu ya magharibi, Ban Chao alifanya michango mingi mikubwa katika vita na diplomasia, akarudisha tene uhusiano wa Han na nchi nyingine uliokatika zaidi ya miaka 60, na alisaidia madola ya magharibi kutuliza ghasia na kuwashinda maadui wa nje. Kwa hivyo Ban Chao alipendwa sana na watu wa nchi za magharibi, aliporudi nyumbani Han kwa kuagizwa na mfalme wake, hata watu walilia machozi wakishika miguu ya farasi kumzuia asiwaache.

Ban Chao aliyekuwa msomi hapo awali na kushika silaha baadaye akawa mfano bora wa wasomi wa kujitolea kwa taifa.