“Ushindani wa Fikra za Aina Mia ”
中国国际广播电台


      Msemo wa Kichina “Ushindani wa Fikra za Aina Mia” ulianzia siku za kale katika Enzi ya Madola ya Kivita. Katika enzi hiyo, falsafa za aina nyingi zilikuweko kwa pamoja, wanasalsafa walikuwa wakitoa maoni na mitizamo yao huria, wakijadiliana, wakichapisha vitabu na kufundisha wanafunzi wao, hali hii ya ustawi wa falsafa tofauti katika uwanja wa taaluma ulipamba moto. Yafuatayo ni maelezo kuhusu msemo huo.

Enzi ya Madola ya Kivita iliyokuwa kabla ya karne ya tano mpaka karne ya tatu kabla ya kuzaliwa Kristo ilikuwa ni kipindi cha mwanzo wa ustaarabu wa China. Madola mengi yalikuwa pamoja na fikra za aina nyingi tofauti pia zilistawi katika jamii. Ili kuwavutia wasomi wa madola mbalimbali wajadiliane huria na kuwafundisha wanafunzi wao, mfalme wa Dola ya Chi alijenga kasri moja kubwa nchini mwake. Mwanaye Chi Xuanwang pia aliwapenda sana mabingwa wa fasihi na washauri wa kuzuru, kwa hiyo alijenga hosteli nyingi ili kuwahudumia bure. Wasomi waliokuja mji mkuu wa Dola ya Chi walifikia hata elfu, Dola ya Chi ikawa kama kituo cha ufafanuzi wa fasihi, falsafa na sayansi. Kila aina ya falsafa na taaluma ilijitahidi kujitangaza na kupinga aina nyingine, na ilitaka wafalme wa madola yote wapokee fikra zao katika utawala wao. Huu ndio msemo wa “ushindani wa fikra za aina mia”.

Sasa nawasimulieni kisa kimoja cha mfano: siku moja Chi Xuanwang alisema mbele ya Mencius: “Nimesikia kwamba mfalme Zhou Wenwang alijitengea sehemu ya uwindaji yenye eneo la kilomita za mraba 35, lakini wananchi wanaona kuwa sehemu hiyo ni ndogo, hali ambapo mimi nimejitengea sehemu ya uwindaji yenye eneo la kilomita za mraba ishirini tu, hata hivyo wananchi wanalalamika wakisema kuwa sehemu hiyo ni kubwa. Hivi leo wananchi hawajali mantiki”. Mencius akamwambia, “Ingawa sehemu ya uwindaji aliyojitengea mfalme Zhou Wenwang ni kubwa kiasi cha kilomita za mraba 35, lakini wananchi wanaruhusiwa kuingia ndani kukata kuni na kuwinda, kwa hiyo mfalme anatumia sehemu hiyo na wananchi kwa pamoja, ndio maana wananchi wanataka sehemu iwe kubwa zaidi. Mimi nilipokuja kwenye dola ya Chi nilisikia kwamba sehemu yako ya uwindaji hairuhusu wananchi kuingia mule ndani, na pindi mtu akiingia huadhibiwa. Kwa hiyo ingawa sehemu yako ni ndogo kiasi cha kilomita za mraba 20 tu lakini wananchi hawaambulii chochote, hii ndio sababu ya wao kuona sehemu yako kuwa kubwa, kwani hii sio kawaida?” Mfalme wa Dola ya Chi aliona aliyosema ni hoja kabisa, basi akawaruhusu wananchi kuitumia sehemu yake. Fikra hizi za Mencius ndio zilitetewa na Confucius, yaani “Ukarimu”.

Fikra zilizotetewa na tapo la Mo Ti ziligongana moja kwa moja na fikra za Confucius, kwamba zinakataza adabu nyingi na harija kubwa za mazishi, bali zilitetea “kubana matumizi”, na pia zilipinga vikali vita kati ya madola, zilitetea amani. Kufuatana na fikra za Mo Ti, iwapo watu wanaishi bila ubadhirifu na kwa kupendana, basi dunia itakuwa na amani daima.

Lilikuwepo tapo lingine la fikra ambalo liliwakilishwa na fikra za Han Fei, huyu ni mwanafalsafa wa uyakinifu. Alitetea mageuzi, aliona kwamba jambo lolote huwa na sheria yake ya mwanzo na mwisho. Yeye alikuwa ndio wa kwanza kutoa hoja ya “hitilafu”. Alieleza ngano moja: Mtu mmoja aliuza mkuki na ngao. Alimwambia mtu aliyetaka kununua mkuki akisema, mkuki wake unaweza kutoboa ngao yoyote duniani, kisha alimgeukia mtu mwingine aliyetaka kununua ngao, akisifu ngao yake inaweza kukinga mkuki wowote duniani. Basi mtu wa tatu aliuliza pembeni: Nikitumia mkuki wako kutoboa ngao yako je? Muuzaji alishindwa kujibu. Kutokana na ngano hiyo Han Fei alitoa hoja ya kuwa kila jambo huwa na pande mbili.

Katika siku za fikra za aina tofauti mashindano ya wasomi licha ya kufundisha wanafunzi pia waliandika vitabu, wakajitokeza wawakilishi kadhaa wa matapo ya fikra tofauti kama Mencius, Zhuanzi, Hanfei, na Mo Ti, ambapo walichapisha maandishi mengi ya taaluma. Fikra zao zilisogeza sana mbele fikra na maendeleo ya utamaduni wa China ya kale. Hivi leo watu wanaendelea kutumia msemo huu wanapofananisha na ushindani huru wa fikra tofauti.