Kutunga Shairi kwa Hatua Saba
中国国际广播电台


       China ina historia ndefu ya miaka elfu tano kwa mujibu wa rekodi. Katika historia ndefu kama hiyo utamaduni wake wa aina mbalimbali ulikuwa ukitajirika zaidi na zaidi kutoka enzi hadi enzi. Utamaduni huu ni kama uhondo tunaoufaidi bila mwisho. Mila na desturi, riwaya, hadithi, matukio na watu wenye vipaji, n.k. mengi yalitokea na yanaendelea kuathiri kwa kina Wachina wa sasa. Leo, katika kipindi hiki nitawasimulieni hadithi kuhusu mtu mmoja mashuhuri, aliyeitwa lake Cao Zhi.

Baba yake Cao Cao alikuwa mwanzilishi wa Dola ya Wei katika karne ya pili, Enzi ya Madola Matatu ya Kifalme. Maisha yake yote yalikuwa ya kupigana vita, lakini pia alikuwa mshairi hodari na mashairi yake mengi yanasomwa mpaka hivi leo. Cao Cao alikuwa na watoto wawili, wote wa kiume. Mkubwa aliitwa Cao Pi, na wapili Cao Zhi. Baada ya Cao Cao kufariki, mwanawe wa kwanza Cao Pi alirithi kiti chake cha ufalme. Cao Pi alikuwa mhakiki wa fasihi, na kitabu chake “Tasnifu” ni utunzi wa kuanza kipindi kipya katika historia ya uhakiki wa fasihi. Mtu anayeelezwa katika kipindi hiki ni ndugu yake Cao Zhi, mtoto wa pili wa Cao Cao. Cao Zhi alikuwa mtu mwenye kipaji kikubwa katika fasihi, alikuwa mshairi hodari wa mwisho katika enzi yake.

Kaka yake Cao Pi baada ya kurithi kiti cha ufalme alimwonea gere kwa kipaji chake cha fasihi. Hata siku moja kwa makusudi alitaka kumtesa, ila atunge shairi moja kamili kabla ya kupiga hatua saba, na shairi lenyewe lilitakiwa liwe na vina. Cao Zhi alielewa kwamba kaka yake alimkanganya kwa makusudi, lakini hakuweza kumkatalia kwa kuwa yeye alikuwa mfalme. Huku akifikiria kuwa anayemtesa ni kaka yake wa tumbo moja, Cao Zhi alijawa na huzuni na hasira, na papo hapo alitunga shairi lake lenye beti nne:

Kunde zachemshwa na vikonyo vyake sufuriani,

Kunde zalia machozi kwa huzuni,

Kunde na vikonyo vyatokana na mzizi mmoja awali,

Ya nini kutesana hivi kikatili.

Shairi hili lilimgusa kaka yake, aliona haya, akaacha nia yake ya kumtesa.

Ufanisi mkubwa wa Cao Zhi maishani mwake ulikuwa tungo zake za mashairi. Katika Enzi ya Madola Matatu ya Kifalme, vita vilikuwa vikiendelea kwa mfululizo, vita vilisababisha jamii kunyauka. Ingawa alikuwa na nasaba ya kifalme lakini aliwahurumia sana wananchi maskini na waliopoteza maskani yao. Dunia ilivyokuwa ya fujo na hali ilivyokuwa ya masikitiko ilimwamsha uzalendo wake, hata katika shairi lake aliandika hivi, “Jitolee mhanga kuokoa taifa, kufa ni kama kuzaliwa”. Ubeti huu ni maarufu katika enzi zote.

Ingawa Cao Zhi alikuwa na ujuzi mkubwa wa kutunga mashairi, lakini hakuridhika nao, bali alikuwa siku zote akitaka kufanikisha mambo ya kisiasa. Kutokana na hayo alishukiwa na kunyanyaswa na kaka yake mfalme, maisha yake yalikuwa hayamwii shwari. Mengi ya mashairi yake yalieleza jakamoyo yake ya kutoweza kukamilisha ndoto yake, lakini alikuwa hawezi kujieleza kinaganaga. Kutokana na sababu hiyo, hali ya ajabu ilitokea katika mashairi yake, kwamba alisawiri wasichana wengi warembo, kama vile katika vitabu vyake vya “Juzuu ya Mashairi ya Vipusa”, “Warembo wa Nchi ya Kusini” n.k. Warembo katika mashairi yake walikuwa sio tu waliumbika kikamilifu bali pia ni wasichana wenye ujuzi mkubwa, maadili mazuri na wenye matumaini mema, aliandika hivi ili kujiliwaza. Miongoni mwa mashairi kama hayo, uliojitokeza ziadi ni Utenzi wa “Malaika Luo Shui”. Luo Shui ni jina la mto karibu na Mji wa Luo Yang. Katika hadithi ya mapokeo msichana mmoja alijitosa mtoni na baadaye akawa malaika. Kwa kutumia hadithi hii Cao Zhi alisawiri msichana mmoja mwenye haiba nyingi, na alieleza uchungu wake asiweze kumwoa malaika huyo kutokana na kuwa binadamu. Ingawa mhusika mkuu huyo ni wa kubuniwa tu lakini kwa ustadi wake mkubwa alimsawiri jinsi alivyovutia kama alivyo hai. Alieleza, “Dansi aliyocheza kama bata-maji arukavyo angani, nyonga aliyokatika kama joka majini”. Utenzi huu unasifiwa na wanafasihi wote.

Cao Zhi mwenye kipaji cha mashairi alikuwa na miaka 41 tu duniani, lakini athari zake ni kubwa katika fasihi nyuma yake. “Kutunga shairi kwa hatua saba” umekuwa msemo wa kueleza fulani mwenye kipaji kikubwa cha fasihi.