Kuchuma Maua katika Bustani ya Qujiang
中国国际广播电台


        Katika karne ya nane wakati Enzi ya Sui nchini China, mfalme alianzisha utaratibu wa kufanya mtihani wa kuchagua maofisa wakubwa wa serikali, hadi Endi ya Tang utaratibu huo uliendelea na kuwa wasomi wa kawaida waliweza kushiriki katika mtihani huo, kwa hiyo utaratibu huo ulikuwa njia ya kujipatia nyadhifa kwa wasomi wote.

Mtihani uligawanyika katika ngazi tatu, ngazi ya mwisho ni mtihani wa kuchagua maofisa wakubwa ambao wanaweza kufanya kazi karibu na mfalme, lakini mtihani huo ulikuwa mgumu kiasi kwamba hata kati ya watu mia moja waliofanya mtihani, waliochaguliwa hawakufika ishirini. Watu wengi walishindwa mara kadhaa, na baadhi walifaulu mtihani hadi walipokuwa na umri wa zaidi ya miaka hamsini.

Mfalme alikuwa anafanya sherehe kubwa kuwapongeza waliofanulu mtihani katika bustani ya Qujiang mjini Xi'an, mji mkuu wa Enzi ya Tang.

Bustani ya Qujiang ilikuwa kubwa, ndani yake kuna ziwa kubwa, maua, pagoda ya Dayan na mahekalu.

Kwenye sherehe, waliofulu mtihani waliweka mabakuli yenye pombe juu ya maji, mabakuli yalielea na yanapotulia karibu na fulani basi yeye anachukua bakuli hilo kunywa pombe na kutunga mashairi, na kuwaalika vijana wawili kwenda kuchuma maua na kumpa kila mmoja wa waliofaulu mtihani kutia kifuani.

Mwaka mmoja, mfalme alifanya sherehe katika bustani hiyo, na baada ya kumaliza sherehe, wasomi waliofaulu mtihani walitembea katika bustani hiyo. Mmoja kati ya wasomi hao alipofika kwenye pagoda ya Dayan alichonga jina lake kwenye jiwe la pagoda hiyo, tokea hapo kuchonga majina ya wasomi waliofaulu mtihani ikawa ni desturi, kwamba baada ya sherehe ya mfalme kila mmoja alikuwa anachonga jina lake kwa wino, na kama baadaye fulani alikuwa jemadari au waziri basi jina lake lilikuwa linapakwa rangi nyekundu.

Utaratibu wa kuchagua maofisa kwa kuwafanyia mtihani uliwawezesha wasomi wa kawaida kabisa kupata nafasi ya kuwa maofisa wakubwa wa kusimamia mambo ya taifa. Lakini utaratibu huo ulibadilika kuwa mbaya, hasa katika enzi za Ming na Qing, mtihani ulibadilika kuwa wa vitabu vya Confucius tu, na makala ilikuwa ni lazima iwe na idadi maalumu ya maneno na mtindo maalumu. Mtihani huo ulikuwa wa kuchezea maneno bila maana. Vitabu vya “Hadithi za Mashetani” na “Mashujaa kwenye Vinamasi” vilifichua ubovu wa mtihani huo.