“Uongo ukirudia mara tatu ukawa kweli”
中国国际广播电台


       Uzushi na kashfa zikivuma kwa marudio, huaminika kuwa kweli. Kifuatacho ndicho kisa chenyewe:

Katika karne ya tano kabla ya Kristo kuzaliwa, nchini China yalikuwako madola madogo madogo mengi, na madola hayo yalikuwa hayaishi kupigana vita kunyakuana ardhi, kwa hiyo wanahistoria wa baadaye wanaziita enzi hizi kuwa “Enzi za Madola ya Kivita”.

Lakini hata hivyo yalikuwako madola mawili yaliyopakana, Dola la Wei na Dola la Zhao, yaliahidiana kuweka urafiki kwa mkataba. Ili kuhakikisha mkataba huo ufuatwe, madola haya yalikubaliana kupeana makole kama ni wadhamini. Mfalme wa Wei aling'amua kumpeleka mwanawe kwenye mji mkuu wa Dola la Zhao, Handan, pamoja na mwanawe kwenda huko pia alikuwako waziri wake, Pang Cong, ili kuhakikisha mwanawe katika hali ya usalama.

Peng Cong alikuwa na wapinzani kadha ndani ya kasri kwa kumwonea gele umahiri wake. Kwa hiyo, alikuwa na wasiwasi kwamba angesingiziwa asipokuwepo. Kufikiri hivyo, kabla ya yeye kuondoka alionana na mfalme wake, alisema:

“Mheshimiwa mfalme, ikiwa fulani atakuambia chui amekuja mjini kwenye barabara, utaamini?”

Mfalme alijibu haraka, “Hataa, chui anawezaje kuja hata barabarani?”

Pang Cong aliuliza zaidi, “Ikiwa watu wawili wakikuambia hivi, utaamini?”

Mfalme alijibu, “Kama nikiambiwa hivi na watu wawili, nitakuwa na tuhuma kidogo.”

Pang Cong aliendelea, “Ikiwa watu watatu je?”

Mfalme alisita kidogo kisha alimwambia, “Nikiambiwa na wote watatu, basi inanipasa niwaamini.”

Kusikia majibu hayo, Peng Cong aliingiwa na wahka zaidi, alishusha pumzi na kusema, “Mheshimiwa, jua kwamba chui hawezi kuja barabarani, huu ni ujuzi wa kawaida kwa kila mtu. Almradi watatu wamesema hivi, basi usemi wa chui wa barabarani ukawa wa kweli. Umbali kati ya mji mkuu wa Dola la Zhao, Handan, na mji mkuu wetu Daliang ni mkubwa sana kuliko umbali kati ya kasri na barabara, na watakaonisengenya pengine watazidi watatu.”

Mfalme alielewa maana aliyokusudia, akasema, “Nishakuelewa, nenda tu usiwe na wasiwasi!”

Basi Pang Cong na mwana wa mfalme walifunga safari kwenda mji wa Hanadan.

Kweli haikuwa muda mrefu kupita baada ya Pang Cong kuondoka, maneno mabaya juu yake yakaanza kuvuma. Mwanzoni mfalme alikuwa humzungumzia, akisema Pang Cong ni mahiri tena ni mtiifu. Lakini wapinzani walikuwa wanarudiarudia kashfa zao, mwishowe mfalme akawaamini kabisa. Baada ya Pango Cong kurudi nchini kutoka Dola la Zhao mfalme hata hakumruhusu aonane naye.

Pia kiko kisa kingine kinachofanana na hiki: Zeng Can alikuwa msomi katika Enzi ya Madola ya Kivita. Yeye alikuwa mwadilifu kamili. Siku moja alisafiri mbali. Kwa sadfa alikuwako mhalifu mmoja mwenye jina sawa na lake, alikamatwa. Jirani kwa haraka alimhabarisha mama yake, “Toba! mwanao amekamatwa kwa uhalifu wa uuaji”. Mama wa Zeng Can alimwamini kabisa mwanawe kwamba uhalifu kama huu kamwe mwanawe hauwezi, aliendelea kufuma nguo yake. Punde si punde mwingine alikuja akimwambia mama huyo, “Ala, mwanao ameua mtu!” Hapo, mama huyo akaanza kushikwa na wasiwasi, lakini pia hakuamini. Muda si muda mtu wa tatu akaja na maneno yale yale. Wakati huo mama huyo akawaamini kabisa, alitupa kazi yake akatoroka haraka.

Visa hivi vyote vinatuambia “ULIMI UNAUA”.