Kuwa katika Hali ya Kuzingirwa na Wapinzani Pande Zote
中国国际广播电台


       Tuseme Fulani akikumbwa na matatizo mengi na hali ya mazingira yenyewe inaelekea kuwa hakika huyo atashindwa, usemi wa Kichina hueleza mtu kama huyo amekuwa katika hali ya kuzingirwa na wapinzani pande zote. Sasa nawaelezeni changzo cha usemi huo jinsi ulivyotokea:

Katika mwaka 202 kabla ya kuzaliwa Kristo historia ya China iliingia katika Enzi ya Kifalme ya Qin. Sanamu za askari na farasi zilizofukuliwa katika Jimbo la Shaansi pamoja na Ukuta Mkuu yote ni masalio ya utamaduni wa enzi hiyo.

Wafalme wa enzi hiyo walikuwa wakijitahidi kutukuza ufahari wao, na kati ya wafalme hao aliyejitokeza zaidi alikuwa Qin Shihuang. Huyo mfalme alijengesha kasri kubwa ya fahari na kaburi la starehe kwa pesa nyingi alizozinyonya kutoka kwa wananchi wake. Hivyo basi wananchi walikuwa wakiinuka mara kwa mara, matokeo yakawa Enzi ya Qin ilipinduliwa baada ya miaka 15 tu tangu ilipoanza. Baada ya Enzi ya Qin kupinduliwa, vilikuwako vikundi viwili vilivyokuwa vikijitahidi kunyakua utawala wa China. Kimoja kiliongozwa na Xiang Yu, kingine kiliongozwa na Liu Bang.

Xiang Yu alikuwa jamadari katika sehemu ya Chu mwenye hulka ya unyoofu, ujeuri na ni mjasiri wa kupigana vita. Liu Bang alikuwa ofisa mdogo kabla ya Enzi ya Qin kupinduliwa mwenye hulka ya ujanja na ni hodari wa kuchagua wasaidi wake. Katika siku za kupindua Enzi ya Qin hao wawili walikuwa ndugu wa kuchanjiana wakisaidiana katika hali na mali. Lakini baada ya tu kufanikiwa kupindua Enzi ya Qin wakageukiana.

Mwanzoni nguvu za Xiang Yu zilimzidi kabisa Liu Bang, alijitawaza kuwa “Mbabe Chu” ambaye ni kama mfalme, Liu Bang akatawazwa kuwa “Mwinyi Han” ambaye ni kama mtawala wa sehemu tu. Ili kuhifadhi nguvu Liu Bang alijidai kukubali utawala wa Xiang Yu, lakini kichini chini aliwakusanya mahodari na kuzidisha nguvu zake za kijeshi. Hivyo basi zaidi na zaidi nguvu zake zikawa zinalingana na nguvu za Xiang Yu.

Vita baina ya Xiang Yu na Liu Bang viliendelea kwa miaka kadha. Kipindi hiki kinaitwa “Vita vya Chu na Han” katika historia. Katika vita Xiang Yu alimshindilia mbali Liu Bang na aliwateka nyara baba na mkewe. Xiang Yu alimtia kizuizini baba wa Liu Bang kama kole, akimdai Liu Bang asalimu amri, sivyo atamchinja na kumchemsha kuwa supu. Lakini bila kutazamiwa, Liu Bang akamwambia Xiang Yu, “Tulipopambana na Qin tulikuwa ndugu, basi baba yangu ni yako pia, ikiwa ukitengeneza supu kwa baba yangu basi usisahau kunigawie.” Kusikia hayo Xiang Yu alikuwa hana budi ila kumrudishia Liu Bang baba yake na mkewe.

Vita vya kuamua mshindi vilipigana katika sehemu ya Gaixia [Jimboni Anhui kwa leo]. Vita vilikuwa vikali na mwishowe askari wa Liu Bang walimzingira Xiang Yu na askari wake. Ingawa Xiang Yu alikuwa katika hali mbaya lakini bado alibaki na askari kiasi cha laki moja na Liu Bang hakuweza kuwafyeka kwa mkupuo.

Siku moja usiku, ghafla Xiang Yu na askari wake waliozingirwa walisikia nyimbo walizozoea kutoka pande zote, wakateka zaidi masikio, kumbe zilikuwa ni nyimbo za watani wao Chu. Xiang Yu na askari wake walistaajabu sana wakidhani Liu Bang keshauteka watani wake na kuwaleta mateka wenyeji wa huko kuimba. Nyimbo zilisababisha askari kukumbuka sana watani wao, nia ya kupigana ikaporomoka, nao wakatoroka katika usiku wenye giza tititii, askari kiasi cha laki moja mwishowe wakabaki mia kadha tu.

Kumbe, hii ilikuwa ni ujanja wa Liu Bang. Aliwashirikisha askari wake kuimba nyimbo za huzuni za sehemu ya Chu ili kuporomosha nia ya askari wa Xiang Yu.

Liu Bang alishinda kabisa katika vita hivyo, akaanzisha Enzi ya Han, na Xiang Yu akalazimika kujiua. Enzi ya Han ilijitokeza sana katika usitawi wa uchumi na utamaduni katika historia ya China.