Matunda Matatu Yaua Watu Watatu
中国国际广播电台


        Katika Kipindi cha Madola ya Kivita, madola mengi yalikuwa yakipambana. Katika Dola la Qi kulikuwa na mabwana watatu wa kivita, waliheshimiwa sana na watu. Lakini watu hao watatu baadaye walikuwa wajeuri.

Waziri mkuu wa Dola Qi alipoona kuwa watatu hao walizidi kuwa wajeuri na wakatili, aliamua kuwaua. Siku moja mfalme wa Dola la Lu alitembelea Dola la Qi, watatu hao pamoja na maofisa wengine walialikwa kwenye chakula pamoja na mfalme wa Dola la Lu, hao watatu walionekana wenye kiburi kupita kiasi. Wakati walipokuwa wanakula, waziri mkuu alimwambia mfalme wake aende kuchuma matunda kuwakaribisha. Lakini baada ya kuwagawia, matunda yalibaki mawili tu na wasiopata matunda walikuwa majasiri hao watatu. Waziri mkuu alitoa shauri kuwa kila mmoja kati ya watu hao watatu aeleze mchango wake, mwenye mchango mkubwa atapata tunda moja. Mfalme alikubali.

Kila mmoja alieleza mchango wake. Mmoja alisimama na kusema, “Nilipofuatana na mfalme kuwinda nilimwua chui mmoja na kumwokoa mfalme, mchango huu si mkubwa?” waziri mkuu alisema, “Mchango huu si mdogo, unastahili kupewa tunda moja.”

Mwingine alisimama na kusema, “Mimi niliwahi kumwua kobe mkubwa na kumwokoa mfalme, mchango huu si mdogo.” Waziri mkuu alijibu, “Mdio, unastahili pia kupewa tunda moja.”

Wa tatu alisimama, na kueleza jinsi aliwashinda jeshi la wavamizi na kulinda usalama wa taifa. Alimwuliza mfalme, “Mchango wangu huu si mkubwa kuliko wengine?” Lakini matunda mawili yaliyobaki yameisha, mfalme alimfariji, “Utapewa safari ijayo.”

Lakini aliona kuwa alipuuzwa vibaya, watu waliokuwa hawakutoa mchango mkubwa kama yeye walipata matunda, yeye mwenye mchango mkubwa zaidi hakupewa. Kwa kufikiri hivyo, alitoa upanga na kujiua. Wengine wawili waliona kuwa hata mwenye mchango mkubwa alijiua na waliwahi kula kiapo kuwa watakufa pamoja, basi walijiua vilevile.

Watu waliokuwa kwenye chakula walishtuka, lakini kwa akili waziri mkuu aliwaua watu hao wajeuri.