Hadithi ya Xi Menbao
中国国际广播电台


       Xi Menbao alikuwa mtu wa karne ya tano K.K. Kutokana na uhodari wake aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya. Alipofika tu wilayani mara aliwaalika wazee wa huko kuwauliza mambo yanayowasumbua. Wazee walimwambia kwamba kila mwaka shetani wa mto alitaka kumwoa mke mmoja.

Wila hiyo iko karibu na Mto wa Huanghe, wenyeji walisema ndani ya mto aliishi shetani mmoja ambaye kila mwaka anataka kumwoa mke mmoja, la sivyo shetani huyo atachafua mto na kuleta mafuriko makubwa. Maofisa na washenga walitumia fursa hiyo kuwatoza raia na kugawana pesa za kodi.

Wazee walimwambia Xi Menbao kuwa kila mwaka mshenga mzee mmoja alitembeatembea kila mahali kuchagua msichana na kusema “Basi huyu msichana achaguliwe kuwa mke wa shetani wa mto!” Kisha alimchukua msichana huyo na kumbadilishia nguo mpya na kumkalisha juu ya kitanda na kumtupa mtoni. Mwanzoni msichana huyo alielea, lakini baadaye alizama. Mshenga alisema, shetani amekubali kumpokea. Baada ya kusikia hayo, Xi Menbao hakusema kitu.

Siku nyingine ya kuchagua msichana iliwadia. Xi Menbao aliongoza askari wake kusubiri kando ya mto. Muda si muda maofisa, matajiri na mshenga walikuja na msichana aliyechaguliwa. Mshenga alikuwa na umri wa miaka zaidi ya 70.

Xi Menbao alisema, “Mwite mke wa shetani wa mto mbele yangu, nione kama ni kisura.” Msichana aliletwa, Xi Menbao alimwangalia na kusema, “Huyu msichana si mzuri, lakini leo shetani anasubiri kumpokea mke wake, basi tumwomba mshenga aende kumwambia shetani kwamba tutamchagua msichana mwingine mzuri zaidi.” Kisha aliwaamuru askari wamtume mshenga mtoni. Baada ya dakika chache, Xi Menbao alisema, “Mbona mshenga hakurudi kutuambia jawabu?” Alimwagiza mfuasi wa mshenga aende kuuliza habari, basi askari wakamtupa mfuasi wa mshenga.

Waliokuwa kwenye ukingo wa mto, matajiri na maofisa walishikwa na hofu. Xi Menbao alisema, “Inaonekana kuwa shetani ni mkarimu wa kuwapokea wageni, afadhali tuwatume wengine kwenda kuonana na shetani. Maofisa na matajiri wote wakapiga magoti na kutubu wasitupwe mtoni.

Kwa sauti kubwa, Xi Menbao aliwaambia watu waliopo, “Huu ni udanganyifu mtupu, katika siku za usoni yeyote atakayeshughulikia jambo hilo atatupwa mtoni.” Tokea hapo watu walianza kuishi katika hali ya utulivu.