Tian Ji Ashindana Mbio za Farasi
中国国际广播电台


      Katika Kipindi cha Madola ya Kivita alikuwepo ofisa mmoja wa Dola la Wei, aliyeitwa Sun Bin. Kutokana na kusingiziwa na maofisa wengine alikuja kwenye mji mkuu wa Dola la Qi.

Jemadari mkuu Tian Ji wa Dola la Qi alimpokea na kuzungumza naye kwa siku tatu. Kutokana na mazungumzo alifahamu kuwa huyo Sun Bin ni hodari kwa ujuzi wa kivita.

Kushindana kwenye mbio za farasi ulikuwa ni mchezo ulioenea sana, lakini Tian Ji kila mara alishindwa na mfalme wake. Sun Bin alimwambia Tian Ji, “Safari ijayo nitakwenda kuangalia mashindano yenyewe, pengine nitaweza kukusaidia upate ushindi.”

Siku moja mashindano ya mbio za farasi yalifanywa tena, watu wengi walifika kutazama mashindano. Sun Bin alielewa kuwa farasi waligawanyika katika ngazi tatu kutokana na uwezo wa mbio, na farasi pia wanatofautiana kwa matandiko tofauti.

Baada ya kuangalia, Sun Bin aligundua kuwa farasi aliyemtumia Tian Ji hakuwa nyuma sana ila tu hakutumia mbinu vizuri. Sun Bin alimwambia Tian Ji, “Usiwe na wasiwasi, naweza kukusaidia kupata ushindi.” Tian Ji alifurahi sana, alimwalika mfalme kushindana naye. Mfalme aliona kuwa hakuwahi kushindwa kwake, hivyo akakubali.

Kabla ya mashindano, Tian Ji alitumia tandiko la farasi wa ngazi ya kwanza kuweka kwenye farasi wa ngazi ya pili. Katika mashindano farasi wa mfalme alipiga mbio na kumwacha nyuma kabisa farasi wa Tian Ji. Mfalme alifurahi sana. Katika raundi ya pili, kama alivyoambiwa na Sun Bin, Tian Ji alitumia farasi wa ngazi ya kwanza kushindana na farasi wa ngazi ya pili wa mfalme, Tian Ji alishinda. Katika raundi ya tatu, Tian Ji alitumia farasi wake wa ngazi ya pili kushindana na farasi wa ngazi ya tatu wa mfalme, Tian Ji alishinda vilevile. Mashindano yalimalizika na Tian Ji alimshinda mfalme kwa mabao mawili kwa moja.

Mfalme alipigwa bumbuazi, hakufahamu sababu. Tian Ji alimwambia mfalme kuwa hakumshinda kwa kupata farasi hodari zaidi bali alitumia mbinu bora, na mbinu hizo ni za Sun Bin. Sun Bin alimwambia mfalme, wakati ambapo nguvu za pande mbili zikiwa karibu sawa, mbinu sahihi ni muhimu sana, na wakati ambapo nguvu za pande mbili zikiwa tofauti sana, mbinu sahihi pia zinasaidia sana kupunguza hasara. Baadaye, mfalme alimteua Sun Bin kuwa jemadari mkuu, na jeshi lililoongozwa na Sun Bin lilipata ushindi mara nyingi katika vita.