Chu Long Amshawishi Mama Mfalme Zhao
中国国际广播电台

Katika Kipindi cha Madola ya Kivita, mtu aliyetawala Dola la Zhao alikuwa mama mfalme Zhao. Mwaka mmoja Dola la Qin lenye nguvu kubwa zaidi lilitaka kuvamia Dola la Zhao. Kutokana na uhusiano mzuri, Dola la Zho liliomba Dola la Qi msaada. Lakini mfalme wa Dola la Qi alitaka kuchukua mtoto wa mama mfalme awe kama dhamana. Mama mfalme Zhao alimpenda sana mtoto wake, alihofia atakuwa hatarini, kwa hiyo alikuwa na wasiwasi bila kufanya uamuzi. Mawaziri walimshawishi mama mfalme akubali kupeleka mtoto wake kwenye Dola la Qi ili kusalimisha taifa. Mama mfalme Zhao alikasirika, alisema, “Yeyote atakayenishawishi kufanya hivyo nitamtemea mate usoni.”

Siku moja waziri mwenye heshima Chu Long aliomba kuonana na mama mfalme. Mama mfalme alidhani alikuja kumshawishi, alikarisika. Lakini Chu Long hakutaja jambo hilo, ila tu kusema, “Nakuja kukusalimu tu, kwa sababu siku nyingi sikukuona.”

Mama mfalme alisema, “Siku hizi sina hamu ya chakula.” Chu Long alisema, “Na mimi vilevile, siku hizi sili sana kutokana na kukaa tu.” Kutokana na maongezi ya mambo ya kawaida, hasira ya mama mfalme ilipungua.

Chu Long alisema, “Nimekuja na shida yangu, kwamba nina mtoto mmoja anaitwa Shu Qi, naona hatakuwa na matumaini ya kuwa mtu wa maana, mimi nimekuwa mzee, naomba wewe ukubali mtoto wangu awe mlinzi katika kasri lako.” Mama mfalme aliuliza, “Ana miaka mingapi?” Chu Long alijibu, “Miaka 15, ingawa umri wake bado mdogo, lakini nataka kumpangia maisha kabla ya mimi kufariki.” Mama malkia alisema, “Sikutegemea kuwa kumbe wanaume pia wanapenda sana watoto wao.” Chu Long alisema, “Pengine zaidi kuliko wanawake.” Chu Long aliendelea, “Wazazi wanapenda watoto wao kwa kuwafikiria mbali.” Kisha Chu Long aligeuza mazungumzo yake akisema, “Lakini naona wewe hujamfikiria mbali mtoto wako.” Mama mfalme hakufahamu maana yake, aliuliza sababu. Chu Long alisema, “Tokea enzi na dahari, watoto na wajukuu wa wafalme walioweza kuendelea na ufalme ni wachache, lakini sio kwa sababu wao walikuwa hawana uwezo, bali kwa sababu ingawa nafasi zao zilikuwa juu sana lakini michango yao kwa ajili ya maslahi ya taifa ilikuwa midogo. Baada ya wao kushika utawala walishindwa kuendelea kwa muda mrefu. Hivi sasa umempangia nafasi mtoto wako na kumpa hazina nyingi, lakini umeacha fursa yake ya kutoa mchango kwa ajili ya taifa, basi atakuwaje kuwa mtawala wa daima baada ya wewe kufariki? Ndio maana nasema hujamfikiria mbali mtoto wako.”

Baada ya kusikia hayo, mama mfalme alikubali kupeleka mtoto wake kwenye Dola la Qi ili kupata msaada wa kijeshi.