Hadithi ya Mo Zi
中国国际广播电台


       Mo Zi alikuwa mtu wa karne ya tano K.K. Wakati huo kulikuwa na madola mengi nchini China. Kati ya madola hayo, Dola la Chu lilikuwa kubwa na Dola la Song lilikuwa dogo.

Fundi aitwaye Gong Shuban alitengneneza ngazi moja ndefu kwa ajili ya kuparamia ukuta mrefu wa mji. Baada ya ngazi hiyo kuwa tayari, Dola la Chu lilipanga vita dhidi ya Dola la Song.

Mo Zi aliposikia habari hiyo, alisafiri kwa siku kumi hadi kwenye mji mkuu wa Dola la Chu, na kukutana na Fundi Gong Shuban. Alisema, “Mtu mmoja wa kaskazini anataka kuniua, naomba kutumia nguvu zako kumwua yeye.” Gong Shuban alikuwa kimya. Mo Zi aliendelea, “Nitakupa pesa nyingi kama ni shukrani zangu.” Gong Shuban alijibu, “Kwa maadili yangu naweza kumwua mtu?” Mo Zi alisema, “Dola la Chu ni kubwa, watu wachache lakini ardhi kubwa, lakini linataka kushambulia dola dogo, hivi ni vita visivyo vya halali, wewe unasema hutamwua mtu, lakini vita vikizuka watu wangapi watauawa kutokana na ngazi yako ndefu?”

Gong Shuban alikuwa hana la kusema, na kwa kisingizio alisema aliamrishwa na mfalme Chu. Mo Zi alikwenda kukutana na mfalme Chu. Mo Zi alimwambia mfalme, “Hivi sasa kuna mtu anayetaka kuiba mkokoteni mbovu wa jirani hali anao mpya, na anataka kuiba nguo zilizochakaa wakati yeye anayo nguo mpya, huyo ni mtu wa namna gani?” mfalme Chu alijibu, “Ana tabia ya kuiba.” Mo Zi alisema, “Dola lako lina ardhi nyingi, na Dola la Song ni ndogo, Dola la Chu lina maliasili nyingi na Dola la Song ni maskini, kwa hiyo naona Dola la Chu ni sawa na mwenye tabia ya kuiba.”

Mo Zi aliendelea kusema, “Wewe mheshimiwa mfalme, usifikiri kuwa baada ya kuteka Dola la Song utaweza kutawala daima, na watu watakubali siku zote bila kukupindua.”

Mfalme Chu mwishowe aliema, “Sitashambulia Dola la Song.” Mo Zi aliliokoa Dola la Song kwa akili zake.