Dola ya Zhao Yaokolewa kwa Kuzingira Dola ya Wei
中国国际广播电台


      Sun Bin alikuwa mtaalamu wa mbinu za kivita katika Enzi ya Madola ya Kivita nchini China yaani kuanzia mwaka 475 hadi 221 kabla ya kuzaliwa Kristo. Hapo awali Sun Bin na Pang Juan waliwahi kujifunza pamoja mbinu za kivita kutoka kwa mwalimu mmoja, na baadaye wote wawili waliihudumia Dola ya Wei. Lakini Pang Juan alimwonea kijicho Sun Bin kwa umahiri wake, alitumia hila kumtumbukiza hatiani, na hatimaye kumsababisha kupata adhabu ya kukatwa magoti. Baadaye Sun Bin alitoroshwa hadi kwenye Dola ya Qi na jemadari Tian Ji wa dola hiyo. Maelezo yafuatayo ni vita kati ya watu hao wawili, Sun Bin na Pan Juan.

Karne ya nne kabla ya kuzaliwa Kristo, katika China ya kale kilikuwa ni kipindi cha Enzi ya Madola ya Kivita. Miongoni mwa madola mengi, Dola ya Wei ilijipatia nguvu kubwa zaidi kwa kufanya mageuzi ya kisiasa. Dola hiyo kwa nyakati tofauti ilimeza baadhi ya madola madogo madogo na dhaifu. Wakati huo madola yaliyolingana na nguvu zake yalikuwa Dola ya Qi kwa mashariki yake, na Dola ya Qin upande wa magharibi yake, madola mengine mawili Zhao na Zhou yalikuwa madogo na dhaifu.

Mwaka 368 kabla ya kuzaliwa Kristo, kwa kusaidiwa na Dola ya Qi, Dola ya Zhao ilivamia Dola ya Zhou iliyokuwa chini ya himaya ya Dola ya Wei. Mfalme wa Dola ya Wei alimtuma jemadari wake Pang Juan na askari laki moja kwenda kuushambulia Han Dan, mji mkuu wa Dola ya Zhao. Kutokana na kuwa dhaifu, Dola ya Zhao iliiomba Dola ya Qi msaada. Waziri wa Dola ya Qi, Zhou Ji, alikataa kutoa msaada kwa kuhofia kuwa nguvu za dola zingedhoofishwa. Lakini waziri mwingine Duan Ganlun alikubali kwa kufikiri kuwa iwapo Dola ya Wei ikiishinda Dola ya Zhao, nguvu zake zitaongezeka, na itakuwa hatari kwa Dola ya Qi. Mfalme akakubali wazo la kuisaidia Dola ya Zhao, akamtuma Sun Bin na askari elfu 80 kwenda kuiokoa Dola ya Zhao.

Kabla ya kuendelea na habari hizo hebu nieleze hadithi moja inayoonyesha umahiri wa kivita wa Sun Bin:

Siku moja mfalme alimwuliza Sun Bin, “Kama majeshi mawili yaliyokabiliana medani, na yanalingana kwa nguvu, kwa hiyo hakuna moja linalothubutu kujitokeza kuanza kushambulia mwenzake, wakati huo utafanyaje?”

Sun Bin alijibu, “Chagua kamanda mmoja jasiri aongoze askari wachache aanze mashambulizi kupambana na maadui ana kwa ana, lakini anaruhusiwa kushindwa tu ili kuwarubuni maadui, huku askari hodari wakijificha ubavuni mwa maadui, na maadui wanapokuwa katika hali ya vurugu mashambulizi yafanyike, hivyo hakika utashinda.”

Sasa turudie kwenye hadithi yetu. Baada ya kufafanua hali ilivyo, Sun Bin aliona kuwa askari wa Dola ya Wei walikuwa na nguvu kubwa zaidi, na kama askari wa Dola ya Qi wakipambana nao uso kwa uso wangepata hasara kubwa, kwa hiyo ilikuwa vema kukwepa nguvu zao kubwa na kushambulia zile dhaifu. Wakati ambapo askari wote hodari wa Dola ya Wei walikuwa wamekwenda vitani nje ya dola na ulinzi wa ndani ulikuwa dhaifu, ni busara kuushambulia mji mkuu wa Dola ya Wei haraka haraka ili kulazimisha askari wa Dola ya Wei kurudi, na kwa kufanya hivyo Dola ya Zhao ingekombolewa.

Ili kutimiza mbinu hizo, Sun Bin kwa makusudi alituma kamanda na askari goigoi kushambulia mji mkubwa wa Dola ya Wei, Ping Ling, ili kuwafanya maadui wawe na mawazo ya kuwa askari wa Dola ya Qi ni dhaifu. Jemadari wa Dola ya Wei, Pang Juan, aliona askari wa Dola ya Wei hawafui dafu, basi aliendelea kushambulia Dola ya Zhao, hakutegemea kuwa askari wa Dola ya Qi wangevamia Da Liang, mji mkuu wa dola yake.

Sun Bin aliongoza askari wake kuuvamia mji mkuu wa Dola ya Wei kwa haraka. Pang Juan alipopata habari hiyo akarudisha askari wake mara moja kutoka kwenye medani. Kutokana na safari ndefu na kupiga mbio, askari na farasi walikuwa hoi, na njiani waliingia ndani ya mtego wa kuzingirwa na Sun Bin, wakasambaratika vibaya.

Kuacha nguvu kuu na kushambulia ile dhaifu, na kujilimbikizia nguvu na kuwashambulia maadui wanapokuwa hoi, ni mbinu licha ya kuisaidia Dola ya Zhao, tena ilidhoofisha nguvu za Dola ya Wei. Hii ndio mbinu ya kuiokoa Dola ya Zhao kwa kuivamia Dola ya Wei, ni mbinu maarufu katika historia ya mambo ya kijeshi ya China.