Vita vya Jing Xing
中国国际广播电台


       Katika China ya kale, yalikuwako madola mengi yaliyokuwa yakipigana miaka hadi miaka mpaka mwaka 221 K.K. ambapo Enzi ya Qin iliyameza madola yote madogo madogo na kuwa enzi ya kwanza ya utawala wa China nzima katika historia ya China. Lakini kutokana na unyonyaji mkubwa na hali mbaya ya maisha ya wananchi maasi mengi yalikuwa yakitokea huku na huko, ambapo mwaka 206 K.K. enzi hiyo ilipinduliwa. Miongoni mwa maasi mengi, mawili yaliimarika zaidi, moja liliongozwa na Xiang Yu, lingine lilikukwa la Liu Bang. Ili kuunyakua utawala wa China nzima Xiang Yu na Liu Bang walipigana karibu miaka mitano. Katika muda huo wa vita, alijitokeza jemadari mmoja katika jeshi la Liu Bang, aliyejulikana kama Han Xin ambaye ni maarufu katika historia ya China kwa busara yake ya kupigana vita. Leo katika kipindi hiki, nitawaeleza vita vya Jing Xing vilivyopiganwa na Han Xin dhidi ya jeshi la Xiang Yu.

Mwezi Oktoba mwaka 204 jemadari Han Xin aliongoza askari wake walioandikishwa karibuni kusafiri mbali, walivuka Milima ya Taihang wakitaka kuivamia Dola ya Zhao iliyokuwa chini ya himaya ya Xiang Yu. Mfalme na jemadari Chen Yu wa Dola ya Zhao walikusanya askari laki mbili na kuwapanga Jing Xing ambayo ilikuwa kipenyo chebamba kati ya magenge mawili wakiwa tayari kupambana nao kufa na kupona.

Kipenyo cha Jing Xing ni njia pekee ya askari wa Han Xin kuivamia Dola ya Zhao. Kipenyo hicho kina urefu wa kilomita 50 hivi na kutokana na ufinyu wake askari hawawezi kupita kwa wingi kwa wakati mmoja. Askari wa Dola ya Zhao walivamia sehemu ya kipenyo hicho mapema wakiwa katika sehemu ya juu na idadi kubwa ya askari, hali ambapo ilikuwa ya manufaa kwao. Askari wa Han Xin walikuwa elfu kumi tu; aidha, walikuwa wamesafiri sana, hivyo kuwafanya wachovu sana.

Mshauri Li Zuoche wa jemadari wa Zhao alipendekeza kwamba kwa upande mmoja askari wengi wapambane na jeshi la Han Xin kutoka mbele, na kwa upande mwingine askari wachache wawazunguke maadui kwa nyuma ili kukata njia ya huduma za chakula na kupammbana nao kutoka mbele na nyuma na kumkamata Han Xin akiwa hai. Lakini jemadari Chen Yu alikuwa hodari wa kupambana na maadui uso kwa uso, aliamini nguvu zake kubwa zingetosha kabisa kuwashinda maadui, hivyo alikataa ushauri wake.

Han Xin alifahamu vema kuwa nguvu zake ni hafifu sana kulingana na jeshi la Zhao, kwa hiyo akipambana nao uso kwa uso alikuwa na uhakika wa kushindwa. Basi Han Xin aliwaweka askari wake mbali kutoka kipenyo cha Jing Xing, huku akichambua sura ya ardhi na mpangilio wa askari wa Dola ya Zhao mpaka ilipobainika kuwa jemadari Chen Yu wa Dola ya Zhao ana mawazo ya kudharau maaduni na kutaka kupata ushindi kwa haraka. Kutokana na uchambuzi huo akaamrisha askari wake wapige kambi umbali wa kilomita 15 karibu na kipenyo.

Usiku wa manane, Han Xin alichagua askari hodari elfu mbili, na kumwagiza kila mmoja achukue bendera moja ya jeshi lao, kwa kutumia giza la usiku wazunguke na kuficha nyuma ya kambi ya askari wa Zhao mpaka siku ya pili ambapo askari wa Zhao watakuwa wametoka na kuacha kambi tupu ndipo washambulie kambi yao na kuchoma bendera za jeshi lao badala bendera ya kijeshi ya Dola ya Zhao.

Baada ya maandalizi hayo yote, Han Xin aliamrisha kufanya mashambulizi, wakati askari wa Han Xin walipofika kwenye mlango wa kipenyo kulikuwa kumepambazuka. Jemadari Chen Yu wa Dola ya Zhao pia alikuwa amekwishakusanya askari wake kwenye kipenyo. Alipoona kuwa askari wa Han Xin ni wachache na yeye alikalia sehemu nzuri kwa vita, akaamrisha askari wake watoke wote kambini kupambana nao. Pande mbili zilipigana kwa nusu siku lakini jeshi la Zhao halikupata ushindi.

Wakati huo kambi ya askari wa Zhao ilikuwa karibu tupu, askari wa Han Xin kiasi cha elfu mbili waliokuwa wamejificha wakaingia kwa ghafla kambini wakachoma bendera zao za kijeshi kila mahali, kisha wakapiga ngoma na kelele kwa nguvu. Askari wa Zhao kwa mshituko wakaona bendera za maadui zikipepea kila mahali kambini, safu zao za mapambano zikavurugika. Kwa kutumia fursa ya vurugu hiyo askari wa Han Xin walifanya mashambulizi makali, wakawasambaratisha vibaya askari wa Zhao, jemadari wao Chen Yu aliuawa, na mfalme wa Dola ya Zhao alikamatwa akiwa hai.

Vita vya Jing Xing vinaeleza jinsi Han Xin alivyowashinda maadui laki mbili kwa askari wake wachache kutokana na busara yake ya kutumia jeshi. Ameacha kumbukumbu nzuri katika historia ya kijeshi ya China.