Cao Gui aongoza jeshi kupambana na dola la Qi
中国国际广播电台


        Kwa kawaida vita ni mapambano ya wanajeshi, lakini katika historia ya China alikuweko raia mmoja ambaye aliongoza jeshi kushinda maadui, raia huyo alijulikana kwa jina la Cao Gui. Basi katika kipindi hiki nimewaletea masimulizi yake.

Katika China ya kale yalikuwako madola mengi kwa pamoja ambayo yalipigana vita kwa miaka mingi yakinyang'anyana ardhi, kipindi hiki kinajulikana kama Madola ya Kivita katika historia ya China. Dola ya Qi ilikuwa moja ya madola hayo.

Mfalme wa Dola ya Qi, Qi Henggong, kwa kutegemea nguvu zake kubwa za kijeshi, mwaka 684 K.K. alianza kuvamia Dola dhaifu ya Lu. Lakini mfalme wa Lu alipania kupambana kufa na kupona.

Wananchi wa Dola ya Lu wlihamaki kutokana na hila za Dola ya Qi. Alikuwako raia mmoja aliyejulikana kama Cao Gui, alitaka kuonana na mfalme na kuomba ashiriki katika vita dhidi ya Dola ya Qi. Baadhi ya watu walimshauri wakisema, “Mambo ya kitaifa yanashughulikiwa na wakubwa, unajisumbua nini wewe kabwera?”

Cao Gui aliwajibu, “ Wakubwa huwa na maono ya karibu karibu, pengine hawana njama za busara. Nawezaje kukaa bure bila kutenda lolote wakati taifa letu linapokuwa hatarini?” Kisha akaenda kuomba kuonana na mfalme wake Lu Zhuanggong.

Cao Gui alieleza ombi lake la kushiriki katika vita dhidi ya Dola ya Qi, huku alimsaili mfalme, “Dola yetu ni dhaifu, unatemegea nini ili uweze kuishinda Dola ya Qi?”

Mfalme Lu Zhuanggong akamjibu, “Nilipokuwa na chakula na nguo nzuri sikuzitumia peke yangu bali nilizigawa kwa wengine. Kutokana na hayo nadhani wangeniunga mkono.”

Kusikia hayo Cao Gui alitikisa kichwa akisema, “Hayo ni mambo madogo tu, na watu waliofaidika kutoka kwako pia ni wachache, raia hawawezi kukuunga mkono kwa sababu hiyo.”

Mfalme aliendelea kusema, “Mbali ya hayo, kila mara nilipoabudu nilifanya hivyo kwa moyo safi.”

Cai Gui akacheka na kusema, “Kuabudu kwa moyo safi ni lazima kwa kila muumini, mungu pia hatakusaidia chochote katika vita.”

Mfalme akakaa kimya kwa kitambo akichemsha ubongo kujitafutia sababu za kuungwa mkono, kisha akasema, “Raia wanapokabiliwa na mashitaka mimi hufanya uamuzi wa haki ingawa siwezi kusema kuwa kila shitaka nililifanyia uchunguzi vilivyo na sikukosea hata kidogo katika uamuzi wangu.”

Cao Gui aliinamisha kichwa akisema, “Hilo ni jambo linalohusu na raia, kwa sifa yako hiyo naona unaweza kuishinda Dola ya Qi.”

Cao Gui aliomba kushiriki kwenye vita pamoja na mfalme. Mfalme akakubali kwa kuona kuwa ana uhakika wa kuwashinda maadui. Watu wote wawili, mfalme na kabwela Cao Gui walipanda mkokoteni mmoja wa kivita na kuanza safari pamoja na askari.

Katika zama za kale nchini China vita vilikuwa vya uso kwa uso, baada ya pande mbili kuwa tayari, upande wa A unapiga ngoma kuashiria kuanza kwa mapambano, na upande wa B nao pia unapiga kuitikia. Ikiwa upande wa B haukupiga kuitikia, basi upande wa A utapiga tena mara ya pili hata mara ya tatu ambayo ni ya mwisho kabla ya kufanya mashambulizi. Sasa turudie kwenye vita vya Qi na Lu. Pande mbili zilipanga askari tayari katika sehemu ya Lai Wu ambapo iko mkoani Shangdong ya leo, kutokana na askari wa Qi kuwa wengi walitangulia kuvumisha ngoma kwa mara ya kwanza ili kuharakisha kufanya mashambulizi. Wakati huo mfalme wa Lu alitaka kutoa amri ya kupiga ngoma ya kuitikia na kuanza mapambano, lakini Cao Gui alimzuia, akisema, “A,a, usiwe na pupa, wakati bado.”

Askari wa Dola ya Qi walivumisha ngoma mara ya pili, lakini Cao Gui alimwambia mfalme wake awatulize askari wake. Kuona jinsi askari wa Qi walivyojivuna, askari wa Dola ya Lu walijawa na munkar na jazba ya kupambana nao mara moja, lakini mfalme pia hakutoa amri, kwa hiyo walilazimika kustahimili.

Jemadari wa askari wa Qi alipoona askari wa Lu ni kimya, akaamrisha kupiga ngoma mara ya mwisho, kwa kudhani kuwa askari wa Lu ni wawaoga, na kuwakimbilia askari wa Lu kwa ujeuri.

Wakati huo Cao Gui akamwambia mfalme wake, “Sasa ni wakati wa kupambana nao.”

Ngoma zilivumishwa kwa nguvu, askari wa Lu waliojawa na mori wakawashambulia askari wa Qi mfano wa simba. Askari wa Qi hawakutegemea askari wa Lu kuwa wakali kiasi hicho, mara safu zao zikavurugika.

Mfalme wa Lu alipowaona maadui wakimbia ovyo kuokoa maisha yao akataka kuwaamrisha askari wake kuwafukuza, lakini alizuiliwa na Cai Gui: “Usifanye haraka.” Kisha akashuka kutoka kwenye gari lake la kivita, akainamisha kichwa kuangalia alama za magurudumu ya mikokoteni ya kivita, baadaye akaparamia kwenye kilele cha mlingoti wa bendera wa mkokoteni wa kivita kuangalia mbali aone jinsi maadui walivyokimbia. Baada ya yote hayo ndipo alipomwambia mfalme, “Haya, waambie askari wako wawafukuze maadui.”

Amri ilipotolewa tu mara askari wa Lu wakawakimbilia maadui kwa mbio ilimradi kila mmoja asikubali kuachwa nyuma, na kuwafukuza maadui nje kabisa ya dola ya Lu.

Kitendo cha Cao Gui kuongoza vita kwa utulivu kilimpa picha nzuri mfalme wake. Baada ya kurudi kwenye kasri na kumsifu kwa maneno machache mfalme alimwuliza Cao Gui, “Kwa nini ulikataa kuanza kupambana na maadui ngoma zilipopigwa mara ya kwanza na ya pili mpaka mara ya tatu tu?”

Cao Gui akamwambia, “Kupigana vita kunategemea moyo mshupavu. Maadui walipopiga ngoma kwa mara ya kwanza walikuwa na ushupavu wa kutosha, mara ya pili ushupavu wao ukapungua na mara ya tatu ushupavu wao ukatoweka kabisa. Kinyume chake, askari wetu wakati huo walikuwa wamejawa na ushupavu mkubwa, na askari wakiwa katika hali hiyo hakika watashinda.”

Mfalme alimwuliza zaidi kwa nini aliwakawiza askari kuwafukuza. Cao Gui akajibu, “Ingawa askari wa Dola ya Qi walikimbia kwa kushindwa, lakini dola yao ni kubwa na nguvu ni kubwa, pengine walijidai kushindwa lakini askari walificha njiani, ni busara kuchukua tahadhari na hali hiyo. Baadaye niliona bendera zao zikiwa zimeshikwa kiholela na alama za magurudumu ya mikokoteni ya kivita zilikuwa ovyo, ndipo nikabaini kuwa kweli walivurugika kwa kushindwa. Hapo ndipo nilipokuambia uwaamrishe askari wawafukuze.”

Mfalme aliposikia hayo akazibuka, akamsifu Cao Gui kuwa mtu makini sana.