Vita vya Bai Ju
中国国际广播电台


       “Mbinu za Kivita” zilizoandikwa na Sun Wu ni maandishi maarufu ya kijeshi duniani katika China ya kale. Leo katika kipindi hiki nawaletea maelezo kuhusu vita vilivyopiganwa Bai Ju, vita vilivyoongozwa na mwandishi huyo mwenyewe.

Wu na Chu ni madola mawili katika Enzi ya Madola ya Kivita katika karne ya 6 kabla ya kuzaliwa Kristo. Ili kujipatia umaarufu wa utawala, madola hayo mawili yalipigana vita vikubwa mara kumi katika muda wa miaka 70 tangu mwaka 584 hadi 514 kabla ya kuzaliwa Kristo. Mwaka 515 kabla ya kuzaliwa Kristo, He Lu alinyakua kiti cha enzi ya Dola ya Wu, ambapo alitaka kuwa mbabe wa kutawala dunia baada ya kuwa mfalme. Aliendeleza uchumi na kuongeza nguvu za majeshi, alimteua Sun Wu kuwa jemadari wa kufundisha mbinu za kivita majeshi yake. Kweli baadaye Dola ya Wu ikajitokeza kwa kuwa na uchumi mzuri na nguvu kubwa za kijeshi.

Chu ilikuwa dola nyingine kubwa katika sehemu ya kusini ya China, ni dola ambayo iliwahi kupora ardhi nyingi za madola mengi madogo madogo. Lakini baada ya Zhao Wang kurithi kiti cha ufalme mwaka 516, kutokana na uozo wa utawala na kupambana na madola mengine, nguvu za dola hiyo zilikuwa zimefifia zaidi na zaidi. Mwaka 512 kabla ya kuzaliwa Kristo hali hiyo ya udhaifu ilimfanya mfalme He Lu wa Dola ya Wu kuwa na uchu wa kutaka kuivamia Dola ya Chu baada ya kuyaweka madola madogo madogo yaliyopakana nayo chini ya utawala wake.

Lakini Sun Wu aliona kwamba eneo la Dola ya Chu ni kubwa na watu wake ni wengi, ingawa hali yake si nzuri kama zamani, lakini nguvu zake za kijeshi bado ni kubwa, wakati ambapo Dola ya Wu imechoka kutokana na vita vingi mfululizo na gharama nyingi zilizotumika katika vita. Kwa hiyo aliona haifai kufanya uvamizi mpaka hali ipevuke. Ili kupevusha hali mapema Sun Wu alishauri kwamba majeshi ya Dola ya Wu yagawanyike katika vikundi vitatu na kupeana zamu kuchokoza majeshi ya Dola ya Chu mipakani.

Mfalme He Lu wa Dola ya Wu alikubali ujanja huo wa Sun Wu. Kila baada ya muda kikundi kimoja hufanya uchokozi mpakani, na mfalme wa Dola ya Chu bila ya kuchunguza hali iliyo, mara akatuma askari wake wengi kwenda huko, lakini walipofika kikundi cha askari wa Dola ya Wu kiliondoka, kisha baadaye kikundi cha pili kikaja tena na uchokozi mpakani, basi mfalme wa Dola ya Chu akatuma tena askari wake kwa wingi. Vivyo hivyo askari wa Dola ya Wu hawakuacha kufanya uchokozi katika muda wa miaka 6, wakawachosha askari wa Dola ya Chu, na kuifanya dola hiyo kupoteza mali nyingi na nguvu za kijeshi kufifia sana.

Mwaka 506 kabla ya kuzaliwa Kristo, Sun Wu aliona hali ya kuivamia Dola ya Chu imepevuka, lakini kutokana na askari wa Chu kuwa bado wengi mara kadhaa kuliko askari wa Wu, Sun Wu alitumia mbinu ya kufanya mashambulizi kwa ghafla. Alichagua askari hodari elfu kadhaa kunyemelea kwa mwendo wa haraka sehemu ya mpakani mwa Dola ya Chu.

Baada ya kupata habari hiyo mfalme wa Dola ya Chu ambaye hakuwa amejiandaa aliwatuma majemadari Nang Wa na Shen Yirong kwa haraka kwenda kwenye medani na askari wote. Askari wa madola hayo mawili walipambana kufa na kupona katika sehemu ya Bai Ju. Shen Yirong aliamua kuongoza jeshi kuu kupambana na maadui na Nang Wa akaongoza askari wachache kuchukua njia nyingine na kuwazunguka kwa nyuma maadui ili wawashambulie maadui kutoka mbele na nyuma na kuwaangamiza kwa pigo moja. Hii ilikuwa njia nzuri ya kushinda askari wa Dola ya Wu. Nang Wa akakubali, lakini baada ya Shen Yirong kuondoka na askari wake, Nang Wa alighairi kwa kusikiliza ushauri wa maofisa wake kuwa akitekeleza mpango huo na kupata ushindi wa vita, Shen Yirong angejipatia sifa nyingi, kwa hiyo alijiamulia mwenyewe kufanya ushambulizi kwa askari wa Dola ya Wu bila ya matayarisho ya kutosha, na matokeo yakawa ni kulishindwa vibaya.

Baada ya kusikia kwamba askari wa Nang Wa wamesambaratika, Shen Yirong kwa haraka akaongoza askari wake kuja kuwasaidia. Lakini kwa kuongozwa na Sun Wu askari wa Dola ya Wu waliwazingira askari wa Shen Yirong. Kutokana na kushindwa kuvunja ngome, jemadari Shen Yirong alimwamrisha askari amkate kichwa chake na kwenda nacho kupiga ripoti kwa mfalme wake Chu kama kuomba msamaha.

Mfalme wa Dola ya Chu, aliposikia kwamba askari wake wamesambaratika, bila kujali upinzaji wa mawaziri wake, na maisha ya wananchi, aliukimbia kimya kimya mji mkuu pamoja na jamaa zake. Habari hiyo ilipofika kwenye medani askari wa Dola ya Chu wakakata tamaa ya kuendelea na mapambano, jeshi la Dola ya Wu likanyakua mji mkuu wa Dola ya Chu. Baadaye waziri mmoja wa Dola ya Chu alitorokea Dola ya Qin ambayo ilikuwa na nguvu sana wakati huo, na kutokana na ombi lake mfalme wa Qin alituma askari wake kuvamia Dola ya Wu, ambapo iliibidi dola hiyo kurudisha askari wake kutoka Dola ya Chu ili kujihami.

Vita vya Bai Ju ni mfano mzuri wa askari wachache kushinda askari wengi na kupata ushindi kwa haraka. Mwanzoni mwa vita hiyo Dola ya Wu ilikuwa na askari elfu 30 tu wakati Dola ya Chu ilikuwa na askari laki mbili. Lakini kutokana Dola ya Chu kutoandaa majeshi yake kwa busara na mbinu ya kivita kuwa potovu, ilishindwa.