Karamu ya Hong Men
中国国际广播电台


     Katika China ya kale, yalikuwako madola mengi yaliyokuwa yakipigana miaka hadi miaka, kwa hiyo pia ziko hadithi nyingi ambapo wadhaifu walishinda wenye nguvu na wenye busara waliwashinda wajasiri. Leo katika kipindi hiki nimewaletea hadithi nyingine iitwayo “Karamu ya Hong Men”.

Enzi ya Qin ni ya kwanza katika historia ya utawala wa China nzima mwaka 221 K.K. Kutokana na unyonyaji mkubwa na hali mbaya ya maisha ya wananchi maasi mengi yalikuwa yakitokea huku na huko. Kutokana na maasi hayo, majeshi mawili yaliimarika zaidi: Moja liliongozwa na Xiang Yu ambaye alikuwa jemadari wa Enzi ya Qin, lingine lilikuwa la Liu Bang ambaye alikuwa afisa mdogo wa Enzi ya Qin.

Xiang Yu alikuwa mjeuri na machachari lakini hodari wa kupigana vita, ukali wake ulijulikana kwa wote; Liu Bang alikuwa mjanja lakini hodari wa kuchagua watu wake. Wote wawili waliungana pamoja wakisaidiana katika vita dhidi ya Enzi ya Qin, na nguvu zao zilikuwa kubwa zaidi. Walikubaliana kuwa yeyote atakayetangulia kuteka Xian Yang, mji mkuu wa Enzi ya Qin angekuwa mfalme.

Mwaka 207 K.K. Xiang Yu alipopambana na jeshi kuu la Enzi ya Qin katika sehemu ya Ju Lu na kushinda, wakati huo Liu Bang alikuwa ameuteka mji mkuu Xian Yang, lakini kutokana na ushauri aliopewa hakuingia mjini, bali alisimamisha jeshi lake nje ya mji, na kuweka kasri ya mfalme na ghala ya fedha ya taifa chini ya ulinzi wake, huku akiwafariji wakazi wa mji huo. Wakazi walimwona Liu Bang kama ni mpole na askari wakifuata nidhamu barabara bila kuwatesa ovyo, wakampendekeza kuwa mfalme.

Xiang Yu alipopata habari kuwa Liu Bang alikwishauteka mji wa Xian Yang alikasirika sana, na kwa haraka akaongoza askari wake laki 4 kwenda Hong Men, karibu na Xian Yang, tayari kuunyakua mji huo. Jemadari wake Fan Zeng akisema, “Liu Bang ni mshabiki wa mali tena ni mtu wa kupenda wanawake, lakini sasa hataki hata senti wala mrembo, hakika ana hila kubwa, ni busara tumchinje kabla hajaimarika.”

Habari ilipomfikia Liu Ban, mshauri wake Zhang Liang alichambua kwamba sasa askari wa Liu Ban walikuwa laki moja tu, nguvu ni dhaifu, haifai kupambana na Xiang Yu moja kwa moja. Hivyo mshauri huyo alikwenda kumwomba rafiki yake ambaye ni baba mdogo wa Xiang Yu aende kuomba msamaha kwa Xiang Yu. Kisha Liu Bang akiwa pamoja na Zhang Liang na jemadari Pan Hui alikwenda Hong Men, akamwambia Xiang Yu kwamba yeye alikuwa analinda tu ule mji wa Xian Yang akimsubiri aende huko kuwa mfalme. Kusikia hayo Xiang Yu alifurahi na kumwamini, akamwandalia karamu. Jemadari Fan Zeng aliketi kando ya Xiang Yu, kwa mara kadhaa alimwashiria amwue Liu Bang, lakini Xiang Yu alijifanya hana habari, basi ilimbidi amwagize jemadari Xiang Zhuang ajifanye kucheza ngoma ya upanga kama kibwagizo cha kufurahia karamu mbele ya Liu Bang ili apate fursa ya kumwua. Kuona hali hiyo, baba mdogo wa Xiang Yu akainuka na kucheza ngoma ya upanga pamoja naye huku akimkinga Liu Bang kwa mwili wake, hivyo Xiang Zhuang hakupata nafasi ya kumwua. Wakati huo Zhang Liang aliyekuwa mshauri wa Liu Bang, kwa haraka akampasha habari jemadari Pan Hui. Mara Pan Hui akiwa na upanga na ngao akajitoma ndani ya hema na kumfokea Xiang Yu, akisema, “Liu Bang ndiye aliyeuteka mji wa Xian Yang, lakini hakuingia ndani bali anakungojea uwe mfalme. Mtu mwema na mwenye sifa kubwa kama huyo wewe badala ya kumzawadia kwa cheo unawasikiliza watu duni kutaka kumwua!” Baada ya kusikia hayo Xiang Yu aliona haya. Kwa kutumia nafasi hiyo, Liu Bang alijidai kwenda nje kujisaidia, akakimbilia moja kwa moja kwenye kambi yake pamoja na wafuasi wake. Mshauri Fan Zeng alipoona Xiang Yu jinsi alivyositasita akawa amemwachia huru Liu Bang, akakasirika, huku akinung'unika, “Xiang Yu hatafanikiwa chochote! Liu Bang ni mjanja, dunia hakika itakuwa yake, mtaona tu.”

Ndugu wasikilizaji, hii ndio hadithi ya “Karamu ya Hong Men” ambayo ni maarufu katika historia ya China. Xiang Yu alijivunia nguvu zake kubwa, na alimwamini Liu Bang akampatia nafasi ya kutoroka. Baadaye Xiang Yu alijitawaza kuwa “kabaila wa Xi Chu” ambaye alikuwa kama mfalme, na alimteua Liu Bang kuwa “mfalme wa Han” ambaye alikuwa kama mtoto wa mfalme wa kutawala sehemu ya mbali isiyokuwa na watu wengi. Ilikuwa si muda mrefu baadaye, Liu Bang alitumia wakati Xiang Yu alipokuwa akivamia sehemu nyingine, aliuteka mji mkuu wa Xian Yang. Basi tokea hapo Xiang Yu na Liu Bang walianza kupambana “vita vya Chu na Han” kwa muda wa karibu miaka mitano. Xiang Yu alikuwa na nguvu zaidi, alishinda Liu Bang mara nyingi, lakini kutokana na ukatili wake na jeshi lake kuwaua raia na kuchoma nyumba zao ovyo, alipoteza imani ya wananchi na nguvu zake za kijeshi zikafifia siku hadi siku. Kinyume cha hali hiyo, Liu Bang alitilia maanani kuungwa mkono na wananchi na alikuwa hodari wa kuchagua watu wake, nguvu zake zikaongezeka zaidi, mwishowe alipata ushindi.

Mwaka 202 K.K. Liu Bang na askari wake waliwazingira askari wa Xiang Yu katika Hai Xia yaani Ling Bi jimboni An Hui kwa leo. Baada ya kuvunja zingio Xiang Yu alifukuzwa na askari wa Liu Bang, na alijiua baada ya kukosa njia nyingine. Liu Bang akawa mfalme, na enzi ya pili ya utawala wa China nzima yaani Enzi ya Han ikaanza.