Mwanzilishi wa Utawala wa Kiini Kimoja, Qin Shihuang
中国国际广播电台

 
      Qin Shihuang ni mwanzilishi wa utawala wa kiini kimoja nchini China. Mwishoni wa kipindi cha madola ya kivita (225—222 K.K.) madola yaliyobaki yalikuwa saba yenye nguvu, nayo ni Qin, Chu, Qi, Yan, Han, Zhao na Wei. Kati ya madola hayo dola la Qin lilikuwa na nguvu zaidi. Tokea mwaka 236 K.K. hadi 221 K.K. dola hilo kwa nyakati tofauti liliyateka madola mengine sita na kusisisi nchi ya kwanza yenye muungano na utawala wa kidikteta wenye kiini kimoja katika historia ya China, Enzi ya Qin.

Mwaka 221 K.K. Qin Shihuang alifanikisha lengo lake la kuiunganisha China. Tokea hapo historia ya China yenye madola mengi ya kujitawala ilikuwa imemalizika na badala yake imekuwa nchi yenye kiini kimoja cha utawala.

Muungano wa China ulioletwa na Qin Shihuang una maana kubwa na ni mchango mkubwa katika historia ya China. Kwanza, kwa upande wa siasa mfalme Qin Shihuang alibatilisha mfumo wa kila sehemu kujitawala na badala yake aliigawa China katika mikoa 36, na chini ya mikoa aliweka wilaya, maofisa wa ngazi zote aliwachagua au kuwaachisha kazi yeye mwenyewe, na maofisa hawakuruhusiwa kurithisha nyadhifa zao. Mfumo huo wa utawala ulioanzishwa katika enzi ya Qin uliendelea kutumika katika historia yote ya kimwinyi, kwa miaka zaidi ya elfu mbili nchini China, na baadhi ya majina ya wilaya yalitumika katika enzi ya Qin yanatumika hadi leo. Kadhalika, Qin Shihuang pia alisawazisha upimaji, kwani upimaji wa urefu, uzito na ujazo ulikuwa tofauti katika kipindi cha madola ya kivita na tofauti hizo zilikwamisha uchumi. Mfalme Qin Shihuang pia alisawazisha sarafu na kuzifanya sheria ziwe za namna moja, hivyo alikuwa ameleta hali nzuri ya kuendeleza uchumi na pia kutilia mkazo utawala wake wenye kiini kimoja nchini China.

Ili kuwapumbaza kimawazo watu wake alitumia hata sera ya kuchoma moto vitabu ambavyo havikuliangana na mawazo yake ya utawala na kuwatesa wasomi wa Confucius; pia watu ambao walitofautiana naye kimawazo aliwazika wakiwa hai ili kudumisha utawala wake. Pamoja na hayo mfalme huyo aliamrisha kujenga na kukarabati kuta zilizojengwa na madola ya Qin, Zhao, Yan na madola mengine na kuziunganisha kuwa ukuta mmoja mrefu. Zaidi ya hayo alitumia fedha nyingi na watu laki 7 kujijengea kaburi lake. Mwezi Julai mwaka 210 K.K. Qin Shihuang alifariki.