Yao na Shun
中国国际广播电台


Kiasi cha miaka 4000 iliyopita, walitokea watu kadhaa mashuhuri, Yao, Shun, Da Yu na wengine. Yao na Shun walikuwa ni wafalme wawili wa mwanzo kabisa nchini China katika masimulizi ya mapokeo, watu hao wawili ndio walioanzisha historia ya China. Katika vitabu vingi vya hekaya na masimulizi ya mapokeo, kuna mengi yaliyoeleza kuhusu Yao na Shun.

Yao alikuwa ni mtemi mwishoni mwa jamii ya kiasili, ni mwakilishi wa utamaduni wa mwanzo kabisa nchini China. Kutokana na masimjulizi ya mapokeo, Yao alikuwa ni kizazi cha babu wa taifa la China Huangdi, alikuwa mtu mwenye akili, roho nzuri na aliheshimiwa sana. Alipokuwa na umri wa miaka 16 aliendekezwa kuwa mtemi. Watu wa kabila la Yao waliishi katika sehemu ya kaskazini ya China, mji wa Baoding mkoani Hebei wa sasa. Kwa kushirikisha makabila mengine yaliyoko katika sehemu yake alipigana na wavamizi na kuwapokea kuwa watu wa kabila lake. Kutokana na nguvu za kabila lake kuongezeka haraka, Yao alikuwa mkuu wa muungano wa makabila kadhaa, watu wa baadaye walimwita mfalme Yao.

Yao alikuwa mfalme mwema, aliishi kama raia wa kawaida na kutenda mambo kwa uadilifu. Alithamini sana maofisa walio wema, alikagua maofisa wake kazi walizofanya na kuwasifu wale walio bora na kuwaadibu walio wabaya. Kutokana na hayo, kazi za utawala wake zilikuwa na utaratibu mwema. Aliweka ofisa wa unajimu ili watu waweze kushughulika na kilimo kwa misimu, watu wa kale wa China walisema, kipindi cha utawala wa Yao kilikuwa kipindi cha maendeleo ya haraka katika kilimo. Yao alikuwa anatilia maanani sana uhusiano mwema kati ya makabila na kuwashawishi watu wake waishi kwa majirani wema, hali ya jamii ilikuwa tulivu na ilijaa upendo.

Yao alikuwa madarakani kwa miaka 70, alikuwa mfalme wa kwanza kabisa kumwachia mrithi wake kiti cha ufalme kwa mujibu wa uhodari wa mtu.

Inasemekana kwamba aliwataka watu na maafisa wa sehemu mbalimbali wawapendekeze watu walio hodari, hata mtu huyo akiwa hana hadhi katika jamii. Mwishowe watu walimpendekeza mtu mmoja maskini aliyeitwa Shun. Inasemekana kwamba wazazi walikuwa wakali kwa Shun na ndugu zake pia walikukwa wajeuri kwa Shun, lakini Shun aliishi nao vema. Watu waliona kuwa Shun ni mtoto mwema kwa wazizi na ni mwenye maadili mema, alistahili kuwa mtawala na anaweza kuongoza vivuri taifa. Yao alimchunguza kwa pande zote, aliona kuwa Shun kweli ni mtu mwenye maadili mema na pia ni hodari. Baada ya miaka mitatu alimwachia Shun kiti chake cha ufalme badala ya kumwachia mtoto wake Dan Zhu. Kitendo hicho kisichokuwa na tamaa binafsi kwa ajili ya maslahi ya wananchi, kinasifiwa kuwa ni demokrasia ya mwanzoni kabisa nchini China.

Baada ya kuwa mfalme, Shun alistawisha zaidi siasa ya demokrasia. Alitunga sheria ya adabu na adhabu, aliwateua maofisa wa kazi mbalimbali kusimamia mambo ya utawala, uchumi, elimu, shughuli za bidhaa za kazi ya mikono, muziki, na pia alitunga sheria ya kuwachunguza maofisa, hivyo utaratibu wa utawala wa taifa ulizidi kukamilika kwa kiasi kikubwa.

Shu alitilia mkazo katika uzalishaji, uchimbaji wa mifereji na visima, na kuweka urafiki na watu wengi. Katika kipindi cha utawala wa Shun kilimo na ufundi vyote vilipata maendeleo ya kasi. Shun alikuwa mfano wa maadili mema kwa vitendo, alishirikiana na wananchi katika dhiki na faraja. Katika kipindi cha utawala wake watu walikuwa na maadili mema, watiifu, na waliishi bila usumbufu, kipindi chake kilikuwa kipindi chenye siasa bora, uzalishaji mkubwa na ustawi wa muziki. Kuhusu urithi wa kiti cha ufalme, Shun pia alitumia njia kama ya mfalme Yao, alimwachia kiti chake Yu (Da Yu), mtu aliyetoka mchango mkubwa katika shughuli za kupambana na mafuriko.