中国国际广播电台
Mtu
yeyote anapozungumzia utamaduni
wa China hawezi kuacha kumtaja
Confucius. Kwenye miaka ya
70 ya karne iliyopita, msomi
mmoja wa Marekani alipoorodhesha
watu 100 wenye taathira kubwa
kabisa katika historia ya
dunia, Confucius alipangwa
wa tano, nyuma tu ya Yesu,
mwanzilishi wa dini ya Buddha,
Sakyamuni, na wengine wawili.
Lakini miongoni mwa watu wa
China, Confucius ni wa kwanza
kabisa, kwani kila mmoja hakika
ameathiriwa na fikra zake
kwa kiasi fulani.
Katika miaka zaidi ya 200
iliyopita nchini China, fikra
za Confucius sio tu zilikuwa
zikiathiri sana siasa na utamaduni,
bali pia ziliathiri fikra
za kila Mchina, kiasi kwamba
hata baadhi ya wasomi wa nchi
nyingine walidhani kuwa fikra
za Confuciusi ni imani ya
dini fulani nchini China.
Lakini kwa kweli fikra za
Confucius zilikuwa ni moja
tu ya falsafa kadhaa zilizokuwepo
katika China ya kale, ni aina
ya falsafa, na wala haikuwa
imani ya dini. Hata hivyo
katika jamii ya kimwinyi ya
miaka zaidi ya 2000 nchini
China fikra zake zilikuwa
zimetukuzwa kama ni fikra
sahihi kabisa na zilikuwa
na heshima ya kipekee. Fikra
za Confucius sio tu zimeathiri
kwa kina utamaduni wa China
bali pia nchi nyingi za Asia.
Hadi leo, kwa sababu Wachina
wametapakaa kila pembe ya
dunia, fikra za Confucius
pia zimevuka China na Asia,
na kuenea duniani kote.
Confucius alizaliwa mwaka
551 K.K. na kufariki mwaka
479 K.K., aliishi kabla ya
msomi maarufu wa Ugiriki ya
kale, Aristotle, kwa zaidi
ya miaka 100. Alipokuwa na
umri wa miaka mitatu Confucius
alifiwa na baba yake, kisha
yeye pamoja na mama yake wakaweka
makazi yao katika mkoa wa
sasa Shandong uliopo mashariki
mwa China. Jina lake la ukoo
kwa Kichina ni Kong na jina
lake ni Qiu, Wachina humwita
“Kong Zi” kwa heshima. Katika
jamii ya China ya kale mbele
ya jina la ukoo likiongezewa
neno “Zi” ina maana ya heshima
kwa mtu huyo.
Zama alizoishi Confucius
zilikuwa ni kipindi cha “Spring
na Autumn” katika historia
ya China. Katika kipindi hicho
China iliyoungana ilisambaratika
na kuwa madola mengi madogo
madogo, na dola alilokuwa
akiishi liliitwa Dola la Lu,
dola ambalo lilistawi zaidi
kiutamaduni kuliko madola
mengine.
Maishani mwake, Confucius
hakuwahi kuwa afisa mkubwa,
lakini alikuwa na elimu kubwa.
Katika China ya kale waliokuwa
na fursa maalumu ya kupata
elimu walikuwa ni watu kutoka
familia za kitajiri tu. Lakini
Confucius alivunja utaratibu
huo, na alipokea wanafunzi
bila kujali wanatoka katika
familia gani, ikiwa tu watalipa
vitu, ikiwa kama ni karo.
Confucius aliwaelimisha wanafunzi
msimamo wake wa kisiasa na
nadharia yake. Inasemekana
kuwa jumla walikuwepo wanafunzi
elfu 3, na kati ya hao waliibuka
wanafikra kadhaa wakubwa kama
Confucius, ambao walirithi
na kuendeleza fikra zake na
kuzieneza sana.
Lakini je, ni kwa nini fikra
za Confucius zilienziwa mpaka
zikashika nafasi ya utawala
katika zama za kimwinyi nchini
China? Hili ni suala ambalo
haliwezi kuelezwa kwa maneno
machache. Lakini kwa kifupi,
fikra zake zilizowagawa watu
katika matabaka tofauti na
mageuzi yake ya kisiasa yalilingana
na manufaa ya tabaka la utawala,
na katika zama hizo fikra
zahizo zilileta matokeo ya
kutuliza na kuendeleza jamii.
Confucius alitilia sana mkazo
katika utaratibu wa maadili,
akiona kwamba ni kosa kubwa
kwa watu wa chini kutowaheshimu
wakubwa, au watoto kutowaheshimu
baba zao. Kutokana na nadharia
yake, jukumu la wafalme ni
kutawala vyema taifa na jukumu
la raia ni kutii wafalme.
Pengine mmoja anaweza kuwa
na nafasi kadhaa kwa pamoja,
maana pengine yeye ni mwana
na huku ni baba wa mtu, na
labda pia ni afisa, lakini
kutokana na mazingira tofauti
anapaswa ajiweke katika nafasi
yake. Hivyo taifa litakuwa
shwari, maisha ya raia yatakuwa
ya utulivu.
Nadharia ya Confucius ilipoibuka
haikuwa wazo tawala mara moja
hadi kabla ya karne ya pili,
China ilipokuwa nchi ya muungano
yenye kiini kimoja cha madaraka
na ilistawi kwa nguvu. Wakati
huo watawala waliona kuwa
nadharia ya Confucius inasaidia
sana kuleta utulivu wa jamii,
ndipo nadharia yake ikatukuzwa
na kuwa nadharia ya kutawala
taifa.
Fikra za Confucius zimekusanywa
katika kitabu kimoja, nacho
ni “Maneno Yaliyoteuliwa ya
Confucius”. Katika China ya
kale kitabu hicho kilikuwa
kama msahafu sawa na biblia
ilivyokuwa katika nchi za
Magharibi. Raia wa kawaida
walikuwa wanajichunga kwa
mawazo ya kitabu hicho; Endapo
watu walitaka kupata nyadhifa
iliwabidi kusoma kitabu hicho
kwa undani. Katika historia
ya China kuna usemi unaojulikana
sana, nao ni “Nusu kitabu
cha ‘Maneno Yaliyoteuliwa
ya Confucius’ yanaweza kutawala
dunia nzima” maana yake ni
kuwa mradi tu ukifuata nusu
na nadharia ya Confucius utaweza
kabisa kutawala taifa.
Kwa kweli Maneno Yaliyoteuliwa
ya Confucius sio kitabu cha
mahubiri ya maadili tu bali
vile vile ni kitabu chenye
mambo mengi ikiwa ni pamoja
na kusoma vitabu, kuhusu muziki,
utalii na kujenga urafiki
n.k. Katika kitabu hicho,
imeandikwa kuwa mwanafunzi
wake mmoja aliyeitwa Zi Gong
alimwuliza Confucius kwamba,
ikiwa lazima afute moja kati
ya jeshi, chakula na raia
katika utawala wake, basi
ni bora afute lipi? Bila wasiwasi,
Confucius akamjibu: Jeshi.
Nadharia ya Confucius inagusia
mambo mengi, na baadhi ya
mambo hayo yanafuatwa hata
katika zama zetu, na maneno
aliyosema yalikuwa mengi katika
kitabu hicho, hadi sasa baadhi
yamekuwa usemi unaojulikana
kwa wote, mathalan, “Kati
ya watu watatu, hakika mmoja
anafaa kuwa mwalimu wangu”,
maana yake ni kuwa kila mmoja
huwa na sifa zake, wanadamu
wanapaswa kujifunza kutoka
kwa wengine.
|