Laozi
中国国际广播电台


Laozi, jina lake la ukoo ni Li na jina lake ni Er, jina Laozi ni jina lake alilopewa na watu kwa heshima. Alikuwa mtu wa Dola la Chu katika Enzi ya Spring na Autumn (770 K.K.—476 K.K.). inasemekana kwamba yeye alikuwa ni mtu mrefu mwenye masikio makubwa, kipaji kipana na midomo minene. Aliwahi kuwa mtunza vitabu, na kutokana na kazi hiyo alikuwa na elimu kubwa. Confucius aliwahi kwenda kukutana naye kutaka kujifunza. Laozi aliandika kitabu cha “Maadili”, kitabu hicho kilikuwa na maneno elfu tano. Katika kitabu hicho aliandika kwamba mambo yote duniani yanahusiana na kusaidiana. Na pia katika kitabu hicho alieleza kuwa mambo yanaweza kubadilika, kwamba mambo mazuri yanaweza kubadilika kuwa mambo mabaya na mambo mabaya yanaweza kubadilika kuwa mazuri, na ndani ya mambo mazuri kuna sehemu ya kuyafanya mambo mazuri kuwa mabaya na ndani ya mambo mabaya kuna sehemu fulani ya kuyafanya mambo mabaya kuwa mambo mazuri. Alisema mbegu ndogo inaweza kuchipuka na kua kuwa mti mkubwa, chembe za udongo zinaweza kujenga jukwaa kubwa. Alisema watu haifai kutishika na taabu, ili mradi tu akiwa na nia ya kufanya juhudi kutoka kazi ndogo ndogo bila kuacha atapata mafanikio makubwa.

Laozi alipinga sana vita. Alisema, mahali palipokuwa na vita patakuwa vichaka, na baada ya vita hakika kutakuwa na maafa ya kilimo, na pia alipinga watawala kuishi maisha ya anasa na kutoza kodi kupita kiasi.

Fikra za Laozi ni muhimu katika historia ya falsafa ya China, na fikra zake zilikuwa na taathira kubwa kwa wanafikra wa kimaendeleo na wanamageuzi ya jamii.