Mwana-hisabati Zu Chongzhi
中国国际广播电台


      

Uwiano kati ya mzingo wa duara na kipenyo ulikuwa tatizo kubwa na gumu katika hisabati. Katika China ya kale wanahisabati wengi walijitahidi kutafuta jawabu la uwiano huo, lakini hawakufanikiwa hadi karne ya tano ambapo Zu Chongzhi alipiga hatua kubwa katika utatuzi wa tatizo hilo.

Zu Chongzhi alikuwa ni mwana-hisabati mkubwa na mnajimu katika China ya kale. Alizaliwa mwaka 429 katika mji ambao sasa unaitwa Nanjing, watu wa familia yake walikuwa na elimu ya unajimu kizazi kwa kizazi. Kutokana na mazingira ya familia yake, tangu utotoni mwake Zu Chongzhi alipewa elimu ya hisabati na unajimu. Mwaka 464 alipokuwa na umri wa miaka 35 alianza kutafuta jawabu la uwiano kati ya mzingo wa duara na kipenyo.

Katika China ya kale, kutokana na mazoezi ya kazi watu walikuwa wanafahamu kwamba “mzingo wa duara ni mara tatu na zaidi kidogo kuliko kipenyo”. Lakini “zaidi” kwa kiasi gani? Majibu yalikuwa tofauti. Zu Chongzhi alitopea katika hesabu zake na baadaye akifanya hesabu tena na tena na mwishowe akapata jawabu lake lenye namba saba mbele ya nukta yaani kati ya 3.1415926 na 3.1415927. Jawabu hilo ni sawa na jawabu walilolipata wana-hisabati wa nchi za nje baada ya miaka zaidi ya 1000. Ili kukumbuka mchango wake katika uwiano huo wana-hisabati wa nchi za nje wanaita alama ya uwiano kati ya mzingo wa duara na kipenyo kuwa “Uwiano wa Zu”.


  Licha ya mafanikio aliyopata kuhusu uwiano kati ya mzingo wa duara na kipenyo, naye pia alishirikiana na mwanawe kufanikiwa kupata kanuni ya kuhesabu ujazo wa tufe. Kanuni waliyotumia ilipewa na jina la “Cavalieri” katika nchi za Magharibi wakati Mtaliana Cavalieri alipogundua kanuni hiyo miaka elfu moja baadaye. Ili kuwakumbuka baba na mwana kanuni hiyo pia inaitwa “kanuni ya Zu” katika elimu ya hisabati.

Mafanikio ya Zu Chongzhi katika uwanja wa hisabati yameonesha kwa kiasi tu maendeleo ya hisabati katika China ya kale. Ukweli ni kwamba kabla ya karne ya 14 China ilikuwa imetangulia mbele katika hisabati. Kwa mfano, uhakiki wa pembetatu mraba katika hesabu za maumbo ulikuwa umeandikwa katika kitabu karne ya pili K.K. wazo la namba hasi na kanuni za kutoa na kuzidisha hesabu za namba hasi na chanya zilikuwa zimekwisha tolewa katika karne ya kwanza.