Mtaalamu wa dawa Li Shizhen
中国国际广播电台


Tiba ya jadi ya Kichina ina historia ndefu, na walitokea wataalamu wengi wa dawa. Katika karne ya 16, Enzi ya Ming nchini China, alikuweko mtu mmoja mashuhuri wa dawa za mitishamba aliyeitwa Li Shizhen. Kitabu maarufu cha “Tiba na Dawa za Mitishamba” ndicho kilichoandikwa naye.

Li Shizhen (1518—1593) alizaliwa katika mkoa wa Hubei. Baba wa Li Shizhen alikuwa mganga, na Li Shizhen alipokuwa mtoto mara kwa mara alifuatana na baba yake kwenda milimani kutafuta dawa za mitishamba na kutengeneza dawa nyumbani. Lakini kutokana na kuwa hadhi ya waganga ilikuwa duni katika jamii, Li Shizhen aliamua kusoma ili apate nafasi ya ofisa.

Mwaka 1531, Li Shizhen alipokuwa na umri wa miaka 14 alifanikiwa katika mtihani wa wilaya, baadaye aliwahi kushiriki mitihani ya taifa kwa mara tatu lakini mara zote alishindwa. Tokea hapo alianza kujifunza udaktari kutoka kwa baba yake. Ili kujipatia elimu nyingi alikuwa mara kwa mara anazungumza na wavuvi, wawindaji, watema kuni na wakulima ili kukusanya tiba za kienyeji, na kwa kufanya majaribio alielewa kazi ya tiba ya kila aina ya mitishamba. Mwaka 1522, Li Shizhen alipokuwa na umri wa miaka 35 aliandika kitabu chake “Tiba na Dawa za Mitishamba”.

Kitabu cha “Tiba na Dawa za Mitishamba” kimekusanya dawa za mitishamba aina 1892 na aina za matibabu zaidi ya elfu 11, na pia kuna picha za mimea ili watu watambue vilivyo mimea yenyewe.

Li Shizhen alitumia maisha yake yote katika ukusanyaji uzoefu wa matumizi ya dawa za mitishamba miongoni mwa watu wa China na aliandika kitabu cha “Tiba na Dawa za Mitishamba”. Kitabu hicho kilichapwa mara kadhaa nchini Japan na pia kilitafsiriwa kwa lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kilatini, kilienea duniani kote tokea karne ya 17.