Daktari wa Ajabu Huatuo
中国国际广播电台


 Watu wanapougua wanakwenda kuonana na daktari wakitumai kupona, lakini kama ugonjwa ukiwa sugu,watu hao husema “laiti daktari ajabu Huatuo angekuwa hai”. Huyu Huatuo alikuwa mganga wa miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita, kutokana na uhodari wake watu walimmsifu kuwa ni “daktari wa ajabu”.

Huatuo alikuwa ni mwenyeji wa mkoa wa Anhui, tarehe yake ya kuzaliwa haiwezi kuthibitishwa, lakini aliuawa kabla ya mwaka 208. Inasemekana kwamba Huatuo alikuwa na afya nzuri na alipokuwa na umri wa miaka mia moja afya yake bado ilikuwa njema. Kutokana na maandishi ya historia, alikuwa mganga wa kienyeji na alikuwa na nafasi nyingi za kuwa ofisa, lakini alikataa. Jemadari mkubwa Cao Cao (155-220) alikuwa na ugonjwa wa kuumwa na kichwa kwa muda mrefu, alimwomba Huatuo amtibu, muda si mrefu Cao Cao alipona kabisa. Tokea hapo Cao Cao alimlazimisha Huatuo aishi naye na kutunza afya yake. Lakini siku chache baadaye Huatuo alirudi nyumbani kwa kisingizio kuwa mkewe alikuwa anaumwa. Ingawa Cao Cao alimhimiza mara kadhaa arudi kwake, lakini Huatuo hakurudi. Cao Cao aliamua kumtia gerezani na baada ya muda alimwua.

Huatuo alikuwa na elimu nyingi za tiba ambazo zinahusika na magonjwa ya maambukizi, minyoo, wanawake na watoto, mfumo wa kupumua na ngozi, na hasa elimu ya kufa ganzi kwa mwili mzima na upasuaji.

Huatuo alikuwa mtu anayependwa sana na watu, kwa kiasi fulani uhodari wake katika matibabu umeonesha maendeleo ya tiba katika miaka elfu mbili iliyopita nchini China. Huatuo alikuwa mmoja wa watu waliotangulia kutumia dawa za ganzi duniani.

Huatuo alikuwa hodari wa kufanya upasuaji. Aliwahi kumfanyia upasuaji msichana mmoja mwenye umri wa miaka 20 ambaye alikuwa na kidonda kwenye goti kwa miaka minane. Huatuo alifunika dawa ya unga kwenye kidonda baada ya kutoa kipande kimoja cha mfupa, msichana huyo alipona baada ya siku saba. Watu wa leo wanaona kuwa kipande cha mfupa alichotoa kilikuwa ni kipande kilichokufa. Kulikuwa na mgonjwa mwingine mzee ambaye alikwenda kumwona, baada ya kuchunguza ugonjwa wake Huatuo alimwambia kuwa ugonjwa wake umekuwa mkubwa na anaweza tu kufayiwa upasuaji wa tumbo, lakini hata hivyo, anaweza kuishi kwa miaka 10 hivi, na bila ya upasuaji pia ataishi muda huo huo, kwa hiyo ni afadhali aache upasuaji. Lakini kutokana na usumbufu wa ugonjwa wenyewe alimwomba Huatuo amfanyie upasuaji, maumivu yalipungua lakini mzee huyo hakuishi zaidi ya miaka 10.

Huatuo pia alikuwa hodari wa kugundua ugonjwa kwa kuangalia sura ya mtu. Siku moja alipokuwa katika baa, aliwaona watu kadhaa wakinywa pombe, aligundua mmoja kati yao alikuwa na ugonjwa mkubwa, alimwambia asinywe zaidi na kurudi nyumbani haraka. Mtu huyo alipokuwa njiani alianguka kutoka kwenye gari na baada ya kufika nyumbani siku chache alikufa.

Watu wa leo wanatilia maanani sana mazoezi ya kuimarisha afya. Miaka elfu mbili iliyopita Huatuo alivuni mazoezi mepesi ili kuimarisha afya, “mchezo wa wanyama wa aina tano” ambayo yalikuwa ni mazoezi mepesi kwa vitendo vya aina tano za wanyama: chui, swala, dubu, nyani na ndege. Watu wanaofanya mchezo huo wananyoosha mishipa, kuongeza mzunguko wa damu, kuongeza uwezo wa kujikinga na maradhi. Wanafunzi wa Huatuo walikuwa wengi, na kati yao watatu walikuwa maarufu ambao walitoa mchango mkubwa katika tiba ya Kichina. Baada ya Huatuo kufariki, watu walimjengea mahekalu mengi kumkumbuka katika mahali alipowahi kutoa matibabu.