Wang Zhaojun
中国国际广播电台


Katika historia ya kale ya China migogoro kati ya kabila la Wahan na makabila mengine ikitokea, ilikuwa inatatuliwa kwa vita, lakini pia iliwahi kutokea njia nyingine ya kutatua migogoro kati ya makabila, nayo ni kumwoza binti wa mfalme kwenye kabila jingine na kupata urafiki na kabila hilo.

Karne ya kwanza ilikuwa ni kipindi cha Enzi ya Han. Kabila la Waxiongnu lililokuwa katika sehemu ya kusini magharibi ya China lilikumbwa na migogoro kutokana na watemi kugombea madaraka. Wakati huo mtemi mmoja aliyejulikana kwa jina la Han Xie alikuja kwa mfalme wa Enzi ya Han kuomba msaada. Mfalme wa Enzi ya Han alimkaribisha kwa ukarimu na alimsaidia kwa nafaka nyingi, na baada ya kurudi alifanikiwa kupata utawala wa kabila la Waxiongnu.

Ili kupata urafiki wa daima mwaka 33 K.K. Han Xie kwa mara nyingine alikuja mji mkuu kuonana na mfalme na kuomba amwoe binti yake. Mfalme wa Enzi ya Han mara alikubali ombi lake. Mfalme aliwaambia vijakazi wake “kati yenu atakayekubali kuwa mke wa mfalme wa kabila la Xiongnu atakuwa binti yangu.”

Kulikuwa na msichana mmoja mwenye sura nzuri na werevu, aliitwa Wang Zhaojun. Msichana huyo alikuwa mwerevu na kupenda kusoma, aliweza kutunga mashairi na kupiga kinanda, alikubali kuolewa na mfalme wa kabila la Waxiongnu kwa ajili ya urafiki wa makabila mawili.

Kwa kusindikizwa na maofisa wa Enzi ya Han Wang Zhaojun alisafiri mbali na kufika sehemu ya kabila la Waxiongnu. Mwanzoni maisha ya kabila hilo yalikuwa magumu kwake lakini baada ya muda alizoea na kuishi vema na Waxiongnu.