Yanzi
中国国际广播电台


      
Katika kitabu maarufu cha “Rekodi ya Historia” kilichoandikwa na Simaqian, walielezwa wanadiplomasia kadhaa mashuhuri, mmoja wao alikuwa Yan Zi aliyeishi katika karne ya sita.

Kipindi kati ya mwaka 770 K.K. hadi 481 K.K. katika historia ya China kinaitwa kipindi cha Spring na Autumn. Wakati huo utawala wa Enzi ya Zhou ulikuwa umeanza kudhoofika, madola yaliyo chini ya himaya kake aylikuwa yanapigana kugombea ardhi na mwishowe yalitokea madola kadhaa yenye nguvu kubwa, na pia walitokea wanasiasa mashuhuri. Yan Zi alikukwa mmojawapo.

Kwa mujibu wa maandishi ya historia, kimo cha Yan Zi kilikuwa mita moja na sentimita arobaini tu, lakini elimu yake ilikuwa pana na alikukwa mtu mwerevu na mcheshi.

Yan Zi aliwahi kwenda kwenye madola mengine mara nyingi akiwa mjumbe wa Dola la Qi, kati ya safari zake, hadithi katika safari mbili alipokuwa katika Dola la Chu zilikuwa maarufu. Mfalme wa Dola la Chu alijua yeye ni mbilikimo, alitaka kumdhihaki. Katika safari ya kwanza alipokuwa kwenye Dola la Chu mfalme aliamuru watu wake wamwingize mjini kutoka kwenye kilango kidogo pembeni mwa lango kubwa. Yan Zi alielewa mfalme Chu akitaka kumdhalilisha, alikataa kabisa na kusema, “Nikifika kwenye dola la mbwa nitaingia kwenye kilango cha mbwa, sasa nimekuja kwenye dola la Chu nikiwa mjumbe wa dola, niwezaje kuingia mjini kupitia kilango cha mbwa!” Walinzi walikuwa hawana budi ila kumpitisha kutoka kwneye mlango mkubwa. Mfalme wa Chu alipokutana na Yan Zi alimwuliza kwa makusudi: “Kwani dola la Qi linashindwa kumchagua mtu mwingine aje kwenye dola la Chu badala yako?” Yan Zi alimjibu kwa utaratibu, “Dola la Qi lina mazoea ya kutuma wajumbe wenye maadili mema kwenye madola yenye maadili mema, na kutuma wajumbe wapumbavu kwenye madola ya wapumbavu. Mimi ni mpumbavu kabisa kati ya wajumbe wote, ndio maana nimetumwa hapa.”

Safari ya pili alipokwenda kwenye dola la Chu, mfalme wa Chu alitaka kumwaibisha Yan Zi hadharani. Wakati mfalme wa Chu alipomkaribisha kwenye chakula, ghafla askari wawili walileta mtu mmoja aliyefungwa kamba mbele ya mfalme, wakisema mtu huyo ni mtu wa dola la Qi, aliiba mali yao. Mfalme alimtupia macho Yan Zi akisema, “Kwani watu wa dola la Qi walizaliwa na wezi?” Mwerevu Yan Zi mara alikumbuka mto Huaihe uliokuwa mpaka wa madola mawili, alitumia michungwa kumjibu mfalme: “Machungwa yaliyopatikana kwenye ukingo wa kusini wa mto ni matamu, lakini yaliyoko kwenye ukingo wa kaskazini ni machungu, sababu udongo wenyewe ni tofauti. Watu wanaoishi katika dola la Qi hawaibi, lakini wanaoishi katika dola la Chu wana tabia ya kuiba, kwani ardhi ya Chu inalea wizi?”

Mambo kama hayo yalikuwa mengi ambayo Yan Zi aliwashinda wapinzani wake waliojaribu kumdhihaki na kuharibu heshima ya dola lake. Alikuwa mwanadiplomasia mashuhuri katika hitoria ya China.