中国国际广播电台
Katika kipindi cha Spring
na Autumn, katika dola la
Chu kulikuwa mwanamuziki mmoja
ajulikanaye kwa jina la Yu
Boya. Huyu Yu Boya alikuwa
mwerevu toka alipokuwa mtoto,
na alipenda sana muziki. Baadaye
alijifunza kupiga kinanda
kwa mwalimu wake Lian Cheng.
Baada ya kujifunza kwa miaka
mitatu, alikuwa mwanamuziki
mashuhuri, lakini Yu Boya
hakuridhika, aliona kiwango
chake kilikuwa bado si kikubwa
kileleni. Mwalimu wake Lian
Cheng alifahamu Yu Boya aliyofikiri
moyoni, alimwambia kwamba
atamwongoza kwa mwalimu wake
ambaye ufahamu wake wa muziki
ni wa juu sana. Yu Boya alikubali.
Baada ya kutayarisha chakula
cha kutosha hao wawili walipanda
mashua na kufika kwenye mlima
wa Penglai. Mwalimu wake Lian
Cheng alimwambaia, “Nisubiri
hapa, nakwenda kumtafuta mwalimu
wangu.” kisha akaondoka. Siku
nyingi zilipita, lakini mwalimu
wake Lian Cheng hakurudi.
Boya aliangalia bahari isiyo
na mwisho na misitu mlimani
alihuzunika sana, kwa kusukumwa
na moyo alipiga kinanda chake.
Muziki ulijaa huzuni, lakini
tokea hapo alikuwa mwanamuziki
mkubwa. Kwa kweli mwalimu
wake Lian Cheng alifanya hivyo
kwa makusudi ili Yu Boya apate
hisia za kweli moyoni.
Kuishi katika kisiwa kilichojitenga,
usiku na mchana kitu alichoona
ni bahari, ndege na misitu,
siku nenda siku rudi hisia
zake zilibadilika na kuelewa
zaidi muziki, alitunga muziki
maarufu uliowagusa mioyo wasikilizaji.
Yu Boya alikuwa mwanamuziki
mkubwa, lakini watu waliofahamu
muziki wake walikuwa wachache.
Siku moja Yu Boya alisafiri
kwa mashua, alipofika karibu
na mlima, mvua kubwa ilinyesha,
aliegesha mashua yake kukimbia
mvua. sauti ya mvua na mandhari
nzuri ya ukungu uliokuwa kwenye
uso wa mto ilimsisimua, alipata
msukumo wa kupiga kinanda.
Muziki alioupiga ulikuwa ni
sauti kutoka moyoni mwake.
Kulikuwa na mtu mmoja kwenye
ukingo wa mto akisikiliza
muziki wake, mtu huyo aliitwa
Zhong Ziqi.
Baada ya kusalimiana Yu Boya
alimkaribisha Zhong Ziqi ndani
ya mashua yake na kumpigia
muziki. Zhong Ziqi alisikiliza
kwa msisimko. Yu Boya alisema,
“Katika dunia hii ni wewe
tu unayefahamu sauti ya moyoni
mwangu, wewe ndiye mwelewa
sauti yangu!” Hao wawili walikuwa
ndugu wa kuchanjiana.
Yu Boya aliahidiana na Zhong
Ziqi kuwa watakutana baadaye.
Siku moja Yu Boya alikwenda
kwa Zhong Ziqi kama walivyoahidiana,
lakini wakati huo Zhong Ziqi
alikuwa amefariki. Baada ya
kusikia habari hiyo Yu Boya
alikimbilia kwenye kaburi
la Zhong Ziqi na kumpigia
muziki kwa huzuni kubwa, kisha
alisimama na kuvunja kabisa
kinanda chake. Tokea hapo
Yu Boya aliacha kabisa kupiga
kinanda.
|