中国国际广播电台
Sun Wu aliyeishi katika karne
ya sita K.K. ni mtu maarufu
sana nchini na duniani, kitabu
chake cha “Mbinu za Kivita
za Sun Zi” kilikuwa ni maandishi
makubwa ya kivita katika China
ya kale.
Sun Wu alizaliwa mwaka 551
K.K. kilikuwa ni kipindi cha
Spring na Autumn katika historia
ya China. Alikuwa mtu wa dola
la Qi, alipokuwa na umri wa
miaka 19 alikwenda dola la
Wu, na katika kiunga cha mji
mkuu wa dola la Wu (mji wa
Suzhou wa leo) aliandika kitabu
chake cha mbinu za kivita
na kumpa mfalme wa dola la
Wu. Mfalme alifurahi sana,
lakini hakujua kama mbinu
zenyewe zinaweza kutumika,
alimtaka Sun Wu afanye mazoezi
kwa masuria waliokuwa ndani
ya kasri la kifalme.
Sun Wu aliwagawa masuria
180 kwa vikundi viwili na
kuwateua wawili waliopendwa
sana na mfalme kuwa viongozi
wa vikundi viwili, kimoja
kulia na kingine kushoto,
na kufanya mazoezi.
Sun Wu alisimama kwenye jukwaa
na kuwafahamisha mpango wa
mazoezi yake. Sun Wu alipiga
ngoma ya kuanzisha mazoezi.
Lakini masuria walikuwa kama
hawajasikia mdundo wa ngoma,
bali walichekacheka na kuchezacheza,
safu zao zilivurugika, ingawa
Sun Wu aliwaasa mara kadhaa,
lakini haikusaidia kitu. Kutokana
na hali hiyo, Sun Wu aliamuru
kuwaua viongozi wawili.
Mfalme alipoona kweli Sun
Wu alitaka kuwaua wapendwa
wake wawili alimsihi awaache.
Lakini Sun Wu hakubali ombi
la mfalme, aliwaua. Kisha
akaanza tena mazoezi, safari
hii masuria walifanya mazoezi
kwa makini, walipiga hatua
mbele na nyuma, waliviringika
na kutambaa kifudi fudi, kila
mmoja alifanya vizuri. Kuona
hali hiyo mfalme alifurahi,
akamteua Sun Wu kuwa jemadari.
Chini ya uongozi wa Sun Wu
jeshi la dola la Wu lilikuwa
hodari sana na lilipata ushindi
kila mara katika vita vya
kupigana na madola mengine.
Mwaka 482 K.K. mfalme wa
dola la Wu alikuwa mbabe kati
ya madola yote kutokana na
mbinu zilizoandaliwa na Sun
Wu.
Kutokana na ushindi, mfalme
alikuwa anavimba kichwa. Kwa
kuona jinsi mfalme alivyokuwa,
Sun Wu aliondoka na kuishi
mbali na mfalme milimani.
Kitabu cha “Mbinu za Kivita
za Sun Zi” ingawa kilikuwa
na maneno elfu 6 katika makala
13, lakini kilionesha kikamilifu
mbinu zake za kivita. Kitabu
hicho kilisifiwa na watu wa
baadaye kuwa ni “kitabu cha
kwanza duniani kuhusu mbinu
za kivita”, na kilitumika
sana katika mambo ya kijeshi,
kisiasa na uchumi.
|