Qi Jiguang
中国国际广播电台


Katika mlima wa Yu Shan mkoani Fujian kuna hekalu moja lililowekwa sanamu ya Qi Jiguang, watalii wanapofika huko hawakosi kwenda kutoa heshima kwake kutokana na uzalendo wake na mchango wake katika mapambano dhidi ya wavamizi.

Qi Jiguang alikuwa jemadari katika Enzi ya Ming, alizaliwa katika ukoo wa jemadari. Kwa kuathiriwa na baba yake, Qi Jiguang toka alipokuwa mtoto alipenda sana mambo ya kijeshi na kuwa na nia ya kuwa mwanajeshi hodari. Wakati huo wavamizi wa Japan walikuwa mara kwa mara wanashambulia China. Alipokuwa na umri wa miaka 17 alirithi wadhifa wa baba yake na kuanza maisha yake ya kijeshi. Alipokuwa tu jemadari tatizo lililomkabili lilikuwa ni mashambulizi ya Japan.

Tokea mwishoni mwa Enzi ya Yuan na mwanzoni mwa Enzi ya Ming maharamia wa Japan mara kwa mara walikuwa wakipora mali na kuua watu kwenye mwambao. Katika nusu ya pili ya karne ya 15 maharamia wa Japan walikuwa wanashirikiana na wafanyabiashara wabaya wa China kufanya uovu.

Mwaka 1555 Qi Jiguang alitumwa kwenye mwambao, aliunda jeshi la wakulima na wachimba migodi. Walitumia mishale na mikuki kuwaua baada ya kuwatega mitegoni.

Jeshi lake lilikuwa na askari elfu 4, na baada ya kuwafundisha na kuwafahamisha askari mbinu za kivita, jeshi hilo lilikuwa hodari sana, na kutokana na kuwa na nidhamu kali liliungwa mkono na wananchi.

Mwaka 1561 maharamia wa Japan elfu kadhaa na mashua zaidi ya mia walifanya mashambulizi katika sehemu ya Taizhou mkoani Zhejiang. Qi Jiguang kwa haraka aliwaongoza askari wake kupambana nao na kuwaangamiza maharamia wote.

Kutokana na juhudi za Qi Jiguang na majemadari wengine, maharamia wa Japan walitoweka, mikoa ya Zhejiang na Fujian ilikuwa tulivu, na uchumi ulistawi. Qi Jiguang alitoa mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya maharamia wa Japan na alisifiwa sana na watu wa China.