Siku ya Tarehe 7 ya mwezi wa 7 kwa kalenda ya kilimo ya China yaani sikukuu ya kuomba baraka
中国国际广播电台

 

Tarehe 7 ya mwezi wa 7 kwa kalaenda ya kilimo ya China ni siku ya kuomba baraka kwa wananchi wa China, inasemekana kuwa, siku hiyo pia ni siku ya kukutana kwa nyota ya Niu Lang na nyota ya Zhi Nu.

Hadithi ilisimulia kuwa, katika zama za kale sana, mbingu ilikuwa ni ya buluu tupu, kulikuwa hakuna mawingu hata kidogo. Mfalme wa mbingu aliona kuwa mbingu na rangi ya buluu peke yake si wa kupendeza, hivyo aliwaambia binti zake 7 wasokote nyuzi na kufuma vitambaa ili kuishonea nguo “mbingu”. Lakini vitambaa vilivyofumwa na binti zake 7 vyote vilikuwa vya rangi ya kijivujivu au nyeupe, vilikuwa bado havipendezi. Binti wa 7 ambaye ni binti mdogo kabisa lakini ni mwenye akili nyingi. Siku moja aligundua maua ya aina moja yaliyochanua yana rangi ya aina 7, kwa hivyo alichuma maua hayo mengi na kupaka rangi mbalimbali kwenye nyuzi walizosokota, baada ya juhudi zake, binti zao walifaulu kufuma vitambaa vyenye rangi mbalimbali, walifurahi sana na dada huyo mdogo alisifiwa kuwa ni binti mwerevu, ambapo waliamua kwa kauli moja kuwa, katika siku za kawaida, wataivalisha “mbingu” nguo nyeupe; siku ya mvua, wataivalisha nguo ya kijivu; na asubuhi na jioni wataivalisha nguo za rangi. Mfalme wa mbinguni alipoambiwa, alifurahi sana, akampa binti yake mdogo hadhi ya malaika “Zhi Nu.”

Malaika Zhi Nu kila siku alifuma vitambaa, akijisikia uchovu, huangalia mandhari ya dunia chini ya mbingu. Kijana mmoja aliyefuga ng'ombe alivutiwa macho, aliona kijana huyo kila siku alilima shamba peke yake, alipopumzika, aliongea tu na ng'ombe aliyemfuga, Zhi Nu alimhurumia sana. Kijana huyo aliitwa Niu Lang.

Siku moja ng'ombe mzee alimwambia Niu Lang: “Kesho ni tarehe 7 Julai, binti 7 wa mfalme wa mbinguni watafika duniani kuoga. Ukificha nguo ya malaika Zhi Nu, atakuwa mke wako.” Niu Lang aliamua kwenda kujaribu.

Siku hiyo tarehe 7 Julai, Niu Lang alijificha ndani ya matete kando ya mto, muda si mrefu baadaye, aliona malaika 7 waliosimama juu ya mawingu 7 wakija duniani, wakifika kando ya mto wakivua nguo zao, wakajitupa ndani ya maji kuogelea. Papo hapo Niu Lang akachukua nguo ya malaika Zhi Niu, halafu akakimbia kwa haraka, vishindo vya matete viliwashtusha malaika 7, wakajiondoa kutoka mto, malaika 6 wakavaa nguo zao na kuruka mbinguni, ila tu malaika Zhi Niu hakuona nguo zake zilipo, akahangaika sana na kusimama kwenye kando ya mto. Niu Lang akamwomba malaika Zhi Niu kuwa, kama akikubali kuolewa naye, atampa nguo yake. Malaika Zhi Niu alipoona Niu Lang ndiye kijana yule anayempenda, alikubali kwa haya kuolewa na Niu Lang.

Jioni ya siku hiyo, Niu Lang na Zhi Nu wakafunga ndoa chini ya usimamizi wa ng'ombe mzee. Katika miaka miwili baadaye, mfumaji nguo alizaa mvulana mmoja na msichana mmoja. Mume na mke, mmoja alilima shamba, mwingne alifuma nguo, maisha yao yalikuwa ni mazuri sana.

Baada ya miaka kadhaa kupita, walijaliwa watoto wawili, wa kiume na wa kike, na hivyo furaha ilitawala familia hiyo.

Lakini siku moja ghafla mawingu mazito yalitanda mbinguni, kimbunga kilivuma kwa nguvu, na askari wawili wa mbinguni wakashuka kwenye nyumbani kwao. Niu Lang akaambiwa kwamba Zhi Nu alikuwa mtoto wa mfalme wa mbinguni, amekuwa akitafutwa kwa miaka kadhaa iliyopita. Askari walimrudisha Zhi Nu mbinguni kwa nguvu.

Niu Lang akiwa na watoto wawili kifuani alibaki kumwangalia mkewe akichukuliwa na askari wawili kurudi mbinguni, alihuzunika sana, lakini aliapa kwamba atakwenda mbinguni kumchukua mkewe Zhi Nu ili kukamilisha familia yake. Lakini binadamu atawezaje kufika mbinguni?

Niu Lang alipoishiwa na ujanja, ng'ombe wake mzee alimwambia, “Nichinje mimi na kujifunika ngozi yangu mgongoni; kwa namna hiyo utaweza kuruka kwenda mbinguni.” Niu Lang kamwe hakukubali, lakini ng'ombe alishikilia. Kwa kuona hana njia nyingine Niu Lang alimchinja huku akilia.

Niu Lang alijifunika kwa ngozi ya ng'ombe, akawabeba watoto wawili kwa mzegazega, mmoja mbele, mmoja nyuma, akaruka kwenda mbinguni. Lakini huko kwenye kasri ya mbinguni watu waligawanyika kwa matabaka, hakuna yeyote aliyemheshimu kabwela maskini na hohe hahe kama Niu Lang. Mungu alimkatalia ombi lake la kuonana na mkewe Zhi Nu.

Niu Lang na watoto wake walimsihi sana, mwishowe aliruhusiwa kumwona mkewe kwa muda mfupi. Mkewe Zhi Nu aliyekuwa amefungwa alipowaona mumewe na watoto wake alijawa na furaha na huzuni. Kufumba na kufumbua muda ukapita, mungu akaamuru kuondolewa kwa Zhi Nu. Maskini Niu Lang na watoto wake walimkimbilia kadri wawezavyo huku wakianguka anguka na kuinuka. Mwishowe walipomkaribia, mke wa mungu alichomoa kibanio cha nywele akachora mstari angani, na mara mto wa kilimia ukatokea kati yao. Tokea hapo Niu Lang na Zhi Nu wakawa wametenganishwa na mto huo, isipokuwa tu kila tarehe 7 ya mwezi wa 7 wanaruhusiwa kukutana. Kila ifikapo siku hiyo, ndege wasio na idadi waliungana pamoja na kuwa kama daraja juu ya mto huo ili Niu Lang na Zhi Nu wakutane.

Katika siku za baadaye, kila ifikapo tarehe 7 mwezi wa 7 kwa kalenda ya kilimo, wasichana huomba baraka kutoka kwa Malaika Zhi Nu, wakichukua sindano 7 na nyuzi za hariri, kama nyuzi zinaweza kupita katundu ya sindano bila kikwazo, hali hii inaonesha kuwa wasichana hao ni werevu. Inasemekana kuwa, usiku wa siku hiyo, watoto wengi hukaa chini ya mizabibu, wakasikia Niu Lang na Zhi Nu wakiongea kwa furaha.