Sikukuu ya Taa ya Tarehe 15 mwezi wa kwanza kwa kalenda ya kilimo
中国国际广播电台

     Katika kalenda ya Kilimo ya China, tarehe 15 mwezi wa kwanza ni “Sikukuu ya Taa” ya Kichina. Hiyo ni miongoni mwa sikukuu kubwa za Kichina.

Wachina walianza kusherehekea sikukuu hiyo tangu Enzi ya Han, yaani zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita. Mfalme Han Wendi alikuwa mfalme wa tatu wa Enzi ya Han baada ya kumpindua mfalme wa pili Lu Hou. Alikalia kiti cha ufalme tarehe ya 15 Januari kwa kalenda ya Kichina. Ili kuikumbuka siku hiyo ya kuwa mfalme, kila mwaka katika siku hiyo mfalme Han Wendi alijifanya raia na kutembelea mjini “kuburudika pamoja na raia” wake. Ingawa simulizi hiyo haijabainika, lakini ni ukweli ni kwamba tangu Enzi ya Han siku hiyo imekuwa siku ya kumtambikia mungu ili kupata baraka.

Binadamu walianza kutumia moto na taa sawia katika maisha yao. Simulizi kuhusu chanzo cha sikukuu ya taa iliyoenea zaidi ni kama ifuatayo:

Katika Enzi ya Han alikuwepo mtu mmoja, aliyeitwa Dong Fangshuo, alikuwa mcheshi na mwerevu. Mfalme alimpenda sana kwa kuwa mara kwa mara alikuwa akimpatia ushauri na kumfurahisha. Mwaka fulani mwezi wa 12, katika majira ya baridi theluji ilianguka sana, Dong Fangshuo alipomwona mfalme alikuwa hana raha, hivyo alikwenda kwenye bustani ili amchumie maua. Alipokuwa bustanini alimkuta mtumishi msichana mmoja, jina lake Yuan Xiao akilia kwa huzuni, na machozi yakimtiririka kwenye mashavu yake. Baada ya kumwuliza sababu, akatambua kwamba msichana huyo alikuwa na wazazi wawili wakongwe. Tangu msichana huyo achaguliwe kuwa mtumishi wa mfalme katika kasri, hakuwahi kuwaona. Kila ilipofika sikukuu ya mwaka mpya huwakumbuka sana. Dong Fangshuo baada ya kumfariji kidogo akamwahidi kumsaidia ili atoke kwenye kasri akaonane na wazazi wake.

Baada ya kumwacha mtumishi huyo wa kike Dong Fangshuo akaenda nyumbani kwa wazazi wake na kuwawekea mpango kwa akili yake. Dong Fangshuo aliondoka nyumbani kwa wazee akarudi mjini, huku akijifanya mpiga ramli barabarani. Kila aliyekuja kwake kupigiwa ramli alimwambia kwamba tarehe 15 Januari ni siku ya “kuunguzwa kwa moto mbinguni”, na dawa ya kukwepa janga hili ni kuwa, “tarehe 13 mungu wa moto atajifanya msichana mwenye kuvaa mavazi mekundu akiwa na punda wa rangi nyekundu hafifu atakuja mjini Chang An kukagua sura ya ardhi, wakati huo wenyeji waende kaskazini ya mji wajipange barabarani ambapo msichana huyo atapitia, wamsihi wakilia na hivyo watu wote wataokoka.” Watu waliambizana hayo na wakisubiri siku ya tarehe 13 iwadie. Siku ilipowadia, Dong Fangshuo alimwambia msichana mmoja aigize kama alivyomtaka, aliingia mjini taratibu akiwa juu ya punda wake. Wenyeji walipomwona wote walimvamia wakimsihi huku wakilia machozi. Msichana akawaambia, “Kutokana na ombi lenu, basi mkabidhi mfalme wenu kadi hii nyekundu aisome.” Kisha akaondoka. Mfalme alifungua kadi akaona juu yake imeandikwa “Tarehe 15 moto utaanguka mbinguni, mji utaunguzwa.” Baada ya kusoma hayo alitetemeka mwili mzima, asijue la kufanya. Kwa haraka akamwita Dong Fangshuo kumwomba ushauri wake. Kwa akili alimwambia mfalme, “Naomba mfalme wangu uwaambie raia wako waanze kutengeneza taa nyekundu toka leo na ifikapo siku ya tarehe 15 watundike barabarani, vichochoroni, milangoni, na kila mahali mjini; wawashe fataki na fashifashi na watu wa mjini na viungani watoke majumbani kuangalia; wewe mfalme na mkeo, mawaziri, masuria na watumishi wasichana, muende mjini pia mjumuike na raia kufurahia taa.” Mfalme akatoa amri kama alivyoambiwa. Tarehe 15 usiku, taa ziling'ara kote mjini kama mchana, fataki na fashifashi zilikuwa zikitatarika angani. Kama walivyopangiwa wazazi walimwona binti yake Yuan Xiao, walipata nafasi ya kubadilishana nae mawazo kwa muda mrefu. Usiku wenye shamrashamra ulipita, mji mkuu wa Chang An ulisalimika, mfalme akafurahi sana. Akatoa amri, kwamba kila mwaka katika siku hiyo sherehe ifanyike kwa kutundika taa nyekundu na kuwasha fataki na fashifashi. Haya ndio masimulizi kuhusu chanzo cha Sikukuu ya Taa.

Baada ya sikukuu ya taa kuwa desturi ya Wachina siku hiyo haikuwahi kupuuzwa katika enzi zote za China. Siku hiyo taa hutengenezwa kwa aina na rangi mbalimbali, matengenezo ya taa ni sanaa maalumu za Kichina na baadhi ya sehemu hufanya maonyesho, taa za mayungiyungi, za kuelea majini, zenye vivuli vya wanyama vinavyozunguka zunguka, za majoka na barafu, zinavutia kwa ufundi mkubwa, watazamaji wanapostaajabu taa hizi huburudika na shamrashamra za michezo ya kuchezesha taa za majoka, ngoma ya mironjo, mashua ya nchi kavu, na kuonja vyakula vya sehemu maalumu.

Sikukuu ya Taa pia inamaanisha kumalizika kwa kipindi cha mwaka mpya wa Kichina.