Siku ya 8 Desemba
中国国际广播电台

      Tarehe 8 Desemba katika kalenda ya Kichina ni siku ya jadi ya kabila la Wahan ambayo pia inaashiria sikukuu ya mwaka mpya wa Kichina kukaribia.

Kutokanna na maandishi ya kale, siku ya 8 Desemba katika kalenda ya Kichina ni siku ya kufanya tambiko katika China ya kale. China ni nchi inayotilia maanani sana kilimo. Kila mwaka mavuno mazuri yalipopatikana watu wa kale walikuwa wanafanya tambiko ili kumshukuru mungu. Baada ya tambiko watu hukusanyika kufanya sherehe za burudani, kupika uji wa mseto na kula pamoja. Katika karne ya 5 serikali ya enzi zile iliweka siku hiyo yaani 8 Desemba kuwa ni sikukuu.

Baada ya dini ya Buddha kuingia nchini China, maana ya siku hiyo ya 8 Desemba ilikuwa imeongezeka. Inasemekana kwamba baada ya Sakyamuni kuwa Buddha alikuwa na maisha magumu, na alikonda vibaya. Katika siku hiyo alimkuta mchungaji msichana ambaye alimpa bakuli moja la uji wa mseto kutokana na kuona jinsi alivyokonda. Kwa hiyo waumini wa dini wa Buddha pia wanapika uji wa mseto katika siku hiyo.

Watu wa China wana desturi ya kunywa uji wa mseto kuanzia Enzi ya Song yaani miaka elfu moja iliyopita. Katika siku hiyo ya 8 Desema kila familia na hata maofisa wa serikali walikuwa wanakunywa uji wenye mchanganyiko wa mchele na kunde.

Aina za uji wa mseto ni nyingi kutokana michele na kunde tofauti zilizotiwa ndani ya uji, lakini kwa kawaida huwa ni mchele, muwele, ngano na mahindi, mtama, choroko, maharage na kunde nyekundu.

Vitu vilivyokuwa vinatiwa ndani ya uji pia kulikuwa na matunda yaliyokaushwa, na mbegu za matunda kama karanga, njugumawe, alizeti, zabibu, tende, n.k.

Baada ya vitu vyote kuwa tayari, uji hupikwa kwa moto mdogo na kwa muda mrefu. Katika majira ya baridi jamaa wanajikusanya pamoja kando ya meza na kunywa uji kama huo.

Wenyeji wa Beijing wanaichukulia siku hiyo kama ni ishara ya kukaribia kwa sikukuu ya mwaka mpya wa Kichina.

Licha ya kunywa uji wa mseto, katika siku hiyo watu hutia saumu ndani ya siki ili watumie katika mkesha mwaka mpya wakati wanapokula Jiaozi , chakula kama sambusa ndogo kilichochemshwa.