Vijiti vya Kulia
中国国际广播电台

      Duniani kuna njia tatu za kupeleka vyakula mdomoni, kwa mkono, kwa kijiko na umma na kwa vijiti vya kulia.

Matumizi ya vijiti vya kulia yalianzia miaka 3000 iliyopita nchini
China. Vijiti vya kulia vinatengenezwa kwa mianzi.

Lakini vipi vijiti vya kulia vilianza kutumika? Inasemekana kwamba watu wa zama za kale walipokula chakula moto moto walikuwa wanatumia vijiti vya mwanzi au vya mti ili kukwepa kuumia vidole. Vijiti vya kulia vina umbo la unene kwa juu na ncha kwa chini na vyenye pembe nne ili kukwepa kuviringika mezani.

Vijiti vya kulia kwa sasa hutengenezwa kwa vitu vya aina mbalimbali, kuna vijiti vya kulia vya shaba, vya pembe za ndovu, na pia kuna vijiti vilivyotiwa fedha kwenye ncha, kama ndani ya chakula kuna sumu fedha hubadilika rangi yake kuwa ya kijani au nyeusi.

Vijiti vya kulia pia ni kama zawadi katika mila ya Wachina. Msichana anayeozwa hupewa jozi mbili za vijiti vya kulia na jozi za mabakuli. Katika sehemu ya kaskazini ya China watu hutupa chumbani kwa maharusi vijiti vya kulia kwa kuashiria watapata mtoto mapema.

Namna ya kutumia vijiti vya kulia ni ufundi mkubwa. Katika nchi za Magharibi kuna klabu ya kufundishia ufundi wa kutumia vijiti vya kulia. Na nchini Ujerumani kuna jumba la kwanza duniani la makumbusho ya vijiti vya kulia, ndani ya jumba hilo kuna vijiti vya kulia vilivyotengenezwa kwa dhahabu, fedha na mifupa ya wanyama. Vijiti hivyo vinatoka nchi tofauti na enzi tofauti.