Vyakula vya Dawa
中国国际广播电台

      Katika China ya kale watu walipata dawa kutoka kwenye mimea na kupata dawa za mitishamba. Mazao ni chakula na baadhi pia ni dawa. Wachina wanasema, “ni bora kupata afya kwa chakula kuliko kwa dawa, na kinga ni bora kuliko tiba.”

Chakula ambacho pia ni dawa ni mila ya upishi wa tiba. Katika Enzi ya Zhou (1046 K.K.—256 K.K.) chakula hicho kilianza kutumika katika tiba. Katika Enzi ya Tang (618—907) mtaalamu wa tiba Sun Simao alieleza mengi kuhusu kutibu magonjwa kwa chakula katika kitabu chake ambacho kimekuwa na athari kubwa kwenye tiba ya Kichina hadi leo.

Bw. Sun Simao aliona kuwa afya inapatikana kwa chakula kinachofaa. Mtu akiwa mgonjwa, kwanza atibiwe kwa chakula, kama hakisaidii kitu basi baadaye atumie dawa.

Sun Simao aliishi kwa zaidi ya miaka 100, maisha yake marefu yanawafanya watu waamini kuwa chakula chenye uwezo wa kutibu ugonjwa ni msingi wa kupata afya bora.

Chakula cha dawa kinatumika sana katika matibabu ya magonjwa, na baadhi ya vyakula vinavyotibu magonjwa fulani vinajulikana miongoni mwa wenyeji. Kwa mfano, mtu akipata mafua, anatakiwa anywe maji moto moto yaliyochemshwa kwa tangawizi, vitunguu vya majani na sukari guru, atatokwa jasho na kupona.

Katika chakula cha dawa pia kuna maua. Kupika aina fulani ya maua kama vitoweo kuliwahi kutumika sana katika Enzi ya Tang.

Nchini China kuna aina za maua kiasi cha elfu moja, na aina mia moja hivi zinaweza kutumika kama ni chakula cha dawa, na katika sehemu ya kusini ya China aina hizo zinafikia zaidi ya 260.

Maua yanayotumika kama chakula yanawasaidia zaidi wanawake. Kwa mfano maua ya waridi, yanasaidia sana kwa kurekebisha hedhi na rangi ya ngozi.

Chakula chenye uwezo wa dawa hupikwa kwa uji, na vitoweo. Kuna mikahawa ya chakula cha dawa ambayo hupikwa kwa ajili ya kusaidia tiba ya ugonjwa fulani.

Sheria ya chakula nchini China inasema, ni marufuku kutia dawa ndani ya chakula. Kwa ajili ya chakula chenye uwezo wa kutibu magonjwa kisikiuke sheria hiyo, idara ya afya imeruhusu mitishamba kumi kadhaa kutiwa kwenye chakula, kama vile tende, tangawizi, nanaa n.k.

Chakula chenye uwezo wa kutibu magonjwa kimeenea sana nchini China na pia duniani. Pombe na chai yenye maua au magamba ya matunda fulani na mizizi ya mimea fulani vimekuwa vinywaji vya kila siku katika nchi za nje.