Jiaozi (sambusa ndogo za Kichina)
中国国际广播电台

      Jiaozi ni aina moja ya utamaduni wa Kichina, kwa kuwa chakula cha jadi cha Kichina kinaonesha ukarimu na furaha kubwa kwa kujiwa na wageni. Kama mgeni fulani kutoka ng'ambo hajawahi kula Jiaozi wengine husema alifika China bure.

Kwa kifupi Jiaozi ni kijazo kilichofungwa kwa unga wa ngano. Katika siku za zamani, Jiaozi ilikuwa inapikwa katika sikukuu tu hasa katika usiku wa kuamkia sikukuu ya mwaka mpya wa Kichina.

Kijazo cha Jiaozi kina aina tofauti ya mboga na ya nyama au mchanganyiko wa mboga na nyama. Watu hutayarisha kijazo kwa kukatakata nyama mpaka kima na kukatakata mboga mpaka chembe, na kisha hutia soyasosi, mafuta ya simsim, na viungo vingine, vishindo vya kukatakata nyama na mboga vinaashiria maisha mazuri.

Baada ya vijazo kuwa tayari, hufungwa kwa unga kama sambusa ndogo na kuweka mezani tayari kwa kuchemsha.

Baada ya kutia Jiaozi ndani ya maji yaliyochemka, Jiaozi huzama chini na baada ya muda huelea juu, katika muda wa kuchemsha kuna haja ya kutia maji kidogo baridi mara tatu kila baada ya dakika chache, kiasi cha dakika ishirini hivi huiva.

Wakati wa kula Jiaozi pia kuna adabu maalumu, bakuli la kwanza ni kwa ajili ya wahenga na wazee marehemu, bakuli la pili ni kwa ajili ya mungu wa jiko, na kuanzia bakuli la tatu watu wanaanza kula, lakini kwanza kwa wazee.

Katika mkesha wa mwaka mpya wa Kichina, Jiaozi ni chakula cha lazima, jamaa wa familia moja hata akiwa mbali na nyumbani lazima arudi na kujumuika na jamaa zake kula Jiaozi pamoja.

Katika siku hizi, kutokana na shughuli nyingi za kazi, watu hupata Jiaozi iliyoganda kwa baaridi na katika maduka ya kujihudumia na kuchemsha nyumbani au jamaa wote wanakula katika mikahawa, na adabu nyingi za zamani zimekuwa hazifuatwi sana hata vijijini.