Mkoba wa vito “Suolinnang”
中国国际广播电台

      Katika zama za kale alikuwepo mfanyabiashara mmoja tajiri katika sehemu ya Dengzhou, tajiri huyo alikuwa na binti moja aliyeitwa Xiang Ling, watu wa familia wote walimpenda sana. Xiang Ling alifikia umri wa kuolewa, wazazi wake walimtayarishia zawadi nyingi za ndoa, na mama yake alimshonea mkoba mmoja uliotariziwa, na ndani yake vilitiwa vito vya kila aina. Inasemekana kuwa msichana akiwa na mkoba kama huo atapata mtoto mwerevu wa kiume.

Katika siku ya ndoa, Xiang Ling alikaa ndani ya kibanda cha bibi harusi cha kubebwa, watu waliomsindikiza walimpigia vigelegele. Njiani mvua kubwa ilinyesha, walikimbia kwenye kibanda kimoja, lakini punde kidogo alikuja bibi harusi mwingine aliyekaa ndani ya kibanda cha harusi, lakini kibanda chenyewe kilikuwa kidogo na kichakaa. Bibi harusi ndani ya kibanda hicho alilia kwa kwikwi. Xiang Lian aliposikia kilio aliwatuma kijakazi na mtumishi mmoja mzee waende kuangalia kulikoni. Bibi harusi huyo aliitwa Zhao Shouzhen, familia yake ilikuwa maskini sana, na mama yake alikufa mapema, aliyebaki ni baba yake tu ambaye alikuwa hana zawadi ya ndoa. Zhao Shouzhen alihofia atachekwa na wengine kutokana na umaskini na kuwa na wasiwasi kwamba hakuna mtu wa kumtunza baba yake, kwa hiyo alilia machozi.

  Kusikia habari hiyo, Xiang Ling alimhurumia sana, akakumbuka jinsi alivyokua katika familia yenye hali nzuri na hakujua kwamba duniani kuna watu maskini kama Zhao Shaozhen. Xiang Ling alifikiri atawezaje kumsaidia? Ghafla aligundua mkoba wake, basi alimpa Zhao Shouzhen bila kutaja jina lake. Wakati huo mvua ilisimama, vibanda viwili vya bibi harusi viliendelea kubebwa na kila kimoja kushika njia yake.

Baada ya miaka sita kupita, katika sehemu ya Dengzhou yalitokea mafuriko, Xiang Ling na mumewe na mtoto walipoteana. Xiang Ling peke yake alizurura zurura hadi sehemu ya Caizhou, maisha yalikuwa magumu sana. Lakini kwa bahati huko alimkuta yaya wake wa zamani ambaye alimwongoza hadi kwenye familia tajiri ya Lu kuwa yaya kumtunza mtoto aitwaye Tian Lin. Tian Lin alikuwa na umri wa miaka mitano tu, alimpenda sana Xiang Lin na kila siku alimtaka acheze naye mpira bustanini.

Siku moja mtoto Tian Lin alirusha mpira ndani ya jumba dogo la ghorofa. Xiang Ling aliingia ndani kutafuta mpira, ghafla aligundua mkoba mmoja ukutani, alichunguza kwa makini mkoba huo ndio aliyompa Zhao Shouzhen. Mbele ya mkoba huo alikumbuka jinsi alivyotengana na mume na mtoto wake, alilia. Mtoto Tian Lin alipoona alilia, alikimbilia kumwambia mama yake. Mama wa Tian Lin ndiye Zhao Shaouzhen, aliolewa na Bw. Lu, na kutokana na mkoba wa vito familia yake ilikuwa imetajirika siku hadi siku. Zhao Shouzhen hakumsahau mfadhili wake, akajenga jumba dogo la ghorofa na kutundika mkoba huo ukutani ikionesha hatamsahau daima. Aliposikia yaya akilia alipoona mkoba, alikwenda kumwuliza aliolewa lini na hali ya njiani ilikuwaje. Xiang Lin alimweleza hali ilivyokuwa, akafahamu kuwa Xiang Ling ndiye mfadhili wake, alifurahi sana na kwa haraka alimletea nguo za gharama na kumtendea kama mgeni wa kuheshimiwa sana, na alimsaidia kuwatafuta jamaa zake.

Muda mufupi baadaye, mume wa Xiang Ling akiwa na mtoto wake pia walikuja katika sehemu ya Caizhou, alisikia kwamba mkewe alikuwa yaya katika familia ya Lu, alikwenda kwa familia hiyo, jamaa wa familia hiyo walikutana. Xiang Ling na Zhao Zhouzhen walikuwa marafiki wakubwa.