Si Lang Aenda Kumtazama Mama Yake  
中国国际广播电台

      Katika karne ya 10 hadi 12 nchini China kulikuwa na madola mawili, moja ni Dola la Liao kaskazini mashariki mwa China, moja ni Enzi ya Song, katikati ya China. Mara kwa mara madola hayo mawili yalikuwa yanapigana.

Katika Enzi ya Song kulikuwa na ukoo mmoja wa majemadari uliitwa ukoo wa Yang, baba aliitwa Yang Linggong, mama aliitwa She Taijun, walikuwa na watoto wa kiume wanane ambao wote walikuwa hodari wa kupigana vita na walitoa mchango mkubwa kwa ajili ya ulinzi wa taifa.

Mfalme wa Dola la Liao alipanga njama, akimwalika mfalme wa Enzi ya Song kwenda kufanya mazungumzo ya amani. Kutokana na kutofahamu ukweli ulivyo, ili kumlinda mfalme, mtoto wa kwanza wa ukoo wa Yang alijipamba kuwa mfalme alikwenda Dola la Liao kwa kulindwa na ndugu zake saba. Njiani walishambuliwa na askari wa Dola la Liao kwa kuviziwa, ndugu watatu waliuawa, na mtoto wa nne aliyeitwa Si Lang alitekwa nyara. Kutokana na kuwa Si Lang alitumia jina jingine Mu Yi badala la ya jina lake halisi, alifanikiwa kuwadanganya askari wa Dola la Liao.

Mama mfalme Xiao wa Dola la Liao aliona kuwa Mu Yi ana sura nzuri na ni hodari wa vita, alimwoza binti yake Tie Jing kwake, hivyo Si Lang aliyetumia jina la Mu Yi alikuwa mume wa binti wa mfalme. Waliishi vizuri na baadaye walipata mtoto mmoja wa kiume, lakini wote walikuwa hawajui kama mume wa binti wa mfalme alikuwa mtoto wa nne wa ukoo wa Yang.

 Madola mawili yaliendelea kupigana. Baada ya miaka 15 Dola la Liao kwa mara nyingine tena lilishambulia Enzi ya Song. Si Lang na binti wa mfalme na mama mfalme wote walikwenda kwenye medani ya vita. Mfalme wa Enzi ya Song alimtuma mtoto wa sita wa Ukoo wa Yang kuwa jemadari kwenda kwenye medani, na mama yake She Taijun pia alifuatana naye kuwahudumia askari na farasi kwa chakula.

Si Lang alipofahamu kwamba mama yake na ndugu yake walikuja kwenye medani ya vita aliwawazia sana akitaka kwenda kuonana nao. Lakini kutokana na sheria ya kijeshi, bila ya kibao cha ruhusa ya mfalme asingeweza kutoka kituo cha ukaguzi. Si Lang alikuwa na wasiwasi mkubwa, lakini hakuweza kumwambia mwingine ukweli wa mambo. Binti wa mfalme alipoona kila wakati mumewe alikuwa kimya na kuonekana kuwa na jakamoyo, alimdadisi. Mwishowe Si Lang alimwambia ukweli wenyewe, kwamba jina lake la ukoo ni Yang, ni jemadari wa Enzi ya Song, alitaka sana kuonana na mama yake. Si Lang alimsihi sana mkewe amsaidie kupata kibao cha ruhusa ya mfalme. Binti wa mfalme mwenye roho nzuri alimwahidi atakwenda kwa mama yake kuiba kibao hicho, lakini huku alikuwa na shaka kuwa Si Lang akienda hatarudi tena, wakati huo Si Lang aliapa atarudi usiku katika siku atakapoondoka.

Bindi wa mfalme alimchukua mtoto wake kwenda kwa mama yake, alipokuwa kwa mama yake alimfinya mtoto wake na mtoto mara alilia kwa kelele. Mama mfalme alimpenda sana mjukuu wake, mara akampakata na kumbembeleza. Binti wa mfalme alimwambia mama yake kuwa mtoto anataka kucheza na kibao cha ruhusa. Kwa kumpenda sana mjukuu wake alimpa kibao hicho na kumwambia binti yake kuwa siku ya pili akirudishe.

Si Lang akiwa na kibao cha ruhusa alipita kituo cha ukaguzi akafika kwenye kambi ya jeshi la Enzi ya Song, alionana na ndugu yake na walizungumzia hali ya vita vilivyoshindwa miaka 15 iliyopita na kusababisha kutengana kwao, ndugu wawili walikumbatiana huku wakilia. Baadaye Si Lang alikwenda kwa mama yake She Taijun. Mama mzee mwenye mvi alipoona mwana wake Si Lang asiyekuwa na habari kwa miaka mingi aliona mshtuko na furaha, mama na mwana walielezana jinsi walivyokumbukana sana. Wakati ulipita haraka, kukapambazuka, Si Lang aliagana na mama yake kwa moyo wa upendo na kurudi kambi yake.

Si Lang alipopita kituo cha ukaguzi aligunduliwa kuwa ni mume wa binti wa mfalme, mara alipelekwa mbele ya mama mfalme. Mama mfalme hakutegemea kuwa mkwe aliyemchagua ni jemadari wa Enzi ya Song, na zaidi ya hayo binti yake alimsaidia kwenda kwenye kambi ya adui kumwona mama yake, alikasirika sana, mara alitaka kumwua. Binti mfalme kwa haraka alimchukua mtoto wake kwenda kumbembeleza mama mfalme mpaka amsamehe Si Lang, na kumruhusu aweze kurudi nyumbani kumtazama mama yake.