Kibanda cha Maua ya Peony
中国国际广播电台

     Katika enzi za kale, alikuwepo mkuu mmoja wa wilaya aliyeitwa Du Bao. Mkuu huyo alikuwa na binti mmoja aliyeitwa Du Liniang, alikuwa mrembo na mwerevu. Baba yeke Du Bao alimpatia binti yake mwalimu wa kumfundisha kila siku nyumbani, na kijakazi aliyeitwa Chun Xiang pia alisoma pamoja naye, lakini kijakazi huyo alikuwa na tabia ya utukutu, mara kwa mara alikuwa anatoka nje kucheza cheza.

Katika jamii ya kimwinyi nchini China, ndoa ilikuwa inapangwa na wazazi, msichana alikuwa anaolewa na mume ambaye hata hakuwahi kumwona. Kutokana na kusoma vitabu vya kale, Du Liniang alipenda sana ndoa yake iwe kujichagulia mwenyewe.

Majira ya Spring yalifika, Chun Xiang alimwambia Du Liniang kuwa nyuma ya nyumba kuna bustani nzuri. Kwa kuwa na Du Liniang alikuwa anafuata maadili ya umwinyi, kila siku ya mwaka mzima alikuwa anajifungia chumbani kusoma na kutaziri tu. Kutokana na kushawishiwa na Chun Xiang, kisirisiri alikwenda kwenye bustani.

Mandhari ya bustani ilikuwa nzuri kweli, maua ya aina mbalimbali yalikuwa yamechanua, miti mikubwa mikubwa na ndege wa kila aina walikuwa wanalia lia na kuruka ruka. Mbele ya mandhari hiyo nzuri, Du Liniang alifikiri, kila siku alijifungia tu ndani ya nyumba, ujana wake utakuwa kama mandhari ya bustani hiyo kwamba itapotea baada ya majira, maua yatasinyaa, majani yatapukutika. Kama uzuri haukumfurahisha mtu yeyote, basi uzuri huo hauna maana yoyote. Du Liniang akiwa na wazo hilo alirudi chumbani kwake, na kutokana na uchovu mara alipata usingizi wa mang'amung'amu.

  Katika ndoto yake, alirudi tena kwenye bustani, alikutana na kijana mmoja msomi mwenye kitabu mkononi, waliongea naye. Kijana huyo alimpenda Du Liniang kwa uzuri wake na werevu wake na kumsikitikia kupoteza ujana bure. Du Liniang aliona kijana huyo kweli anamfahamu sana, alianza kumpenda moyoni mwake.

Mama yake alipokuja chumbani alimzindua Du Liniang kutoka kwenye ndoto nzuri. Baadaye alikwenda tena kwenye bustani na kutafuta ndoto yake. Mandhari ilikuwa ni ile ile, lakini kulikuwa hakuna kijana msomi. Alimtafuta tafuta na huku akimkumbuka kumbuka, asimpate. Alihuzunika sana na baada ya kurudi chumbani akawa mgonjwa. Kila siku alikuwa anakumbuka ile ndoto nzuri, alijichorea picha yake na kumwomba Chun Xiang aiweke katika bustani kwenye mlima wa bandia, muda si muda alifariki. Kabla ya kufa, aliwaomba wazazi wake wamzike katika bustani kwenye mti mmoja mkubwa, na kumwekea jiwe la kaburi.

Baadaye, wazazi wa Du Liniang walihama. Baada ya siku chache kijana mmoja msomi alipita kwenye bustani hiyo, na bahati mbaya aliugua, akapumzika karibu na bustani. Kijana huyo aliitwa Liu Mengmei, ambaye ndiye Du Liniang aliyemkuta ndotoni.

Baada ya kupona, kijana Liu Mengmei alitembelea bustani, kwa bahati aliona picha ya Du Liniang, aliona sura ya picha hiyo si ngeni kwake, akaichukua picha hiyo na kubandika ukutani. Kila siku aliiangalia na kila alipoigangalia alizidi kupenda, na aliichukulia picha kama ni mtu hai.

Du Liniang ingawa alikufa lakini alibakiza muzimu wake kwenye bustani. Alipoona kijana huyo kweli anampenda sana, basi alikuja chumbani na kukaa na kijana kila siku, na kuondoka asubuhi. Kijana Liu Mengmei alimwuliza atawezaje kuishi naye siku zote. Du Liniang alisema: Pindi akifukua kaburi lake, atafufuka. Kijana huyo alifurahi sana, na mara akaenda kwenye kaburi, akafukua kaburi na Du Liniang kweli alifufuka, alikuwa mrembo kama zamani. Tokea hapo walikuwa mume na mke na kuishi kwa furaha kila siku.

Hadithi ya msichana Du Liniang aliyekufa kwa ajili ya mapenzi na kufufuka kwa ajili ya mapenzi vile vile inawasisimua watu wengi.