Baraza la serikali la China na wizara zake

中国国际广播电台

Baraza la serikali
Baraza la serikali la China yaani serikali kuu ya umma, ni chombo kikuu cha mambo ya utawala cha nchi. Baraza hilo linatekeleza sheria na maazimio yaliyopitishwa na Bunge la umma la China na halmashauri yake ya kudumu, na kuwajibika pia kutoa ripoti ya kazi kwa Bunge la umma la China na halmashauriano yake ya kudumu,. Baraza la serikali lina madaraka ya kuweka hatua za utawala, kubuni sheria na kanuni za utawala, na kutoa maazimio na maagizo ndani ya madaraka yake. Baraza la serikali linaundwa na waziri mkuu, manaibu mawaziri, wajumbe wa kitaifa, mawaziri wa wizara mbalimbali, wakurugenzi wa kamati mbalimbali, mkaguzi mkuu wa uhasibu, na katibu mkuu. Waziri mkuu wa hivi sasa ni Bwana Wen Jiabao.

Hivi sasa Baraza la serikali la China linaundwa na wizara na kamati 28 kama vile Wizara ya mambo ya nje, Wizara ya ulinzi wa taifa, Kamati ya maendeleo na mageuzi ya taifa, Wizara ya elimu, Wizara ya sayansi na teknolojia, Kamati ya viwanda vya sayansi na teknolojia za ulinzi wa taifa, Kamati ya mambo ya makabila madogomadogo, Wizara ya usalama wa umma, Wizara ya usalama wa nchi, Wizara ya mambo ya kiraia, Wizara ya sheria, Wizara ya fedha, Wizara ya ajira, Wizara ya kazi na huduma za jamii, Wizara ya reli, Wizara ya mawasiliano, Wizara ya maliasili ya ardhi ya taifa, Wizara ya ujenzi, Wizara ya shughuli za upashanaji habari, Wizara ya maji, Wizara ya utamaduni, Wizara ya afya, Wizara ya Kilimo, Wizara ya biashara, Kamati ya idadi ya watu na uzazi wa mpango, Benki ya umma ya China na Idara kuu ya ukaguzi wa uhasibu.

Wizara ya mambo ya nje
Wizara ya mambo ya nje ni wizara ya Baraza la serikali inayowajibika na utekelezaji wa sera za China kwa nchi za nje na kushughulikia kazi ya kiplomasia ya kila siku. Jukumu kuu la wizara hiyo ni kuwakilisha taifa na serikali kusimamia mambo ya kidiplomasia kama vile kutangaza sera na maamuzi ya taifa kwa nchi za nje, kutangaza nyaraka na taarifa kuhusu mambo ya kidiplomasia; kushughulikia mambo ya kidiplomasia na kufanya mawasiliano ya kidiplomasia, kusaini mikataba, makubaliano na nyaraka nyingine za kidiplomasia; kuhudhuria mikutano ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa na kati ya serikali na serikali na kushiriki kwenye shughuli za jumuiya za kimataifa; kushughulikia kazi ya kuanzisha ubalozi na ofisi husika za wawakilishi katika nchi za nje, kuwasimamia watumishi wa serikali wanaofanya kazi katika idara hizo, kuelekeza, kushirikisha na kuratibu shughuli za kidiplomasia kati ya idara za mambo ya nje katika wizara mbalimbali za Baraza la serikali na mikoa, mikoa inayojiendesha na miji inayotawaliwa moja kwa moja na serikali kuu, na kushughulikia kazi ya kuwaandaa na kuwasimamia makada wa kidiplomasia.
Waziri wa mambo ya nje wa China wa hivi sasa ni Bwana Li Zhaoxing.

Kamati ya maendeleo na mageuzi ya nchi
Jukumu la kamati hiyo ni kubuni na kutekeleza mikakati ya maendeleo ya uchumi na jamii, mipango ya muda mrefu na wastani na mipango ya mwaka; kufanya utafiti na uchambuzi kuhusu hali ya uchumi wa nchini na ng’ambo na maendeleo ya hali hiyo, kufanya makadirio na kutoa tahadhari kuhusu uchumi wa taifa; kufanya utafiti kuhusu masuala muhimu yanayohusika na usalama wa uchumi wa taifa, kutoa mapendekezo kuhusu sera za marekebisho na udhibiti wa uchumi, kufanya usawazishaji wa maendeleo ya uchumi na jamii; kufanya mipango kuhusu miradi mikubwa na nguvu kazi nchini; kufanya mipango kuhusu fedha za ujenzi za taifa, kuelekeza na kusimamia matumizi ya fedha za mikopo kutoka nchi za nje kwa ujenzi wa China, na kuelekeza na kusimamia mwelekeo wa matuizi ya mikopo ya kisera; kuelekeza mwelekeo wa fedha za raia katika uwekezaji wa mali zisizohamishika; kufanya utafiti na kutoa malengo na sera za kimkakati kuhusu matumizi ya mitaji na uwekezaji kutoka nje; kupanga miradi ya ujenzi inayogharimiwa na serikali na miradi mikubwa ya ujenzi, miradi mikubwa ya uwekezaji wa nje, miradi ya uendelezaji wa maliasili na miradi ya uwekezaji mkubwa katika nchi za nje; kubuni na kutunga sheria na kanuni husika za utawala kuhusu maendeleo ya uchumi na jamii ya taifa pamoja na mageuzi ya mfumo wa uchumi, kuzifungulia mlango nchi za nje, na kushiriki kazi za kutunga sheria na kanuni za utawala na utekelezaji.
Mkurugenzi wa sasa wa Kamati ya maendeleo na mageuzi ya taifa ni Bwana Ma Kai.

Wizara ya biashara
Wizara hiyo ilianzishwa rasmi mwezi Machi mwaka 2003.
Jukumu lake kuu ni kubuni mikakati, mwongozo na sera kuhusu maendeleo ya biashara nchini na ng’ambo na ushirikiano wa kimataifa wa sekta ya uchumi, kutunga sheria na kanuni kuhusu biashara ya nchini na ng’ambo, ushirikiano wa kiuchumi wa kimataifa na uwekezaji wa wafanyabiashara kutoka nje; kubuni mipango ya maendeleo ya biashara ya nchini, kufanya utafiti na kutoa maoni kuhusu mageuzi ya utaratibu wa mzunguko wa bidhaa, kuandaa na kuendeleza soko mijini na vijijini; kufanya utafiti kwa kubuni sera kuhusu utaratibu kamili wa uendeshaji wa soko, utaratibu wa mzunguko wa bidhaa na kuvunja ukiritimba wa soko na vikwazo vya kisehemu, kujenga mfumo wa soko wenye utaratibu kamili, wa kufunguliwa mlango na wa ushindani; kufuatilia na kuchambua hali ya uendeshaji wa soko na hali ya utoaji wa bidhaa sokoni, kutekeleza hatua za marekebisho na udhibiti kuhusu bidhaa muhimu za matumizi sokoni na usimamizi wa mzunguko wa raslimali muhimu za uzalishaji; kufanya utafiti na kubuni njia za usimamizi wa bidhaa ziagizwazo kutoka nje na ziuzwazo kwa nje pamoja na orodha ya bidhaa hizo, kutekeleza mipango ya mgao wa kuagiza bidhaa na kuuza bidhaa, kuthibitisha kiasi cha mgao na kutoa kadi za kibali; kutunga na kutekeleza sera kuhusu zabuni ya mgao wa bidhaa ziagizwazo kutoka nje na ziuzwazo kwa nje; kuratibu kazi ya kupinga mauzo ya bidhaa nyingi za bei chini, kupinga utoaji ruzuku, kutoa hatua za uhakikishaji na kazi nyingine zinazohusika na biashara ya haki, kuanzisha utaratibu wa utoaji tahadhari kuhusu biashara ya haki, kufanya uchunguzi kuhusu hasara za mashirika; kuelekeza na kuratibu kazi ya kujibu mashitaka kuhusu bidhaa za China zilizouzwa nje na kazi nyingine zinazohusika.