Chama cha kikomunisti cha China

中国国际广播电台Chama cha kikomunisti cha China ni chama cha watangulizi wa tabaka la wafanyakazi wa China, pia ni chama cha watangulizi wa wananchi wa China na taifa la China. Chama hicho ni kiini cha uongozi wa jitihada za ujenzi wa mambo ya ujamaa wenye umaalum wa kichina, ambacho kinawakilisha matakwa ya maendeleo ya nguvukazi ya kisasa ya China, kuwakilisha mwelekeo wa kusonga mbele wa utamaduni wa kisasa wa China na kuwakilisha maslahi ya kimsingi ya wanachi wengi kabisa wa China.

Tumainio kubwa kabisa na lengo la mwisho la Chama cha kikomunisti cha China ni kutimiza ukomunisti. Katiba ya chama hicho inaeza kuwa, dira ya vitendo vya Chama cha kikomunisti cha China ni Umax-Lenin, Fikra Mao Zedong, Nadharia ya Deng Xiaoping na wazo muhimu la “Uwakilishi mtatu”.

Chama cha kikomunsti cha China kilizaliwa mwezi Julai mwaka 1921. Toka mwaka 1921 hadi 1949, chama hiki kiliwaongoza wananchi wa China katika kufanya mapambano magumu, na kupindua utawala wa ubeberu, umwinyi na ubepari wa utawala msonge, hatimaye kuanzisha Jamhuri ya Watu wa China. Baada ya kuzaliwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, Chama cha kikomunsti cha China kiliwaongoza wananchi wa makabila mbalimbali wa nchi nzima katika kulinda uhuru na usalama wa nchi, kufanikiwa kuiwezesha jamii ya China ibadilike kuwa jamii ya ujamaa badala ya jamii ya demokrasia mpya, na kuanzisha ujenzi mkubwa wa ujamaa kwa kufuata mipango, na kuyafanya mambo ya uchumi na utamaduni ya China yapate maendeleo makubwa sana ambayo hayakupatikana katika historia.

Baada ya kukamilisha kimsingi mageuzi ya kiujamaa ya mfumo wa umilikaji wa binafsi wa raslimali za uzalishaji mwaka 1956, kutokana na ukosefu wa uzoefu, Chama cha kikomunisti cha China kiliwahi kufanya makosa kadhaa katika mchakato wa kuongoza ujenzi wa ujamaa; na makosa makubwa yaliyowahi kufanyika ni “mapinduzi makubwa ya utamaduni” kote nchini kwa muda mrefu, tokea mwaka 1966 hadi 1976.
Mwezi Oktoba mwaka 1976, “mapinduzi makubwa ya utamaduni” yalikomeshwa, China ikaingia katika kipindi kipya cha maendeleo ya historia. Baada ya kufanyika kwa mkutano wa 3 wa wajumbe wote wa Kamati kuu ya 11 ya Chama cha kikomunisti cha China mwishoni mwa mwaka 1978, mabadiliko makubwa yenye umuhimu mkubwa yalipatikana tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China. Kuanzia mwaka 1979, Chama cha kikomunisti cha China kilitekeleza sera iliyopendekezwa na Deng Xiaoping kuhusu kufanya mageuzi na kuzifungulia mlango nchi za nje. Tokea sera hiyo ianze kutekelezwa, mafanikio makubwa ya kuvutia dunia nzima yalipatikana katika maendeleo ya uchumi na jamii ya China, ambapo sura ya nchi ilipata mabadiliko makubwa kabisa, kipindi hiki ni kipindi chenye hali nzuri kabisa tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, vilevile ni kipindi ambacho wananchi walipata manufaa makubwa kabisa.

Chama cha kikomunisti cha China kinatetea kufanya juhudi za kuendeleza uhusiano na nchi za nje na kufanya juhudi za kujipatia mazingira ya kimataifa yanayosaidia mageuzi na ufunguaji mlango na ujenzi wa mambo ya kisasa ya China. Katika mambo ya kimataifa, Chama cha kikomunisti cha China kinashikilia sera ya kidiplomasia ya amani ya kujitawala na kujiamulia mambo, kulinda uhuru na mamlaka ya nchi ya China, kupinga umwamba na siasa ya mabavu, kulinda amani ya dunia na kusukuma mbele maendeleo ya binadamu; kuendeleza uhusiano na nchi mbalimbali duniani kwa msingi wa kanuni tano za kuheshimu mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi, kutoshambuliana, kutoingiliana mambo ya ndani, kuwa na usawa na kunufaishana, na kuishi pamoja kwa amani. Chama cha kikomunisti cha China kimeanzisha na kuendeleza uhusiano wa kirafiki na vyama vya nchi mbalimbali kwa kufuata kanuni nne za kujitawala na kujiamulia, kuwa na usawa kabisa, kuheshimiana na kutoingiliana mambo ya ndani. Hivi sasa Chama cha kikomunisti cha China kimedumisha mawasiliano ya kirafiki na vyama zaidi ya 300 vya nchi zaidi ya 120 duniani.

Chama cha kikomunisti cha China ni umoja unaojumuika kwa kufuata mwongozo na katiba yake na utaratibu wa utawala wa kidemokasia. “Katiba ya Chama cha kikomunisti cha China” inaeleza kuwa, watangulizi wa wafanyakazi, wakulima wanajeshi, wasomi na wengine wa jamii, yeyote aliyetimia umri wa miaka 18, anayetambua mwongozo na katiba ya chama, anayependa kujiunga na jumuiya ya chama na kufanya kazi kwa bidii ndani yake, anayetekeleza maazimio ya chama na kutoa ada ya mwanachama kwa wakati, anaweza kutoa ombi la kujiunga na Chama cha kikomunisti cha China.
Vyombo vya kamati kuu ya chama ni pamoja na Bunge la umma la China, Kamati kuu ya chama, Ofisi ya siasa ya Kamati kuu ya chama, Kamati ya kudumu ya Ofisi ya siasa ya kamati kuu ya chama, Sekretarieti ya Kamati kuu ya chama, Kamati ya kijeshi ya Kamati kuu ya chama na Kamati kuu ya ukaguzi wa nidhamu. Mkutano wa wajumbe wa nchi nzima wa chama unafanyika mara moja kila mwaka. Wakati mkutano huo unapofungwa, Kamati kuu ya chama ni chombo cha uongozi wa juu kabisa cha Chama cha kikomunisti cha China.
Chama cha kikomunisti cha China hivi sasa kina wanachama karibu milioni 70, katibu mkuu wa chama hicho ni Xi Jinping.