"Njia ya Hariri"
Radio China Kimataifa

"Njia ya Hariri" iliyofunguliwa miaka elfu mbili iliyopita inajulikana sana duniani. Hii ni njia kama daraja kati ya China na nchi za Ulaya, Asia na Afrika, na ilitoa mchango mkubwa katika biashara ya mabadilishano ya vitu kati ya Mashariki na Magharibi.

"Njia ya Hariri" ilisafirisha hariri za China hadi Magharibi. Kutokana na uchunguzi njia hiyo ilianza katika Enzi ya Han, wakati huo njia hiyo ya upande wa kusini ilielekea magharibi hadi Afghnistan, Iran na Misri, njia nyingine ilipitia Pakistan, Kabul nchini Afghanistan, na kufikia Karach nchini Pakistan na kutoka Persia kufikia Rome.

Tokea karne ya pili K.K. hadi karne ya pili, njia hiyo iliunganisha nchi nne kubwa, nchi hizo zilikuwa ni Rome, Parthia (Iran ya kale), Kushan (Asia ya kati) na Enzi ya Han ya China. Tokea hapo maendeleo ya utamaduni wa nchi yoyote hayakuwa ya nchi moja tu.

Tokea karne ya 7 hadi karne ya 9 katika Enzi ya Tang, biashara iliyofanywa kwa kutumia njia hiyo ilikuwa ya kufana kabisa, bidhaa nyingi za China zilisafirishwa nchi za nje na bidhaa za nchi za Magharibi ziliingizwa nchini China. Pamoja na bidhaa, vyombo vya vioo, wanyama, vito na lulu, ubani, muziki na dansi pia ziliingizwa nchini China, na pamoja na hariri, ufundi wa kutengeneza karatasi, uchapaji, baruti, dira na vyombo vya vanishi pia vilijulikana katika nchi za Magahribi.

Kadhalika, dini ya Buddha ilijulishwa nchini China katika Enzi ya Han Magharibi (206-220), picha zilizochorwa kwenye kuta za mapango yaliyochongwa katika karne ya 3 mkoani Xinjiang zimeonesha wazi jinsi dini ya Buddha ilivyoingia nchini China kutoka India.

Hadi kufikia karne ya 9, kutokana na mabadiliko ya uchumi na siasa katika nchi za Ulaya, na hasa kutokana na maendeleo ya uchukuzi wa baharini, njia hiyo ilianza kuzorota. Hadi kufikia karne ya 10 yaani Enzi ya Song, njia hiyo haikutumika sana kwa ajili ya biashara.

"Njia ya Hariri" ni ndefu na ilikuwa na miaka mingi, iliwahi kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya ustaarabu duniani. Katika miaka ya karibuni UNESCO imetoa wito wa kuanzisha "uchunguzi mpya wa njia mpya ya hariri", na kuipatia "njia ya hariri" kuwa "njia ya mazungumzo" ili kustawisha mazungumzo na maingiliano kati ya Mashariki na Magharibi.