Kaburi la Yi na Kengele Mfululizo
Radio China Kimataifa

Kwa mujibu wa maandishi ya kale, watawala wa enzi za kale nchini China walitilia maanani sana muziki. Kila wanapofanya sherehe walikuwa wakiburudika na muziki, na waliona muziki ni dalili ya ustawi wa taifa. Mwaka 1978, kengele mfululizo za muziki zilifukuliwa kutoka kaburi la mtu wa kale Yi katika mji wa Suizhou, mkoani Hubei.

Februari mwaka 1978 sehemu moja ilipojengwa, wajenzi waligundua sehemu ya "udongo wenye rangi nyeusi" tofauti na sehemu nyingine. Baada ya kuchimba waligundua kaburi lenye urefu wa mita 21 na upana wa mita 16. Baada ya kufumua kaburi hilo waligundua vitu zaidi ya 15,000 vya vyombo vya shaba nyeusi, ala za muziki, silaha, vyombo vya dhahabu na vya mianzi, lakini kilichovutia zaidi ni kengele mfululizo 65 za shaba nyeusi.

Kengele kubwa ina kimo cha sentimita 153.4 na ndogo ina urefu wa sentimita 20.4, jumla ya uzito ni kilo 2500, kuna maneno 2800 yaliyochongwa kwenye kengele hizo. Kila kengele ina sauti mbili za muziki, na zinaweza kupigwa muziki wa aina yote.

Kwa kufanya utafiti wataalamu wamethibitisha kuwa kwenye kaburi hilo alizikwa mtu aliyeitwa Yi ambaye alikuwa mtemi wa Dola la Zeng, na mtu huyo alizikwa kiasi cha miaka 400 K.K.

Kutokana na kuwa kaburi hilo lilikuwa ndani ya maji chini ya ardhi, vitu ndani ya kaburi havikuharibika na kwa sababu ya maji, vitu kwenye kaburi hilo havikuibiwa.

Baada ya kufukua kengele mfululizo, serikali ya mkoa ilijenga jumba la maonesho, na kaburi lilirudishwa kama awali, na vilevile imeundwa bendi ya kupiga muziki kwa kengele hizo.