Makaburi ya Wafalme wa Dola la Xixia
Radio China Kimataifa

Ugunduzi wa kaburi la mfalme wa Dola la Xixia ni ugunduzi mkubwa wa mambo ya kale katika karne ya 20 nchini China, kaburi hilo liko katika sehemu ya kaskazini magharibi ya China.

Miaka 770 iliyopita, nchini China kulikuwa na enzi tatu za kifalme kwa pamoja, nazo ni Song, Liao na Xixia.

Dola la kifalme Xixia lilikuwa na lugha na maandishi yake, lakini kwa bahati mbaya, mwaka 1227 liliposhambuliwa na jeshi la kabila la Wamongolia maandishi yote yalichomwa moto, kwa hiyo habari kuhusu maandishi ya dola hilo imekuwa kitendawili.

Mwanzoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita makaburi ya wafalme wa Dola la Xixia yaligunduliwa, na katika muda wa miaka 30 wataalamu wa mambo ya kale walifanya uchunguzi mara nyingi na kupiga ramani katika sehemu ya makaburi na kimsingi wamethibitisha makaburi ya wafalme yalipo na hali ya ndani ya makaburi hayo.

Makaburi ya wafalme yako katika sehemu ya jangwa yenye kilomita za mraba 50, kwa jumla kuna makaburi tisa ya wafalme na makaburi ya matajiri 250. Sehemu hiyo ya makaburi ni kubwa ambayo inaweza kulingana na sehemu ya makaburi ya wafalme wa Enzi ya Ming mjini Beijing. Kila moja kati ya makaburi ya wafalme tisa lilijengwa kwa umbo la mstatili kutoka kaskazini hadi kusini.

Kaburi la Nam. tatu kati ya makaburi tisa lina eneo kubwa zaidi, wataalamu wanaona kuwa kaburi hilo ni la mfalme wa kwanza wa Dola la Xixia, Li Yuanhao.

Pagoda ndani ya sehemu ya makaburi hayo inasifiwa kama ni "piramidi ya Mashariki". Mnara una pembe nane, na kipenyo kirefu kina urefu wa mita 34, na kinapungua jinsi mnara unavyokwenda juu, lakini hivi sasa ni vigumu kuthibitisha kama mnara huo ulikuwa na matabaka matano au saba.

Katika ugunduzi uliofanyika tarehe 30 Aprili mwaka 2000 katika kaburi la namba tatu, wataalamu waligundua sanamu yenye mwili wa ndege na kichwa cha binadamu. Wataalamu walisema, sanamu hiyo ni pambo katika hekalu la dini ya Buddha.

Hivi sasa vitu zaidi ya laki moja vimegunduliwa katika sehemu hiyo, ambavyo ni thamani kubwa kwa ajili ya utafiti wa utamaduni wa Dola la Xixia.