Sanda Iliyotengenezwa kwa Vito
Radio China Kimataifa

Katika Enzi ya Han Magharibi nchini China yaani kuanzia mwaka 206 kabla ya kuzaliwa Kristo hadi mwaka 8, watu waliamini maiti wangeweza kuhifadhiwa bila kuoza. Kutokana na mawazo hayo, wafalme na matajiri wa enzi hiyo walitumia sanda zilizotengenezwa kwa vito kuhifadhi maiti zao. Mwaka 1968 katika mji wa Mancheng, mkoani Hebei, kaskazini mwa China wataalamu wa mambo ya kale kwa mara ya kwanza waligundua sanda kama hiyo.

Katika wilaya ya Mancheng mkoani Hebei umbali wa kilomita 200 kutoka Beijing lilikuwepo kaburi moja alimozikwa mfalme wa kwanza wa Dola la Zhongshan katika Enzi ya Han, Liu Sheng, na mkewe Dou Wan kwa pamoja. Kutokana na maandishi ya kihistoria, Liu Sheng alipata ufalme wa Dola la Zhongshan mwaka 154 K.K. na alitawala kwa miaka 42. Huyo ni mfalme wa kwanza katika dola hilo.

Kaburi hilo lilijengwa kwenye kilima kimoja kizima. Ndani ya kaburi hilo kuna mapango mengi yaliyotumika kwa kazi mbalimbali kama vile kulala, sebule na muziki. Kwa hiyo kaburi hilo ni kama kasri kubwa mlimani.

Kutokana na namna mapango yalivyopangwa kibusara, inaonesha kwamba kaburi hilo lilikuwa limesanifiwa kwa makini kabla ya kuchimbwa, na kazi hiyo ilikuwa ngumu sana. Uchongaji wa mapango hayo makubwa kwenye mlima wa mawe hata sasa ungehitaji muda wa mwaka mzima kwa watu zaidi ya mia moja na vyombo vya kazi vya kisasa.

Ndani ya kaburi kulikuwa na vitu vingi vya kafara, ambavyo viliwekwa kwa mpangilio mzuri, na miongoni mwa vitu hivi vyombo vya udongo ni vingi zaidi, vingine ni vya shaba, chuma na fedha. Lakini vilivyostaajabisha zaidi ni "sanda iliyotengenezwa kwa vito vilivyounganishwa kwa nyuzi za dhahabu".

"Sanda" hiyo ilitengenezwa kwa kuunganisha vipande vya mawe vyenye maumbo ya mstatili, mraba, pembe tatu n.k. na kila kipande kwenye kona kuna tundu kwa ajili ya kupitisha uzi wa dhahabu. Sanda hiyo ina sehemu ya kichwa, nguo, suruali, glavu na viatu. Ina urefu wa jumla ya mita mbili na vipande vya mawe 2498, nyuzi za dhahabu kiasi cha gramu 1100. kwenye sehemu ya kichwa kuna vizibo vya macho, pua, masikio na kinywa. Na kwenye sehemu ya kiuno kuna kikasha cha kufunika sehemu za siri.

Kutokana na maelezo ya wasomi, utengenezaji wa sanda kwa vipande vya mawe ni mgumu sana, kwanza mawe yahitajika kukatwa vipande vidogo na vyembamba kulingana na mwili kwa ukubwa tofauti na halafu kutoboa matundu ili kuunganishwa pamoja. Kwa kupima, baadhi ya nyufa kati ya vipande vizima ni milimita 0.3 tu, huu ni ufundi mkubwa kweli.

Kwenye pango la mke wa mfalme Liu Shen, imegunduliwa sanda nyingine ya mawe ambayo pia ina sehemu tano kama ya kichwa, nguo, suruali, glavu na viatu ila tu ni fupi kidogo ikilinganishwa na sanda ya mume wake. Sanda hizi mbili ni nzima hadi sasa, ambapo ni mara ya kwanza kupatikana zikiwa nzima. Ugunduzi wake umetufahamisha zaidi sanda ya vipande vya mawe katika Enzi ya Han.

Mbali na sanda za vito, kutoka kaburi la Liu Sheng pia zimegunduliwa sindano za tiba na beseni zenye neno "tiba", ambazo ni vitu halisi vinavyothibitisha hali ya utibabu na akyupancha katika siku za kale nchini China. Upanga aliokuwa nao kiunoni mfalme Liu Sheng unaonesha kufuliwa mara kadhaa, na umeonesha ufundi mkubwa wa kuyeyusha chuma cha pua katika siku za kale.

Kutokana na thamani kubwa ya kaburi hilo la Enzi ya Han, mwaka 1988 liliorodheshwa kwenye kumbukumbu za taifa.