Utamaduni wa Dola la Yelang
Radio China Kimataifa

"Ujeuri wa Yelang" ni usemi unaojulikana kwa wote wa China. Usemi huo ulitokana na hadithi iliyotokea miaka 2000 iliyopita katika Dola la Yelang, kusini magharibi mwa China. Dola hilo liliwahi kustawi kwa miaka mia moja hivi, lakini baada ya muda huo likatoweka haraka kama kimwondo. Mwanzoni mwa karne hii wataalamu wa mambo ya kale walifumua siri za dola hilo.

Mwezi Septemba mwaka 2001 makaburi 108 ya dola la Yelang yaligunduliwa katika wilaya ya Hezhang, mkoani Guizhou, kusini magharibi mwa China. Dola la Yelang lilikuwa la kabila dogo lililokuwa katika karne ya tatu K.K. hadi karne ya kwanza. Dola hilo lilikuwa na ustawi mkubwa na jeshi lake hata lilikuwa na askari laki moja. Kutokana na kuwa dola hilo lilikuwa milimani na likijitenga na sehemu nyingine, kwa hiyo mfalme wa dola hilo alipokutana na mjumbe wa Enzi ya Han Magharibi alimwuliza, "Dola lako na langu Yelang lipi ni kubwa?". Mfalme wa Dola la Yelang aliuliza hivyo kwa kutojua kwamba Enzi ya Han Magharibi ni dola kubwa kiasi gani. Tokea hapo "ujeuri wa Yelang" umekuwa usemi wa kudhihaki mjeuri, lakini kwa upande mwingine umethibitisha kwamba kweli Dola la Yelang lilikuwepo.

Lakini dola hilo lilitoweka ghafla, na historia yake na utamaduni wake umekuwa mafumbo katika historia ya China. Ugunduzi wa makaburi ya dola la Yelang uliopatikana katika mwaka 2001 umekuwa mkubwa kabisa katika mwaka huo nchini China.

Makaburi yote yalikuwa karibu sawa, na si makubwa, kila moja lina urefu wa mita tatu na upana wa kiasi cha mita moja. Kitu cha ajabu kilichogunduliwa ndani ya makaburi hayo ni kuwa kila maiti imefunikwa na kitu kama beseni ya shaba kwenye kichwa na miguu. Wataalamu wanaona kuwa mila ya kufunika maiti kwa beseni ya shaba inaonesha kuwa watu wa Dola la Yelang walikuwa na imani kwa vitu vya kusafishia, na baadhi ya wataalamu wanaona kuwa mila hiyo inahusika na imani ya dini fulani.

Makaburi yaliyogunduliwa wilayani Hechang yamewapatia watu wa leo ufunguo wa kufungua siri za utamaduni wa dola hilo, lililokuwepo miaka elfu mbili iliyopita.