Vyombo vya Kauri na China
Radio China Kimataifa

 

Neno "China" katika Kiingereza lina maana ya taifa la China na pia lina maana ya vyombo vya kauri, lakini kuna uhusiano gani kati ya China na vyombo vya kauri?

Uchunguzi wa mambo ya kale umethibitisha kwamba vyombo vya kauri nyeupe tulivyo navyo hivi leo vilitokana na vyombo vya kauri nyeusi, na vyombo vya kauri nyeusi vilitokana na vyombo vya udongo. Vyombo vya kauri nyeusi vilikuwa na tabia ya vyombo vya udongo kama vyombo vya kauri nyeupe. Vyombo hivyo vya kauri nyeusi vilivyokuwa vya zamani sana viligunduliwa kutoka magofu ya Longshan wilayani Xia katika mkoa wa Shanxi, ambavyo hadi leo vimekuwa na miaka 4200.

Vyombo halisi vya kauri vilianza hasa katika Enzi ya Han Mashariki, enzi ambayo ilianzia mwaka 23 hadi 220. Mwanzoni vilianza kutengenezwa katika sehemu ya akusini mwa China mkoani Zhejiang, baadaye ufundi huo ulienea hadi kaskazini na ukapata maendeleo makubwa na kutokea ufundi wa kutengenezea vyombo vya kauri nyeupe. Tofauti iliyopo kati ya kauri nyeusi na nyeupe ni kiasi cha chuma ndani ya udongo. Udongo wenye kiasi kidogo cha chuma unaonekana mweupe baada ya kuchomwa na wenye kiasi kikubwa utaonekana wa kijivujivu au mweusi kidogo. Awali, vyombo vya kauri vilikuwa havina rangi lakini baada ya kutokea kwa vyombo vya kauri nyeupe watu wakapaka rangi tofauti za kioo lakini rangi tawala huwa nyeupe, hivyo rangi tofauti huonekana wazi na kupendeza zaidi. Kwa hiyo, kutokea kwa kauri nyeupe kuna maana kubwa katika maendeleo ya vyombo vya kauri.

Katika enzi za Tang na Song yaani toka karne ya 10 hadi mwanzoni mwa karne ya 13, ufundi wa kutengenezea vyombo vya kauri uliendelea mbele kwa hatua nyingine kubwa. Vyombo vya kauri vyenye rangi tatu vilianza kutengenezwa katika kipindi hicho. Vyombo hivyo vilipakwa rangi tatu maalumu za kioo kabla ya kuchomwa, na wakati wa kuchomwa ndani ya tanuru rangi hizo zikabadilika kikemikali na zikawa na rangi nyingi zaidi, matokeo yake ni kama picha za kuchorwa za mtindo wa Kichina, rangi hizo zinajulikana kama rangi tatu za Enzi ya Tang.

Katika Enzi ya Ming, enzi ambayo ilianzia mwaka 1368 hadi 1644 na Enzi ya Qing iliyoanzia mwaka 1644 hadi 1911 ufundi wa kutengenezea vyombo vy akauri ulifikia kwenye kiwango kikubwa kwa idadi au kwa ubora. Mji uliopo kusini mwa China uitwao Jingdezhen ulikuwa "mji wa kauri" hasa uliojulikana katika enzi hizo unaendelea na sifa yake hadi leo, na takriban vyombo vyote vya kauri vya hali ya juu vinatengenezwa katika mji huo. Vyombo vya kauri vya China vilianza kusafirishwa hadi nchi za nje katika karne ya 8, kabla ya hapo njia ya hariri iliyojulikana kote duniani ilikuwa ikiunganisha biashara za China na nchi za nje. Katika karne hiyo ya 8 pamoja na kusafirisha nje vyombo vya kauri, China ikajulikana duniani kwa jina jingine la "nchi ya kauri".

Mwanzoni vyombo vya kauri viliuzwa katika Asia tu, baada ya karne ya 17 vikaanza kuwa mapambo ya fahari ndani ya kasri ya kifalme katika Ulaya ya Magharibi. Baada ya Ureno kufungua njia ya usafiri baharini, vyombo vya kauri vya China vikaanza kuwa zawadi kubwa katika Ulaya nzima. Katika zama hizo mtindo wa sanaa uitwao Rococo ulioenea katika Ulaya ulilingana na sanaa za kauri za China, hii ilikuwa sababu ya vyombo vya kauri kuenea sana katika Ulaya nzima. Kutokana na takwimu isiyokamilika, katika karne ya 17 vyombo vya kauri vya China vilivyosafirishwa nchi za nje vilifikia laki 2 kila mwaka na ilipofika karne ya 18 viliongezeka hadi milioni. Vyombo vya kauri viliuzwa kote duniani, kadhalika neno "china" pia likaenea pamoja na vyombo hivyo katika Uingereza na bara la Ulaya. Neno "china" likawa na maana mbili, yaani vyombo vya kauri na jina la nchi. Ingawa hatuwezi kubainisha kwamba toka lini neno "china" limekukwa jina la nchi, lakini tuna uhakika kwamba ndio sababu ya ufundi wa kutengenezea vyombo vya kauri vinavyowapendeza sana watu wa dunia umeungaisha vyombo vya kauri pamoja na jina la nchi, China.