Mji wa Kale wa Lijiang
中国国际广播电台

      Mji wa Lijiang ulianza kujengwa mwishoni mwa Enzi ya Song na mwanzoni mwa Enzi ya Yuan (mwishoni mwa karne 13). Eneo la mji huo ni kilomita za mraba 3.8.

Ndani ya mji huo kuna mito midogo mingi, barabara zilitandazwa kwa mawe mekundu, katika siku za mvua hakuna matope, na katika siku ya kiangazi hakuna vumbi. Kutokana na kuwepo kwa mito mingi kuna madaraja mengi, kwenye eleo la kilomita moja kuna madaraja 93, na kati ya madaraja hayo mengi, baadhi yalijengwa katika enzi za Ming na Qing (karne ya 14-19).

Jumba ndani ya mji huo liitwalo Mu Fu lilijengwa katika Enzi ya Yuan (1271-1368), mwaka 1998 lilibadilishwa kuwa jumba la makumbusho la mji. Ndani ya jumba hilo zimeoneshwa mbao 11 zenye maandishi ya wafalme wa enzi mbalimbali.

   

  Jumba la Wu Feng Lou lilijengwa mwaka 1601. Urefu wa jumba hilo ni mita 20. Jumba hilo lilijengwa kwa mchanganyiko wa mitindo ya makabila ya Wahan, Watibet na wanaxi, ni jengo lenye thamani kubwa katika majengo ya kale nchini China.

Sehemu ya makazi iko upande wa kaskazini wa mji. Sehemu hiyo ilikuwa ni kituo cha siasa, uchumi na utamaduni katika Enzi ya Song. Sehemu hiyo iliweka msingi wa ujenzi wa mji wa kale wa Lijiang.

Sehemu nyingine ya makazi iliyoko upande wa kaskazini magharibi mwa mji huo, hapo mwanzo ilikuwa ni soko, makazi yalijengwa katika Enzi ya Ming (1368-1644).

Mji wa Lijing una historia ndefu, wakazi wa mji huo ni wa kabila la Han, Bai, Yi na Tibet. Utamaduni katika mji huo ni wa makabila tofauti.

 

 

  Kutokana na historia ndefu na mchanganyiko wa watu wa makabila tofauti, mitindo ya majengo, mila na desturi za wenyeji pia ni tofauti. Mji huo ni urithi mkubwa wa utamaduni duniani, na unasaidia sana wataalamu kufanya utafiti wa mambo ya kale.

Mwezi Desemba mwaka 1997 mji huo uliorotheshwa na UNESCO kwenye urithi wa dunia.