Ukuta Mkuu
中国国际广播电台

      China ni nchi yenye historia ndefu na utamaduni mkukbwa, na vivutio vingi vya utalii. Kumbukumbu nyingi za mandhari ya kimaumbile na za utamaduni zinadhihirisha akili nyingi na juhudi kubwa za watu wa China ya kale. Mwaka 1985 serikali ya China ilijiunga na “Mkataba wa Uridhi wa Dunia”, na mwaka 1987, kumbukumbu 6 za urithi wa China ikiwa ni pamoja na Ukuta Mkuu na Kasri ya Kifalme ya China viliwekwa kwenye orodha ya urithi wa dunia.

  Ukuta Mkuu unasifiwa kama ni “moja katika maajabu 7 ya dunia” ni jengo kubwa ambalo lilitumia miaka mingi na kazi kubwa duniani, katika ngoma zote za kuzuia maadui katika zama za kale. Ukuta huo una urefu wa zaidi ya kilomita 7,000.

Historia ya ujenzi wa ukuta huo inaweza kufuatiliwa hadi karne ya 9 kabla ya Kristo. Katika kipindi cha “Madola Kivita” kilichokuwa kati ya mwaka 770 K.K. na 476 K.K. madola yalikuwa yakipigana vita na kila moja likitaka kuliangamiza lingine ili kupata utawala wa China nzima, kutokana na sababu hiyo kila dola lilijenga ukuta milimani kwenye mipaka ili kuzuia mashambulizi ya maadui. Mwaka 221 kabla ya Kristo, mfalme Qin Shuhuang aliiunganisha China nzima, kisha akaziunganisha kuta zote zilizojengwa na madola hapo awali na zikawa ukuta mkuu. Katika miaka zaidi ya elfu mbili kila enzi ilizidi kuongeza urefu wa kuufanya ukuta huo kuwa na kilomita elfu 50, urefu ambao unaweza kuizunguka dunia kwa duara na zaidi kwa kufuata ikweta.

Siku hizi watu wanapotaja “ukuta mkuu” huwa wanalenga ukuta uliojengwa katika Enzi ya Ming, enzi iliyokuwa kati ya mwaka 1368 na 1644 baada ya Kristo. Ukuta huo unaanzia sehemu ya Jiayuguan, mkoani Gansu magharibi mwa China hadi kwenye ukingo wa mto Yalujiang, mkoani Heilongjiang mashariki mwa China, urefu wake ni kilomita elfu 7 na mita 3 ukipita mikoa na miji 9.

Ukuta huo uliojengwa milimani unapita sehemu za jangwa, mbuga za majani na ardhioevu, unainuka na kushuka, unapindapinda, ukionesha vya kutosha akili za wahenga wa China. Nje ya ukuta ni magema, ukuta na magema yanasaidiana kuzidisha kinga. Katika zama za kale, maadui wakitaka kuparamia magema makali na kufikia kwenye ukuta na kufanya mashambulizi kwa kubinua shingo nyuma ilikuwa ni vigumu na pengine haikuwezekana.

Ukuta ulijengwa kwa matofali makubwa na mawe makubwa kwa nje, na ndani ulijazwa kwa udongo na kokoto, kimo chake ni mita 10 na upana wa mita 5, upana huo ni wa kutosha kwa ajili ya askari kufanya vita na kupelekea mahitaji ya vita kama chakula na silaha. Kwa upande wa ndani ukuta huo una ngazi za mawe na mapango kurahisisha kupanda na kushuka ukutani. Kila baada ya safari fulani hujengwa dungu kwa ajili ya kuwekea silaha, chakula na kupumzikakwa askari, maadui wakija moto huwashwa juu ya dungu hizo ukitoa mwanga na moshi kupasha habari.

Katika zama za leo ingawa ukuta huo hauna maana katika mambo ya kijeshi lakini ujenzi wake unastaajabisha sana. Kwa mbali ukuta huo unaonekana wenye fahari na taadhima, unapindapinda kama nyoka mkubwa kwenye migongo ya milima. Kwa karibu unaonekana umejengwa kwa makini na werevu juu ya majabali, na dungu za kuwashia moto zinazounganisha ukuta huo kila baada ya urefu fulani zinaonesha uhodari mkubwa wa wajenzi.

Ukuta huo licha ya kuwa na maana muhimukatika historia, pia una maana katika utalii. Nchini China watu husema, “Asiyefika kwenye Ukuta Mkuu sio jabari”, watalii wa nchini na wa nchi za nje huona fahari kufika kwenye ukuta huo hata viongozi wa kitaifa wa nchi za nje, na watalii huwa wengi siku zote.

  Kwa kweli Ukuta Mkuu umelowa jasho na damu za wahenga wa China na pia ni matokeo ya akili za mababu wa China. Ukuta huo umepita miaka zaidi ya elfu moja bila kuanguka, sifa zake haijapotea, umekuwa ni ishara ya taifa la China. Mwaka 1987 ukuta huo uliorodheshwa kwenye urithi wa dunia kwa jina la “ishara ya taifa la China”.