Mapango ya Dunhuang
中国国际广播电台

      Mapango ya Dunhuang yaliyochongwa katika mlima Minshan, kaskazini magharibi mwa China, ni hazina kubwa ya sanaa, na ni makubwa kabisa kupita mapango yote mengine matatu nchini China. Kwenye mapango hayo zimechongwa sanamu nyingi za Buddha ambazo ni kumbukumbu zenye umri wa miaka elfu moja na enzi zaidi ya kumi za China. Mapango hayo bado mazima mpaka leo.

Mapango ya Dunhuang yako katika kitongoji cha Mji wa Dunhuang, mkoani Gansu, kaskazini magharibi mwa China. Katika Mlima wa Mingsha upande wa mashariki kwenye genge lenye urefu wa kilomita mbili kutoka kusini hadi kaskazini yalichongwa mapango kwa safu tano kutoka juu hadi chini, na hayo ndiyo mapango maarufu ya Dunhuang duniani.

Mapango hayo yalichongwa kuanzia mwaka 366. Siku moja sufii mmoja aliyejulikana kama Ledun alitembelea Dunhuang akagundua mwangaza mkali mlimani Mingsha; kwenye utusitusi aliona kama kuna mabuddha wengi kwenye mwangaza huo. Sufii Ledun akafikiri, “Hapa hakika ni mahali patakatifu!” Basi akawaagiza watu kuchonga pango la kwanza la kuwekea sanamu ya Buddha. Tokea hapo mapango yalikuwa yanaongezeka katika enzi kadhaa, hadi karne ya saba ya Enzi ya Tang, mapango yalikuwa yamefikia zaidi ya elfu moja. Kwa hiyo mapango ya Dunhuang pia yanaitwa “Mapango Elfu Moja ya Buddha”.

 

  Mapango ya Dunhuang yamedhihirisha sanaa ya ujenzi wa kale, picha za kuchorwa ukutani na sanamu za kuchongwa. Katika enzi kadhaa nchini China watu walichonga mapango na sanamu za mabuddha, na kuchora picha nyingi ukutani ndani ya mapango.

Ingawa karne nyingi zimepita, na kuharibiwa na binadamu, hadi leo kuna mapango karibu 500 na picha zenye eneo la mita elfu 50 na sanamu zaidi ya elfu 2. Kama picha zote zingeunganishwa pamoja zingekuwa na urefu wa kilomita 30.

 

  Kutokana na mapango ya Dunhuang kuwa katika sehemu isiyofikika kwa urahisi, hayakuwa maarufu sana katika miaka mingi iliyopita. Lakini mwanzoni mwa karne ya 20 baada ya kugunduliwa bohari ya vitabu, mapango hayo yakapata umaarufu haraka kote duniani, na kwa ajili hiyo wizi mkubwa wa vitu vya utamaduni ukatokea huko.

  Mwaka 1900, mtunzaji wa mapango Wang Daoshi alipokuwa akifuta vumbi, kwa bahati nzuri aligundua chumba kilichokuwa na vitabu vya msahafu. Chumba hicho kina urefu na upana wa mita tatu, kilikuwa kimesheheni vitu elfu 50 zikiwemo misahafu, tarazo, picha za kuchorwa n.k. ambazo ni adimu sana duniani. Hivi ni vitu kuanzia karne ya 4 hadi 11, ambavyo vinahusu na historia, jiografia, siasa, makabila, mambo ya kijeshi, lugha, fasihi, sanaa, dini, dawa na ufundi katika Asia ya Katikati, Asia ya Kusini na Ulaya, vinajulikana kama “ensaiklopidia ya zama za kale”.

Mtunzaji Wang Daoshi alifurahi mno kwa kuona vitu vingi vyenye thamani kubwa ambapo alichukua baadhi kuviuza ili ajipatie faida. Kutokana na vitu hivyo kuenea uraiani, vitu vingi ndani ya pango hilo vikatoweka bila kujulikana. “Wapelelezi” wa nchi mbalimbali walipopata habari walikwenda huko. Kutokana na udhaifu wa serikali ya Enzi ya Qing, “wapelelezi” hao kutoka nchi za Urusi, Uingereza, Ufaransa, Japan na Marekani walipora karibu misahafu elfu 40 na picha na sanamu nyingi, ambapo ni hasara kubwa mno. Hivi leo Uingereza, Ufaransa, Russia, India, Ujerumani, Denmark, Sweden, Korea ya Kusini, Finland na Marekani zote zina theluthi mbili ya vitu kutoka kwenye mapango ya Dunhuang.

Pamoja na ugunduzi wa chuma kilichokuwa na misahafu na vitu vya thamani, wasomi wa China walianza kufanya utafiti. Mwaka 1910, maandishi ya kwanza kuhusu utafiti wa vitu vya mapango ya Dunhuang yalichapishwa na kuanzia hapo taasisi ya maandishi ya Dunhuang ikaasisiwa. Katika muda wa zaidi ya miongo kadhaa, wasomi wa nchi nyingi wamekuwa wakifanya utafiti kuhusu sanaa ya Dunhuang, na wasomi wa China ndio waliopata mafanikio zaidi katika utafiti wao.

Mapango ya Dunhuang ni hazina ya utamaduni wa China. Serikali ya China ya leo siku zote inatilia maanani hifadhi yake. kwenye sehemu ya Dunhuang serikali imejenga jumba la makumbusho na vitu vilivyoonesha ndani ya jumba hilo baadhi ni vya bandia.

Hivi karibuni serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kutengeneza filamu ya mazingira ya mapango ya Dunhuang. Watu wanaweza kuona mambo yote yakiwa na picha na sanamu ndani ya mapango kwa kuangalia filamu bila ya kwenda kwenye mapango yenyewe. Hivyo uharibifu wa mapango unapungua sana.