Mji wa Kale Pingyao
中国国际广播电台

      Mji wa Pingyao uko katika sehemu ya kaskazini ya China, mkoani Shanxi. Kutokana na utamaduni wake usio wa kawaida, mwezi Desemba mwaka 1997 mji huo uliorodheshwa na UNESCO kwenye kumbukumbu za urithi wa utamaduni wa dunia.

  Mji wa Pingyao una umbo la mraba, na eneo la kilomita 2.25 tu. Barabara iliyonyooka toka kusini hadi kaskazini inapita katikati ya mji na inakutana na barabara nyingine iliyonyooka kutoka mashariki hadi magharibi kwenye kitovu cha mji. Barabara hizi mbili ndio mawasiliano pekee katika mji huo. Mapaa ya rangi ya njano kwenye makazi ya maafisa wa kifalme na mahekalu na mapaa yenye rangi ya kijivu ya nyumba za wananchi wa kawaida zinaonesha wazi matabaka ya watu katika jamii ya zamani nchini China.

Mji huo ulijengwa miaka 2800 iliyopita, na katika mwaka 1370 kuta za mji zilijengwa kwa matofali na kuimarishwa mara nyingi, hadi sasa kuta za mji bado ni imara.

Urefu wa kuta za mji ni zaidi ya mita elfu 6 na urefu wa kwenda juu ni mita 12, kuna milango sita.  

Kando ya barabara kuu mbili kuna vichochoro na maduka mengi.

Makazi katika mji wa Pingyao ni nyumba zilizojengwa kwenye pande nne zikiacha uwazi katikati, huu ni mtindo wa ujenzi wa kaskazini mwa China, ambao huwa na mstari katikati, na pande mbili za mstari huo zinalingana, aghlabu nyumba huwa na safu mbili au hata tatu kutoka nje hadi ndani. Karibu na nyumba kuna ukuta mrefu kiasi cha mita 8 hivi bila ya dirisha ili kukinga upepo wenye mchanga. Kwenye milango na madirisha kuna michongo makini ikionyesha upendo au matumaini mema ya wenye nyumba. Nyumba nyingi za raia zilijengwa katika Enzi ya Ming na Qing.

Ndani ya mji huo kuna mahekalu makubwa sita ambayo yalijengwa katika enzi za Ming na Qing.

Licha ya mahekalu hayo, pia kuna kumbukumbu nyingi za kale. Mathalan, ukumbi mkubwa wa Wanfo, ukumbi huo umekuwa na miaka zaidi ya elfu moja, na ndani ya ukumbi huo kuna sanamu za ufinyanzi zaidi ya elfu mbili na mawe yenye maandishi 1000.

  Mapema mwaka 1824 katika mji huo kulianzishwa duka la ubadilishaji wa fedha lililojulikana kwa jina la “Re Sheng Chang” ambalo ni la kwanza kabisa katika hisroria ya China kutumia hundi badala ya fedha taslimu. Kuanzishwa kwa duka hili kuna maana ya mwanzo wa kipindi kipya katika mambo ya fedha nchini China. Biashara yake hata ilifikia Japan, Singapore, Urusi, na maduka ya ubadiishaji wa fedha yalifikia 22.

Barabara ya magharibi inastahiki kuitwa barabara ya biashara katika enzi hizo. Hadi sasa pembeni mwa barabara hiyo maduka yanashikamana, hali inayoonesha ustawi ulivyokuwa zamani. Nyumba zenye maduka si za ghorofa lakini hazionekani kama zimechakaa ingawa ni miaka mingi imepita. Biashara inaendelea kuwa moto moto kana kwamba ilikuwepo miaka zaidi ya 100 iliyopita. Duka la kwanza la kubadilisha fedha bado lipo miongoni mwa maduka mengi. Kutokana na hali yake duka hili halioneshi kama ni la kifahari, lakini lilikuwa kituo cha mambo ya fedha nchini China.

Ingawa mji wa Pingyao ni wa kale, lakini hivi sasa bado una mvuto wake. Mji wa kale una sura yake maalumu na nje ya mji umejengwa “mji mpya”, na mji wa kale na mji mpya unasaidiana kuongeza mvutio.