Kaburi la Mfalme Qinshihuang na Sanamu za Askari na Farasi
中国国际广播电台

      Mfalme Qinshihuang aliyezaliwa mwaka 259 na kufariki dunia mwaka 210 kabla ya kuzaliwa Kristo, alikuwa mfalme wa kwanza wa jamii ya kimwinyi ya China. Mfalme huyo anatajwa sana katika historia lakini hadi sasa uamuzi unaokubalika juu ya hadhi yake haujapatikana. Alikuwa wa kwanza kabisa kuunganisha China nzima; alitumia hatua mbalimbali za kustawisha uchumi na utamaduni, miongoni mwa hatua hizo ni kusawazisha sarafu, maandishi, upimaji wa uzito na urefu, na alijenga ukuta mkuu wa kukinga maadui. Hatua hizo zilimpatia sifa za kuwa mwanasiasa mashuhuri katika historia ya China. Lakini kwa upande mwingine alikuwa mfalme mkatili na mbadhirifu kupita kiasi. Ili kuwapumbaza kimawazo watu wake alitumia hata sera ya kuchoma moto vitabu ambavyo havikulingana na mawazo yake ya utawala na kuwatesa wasomi wa Confucius; pia watu ambao walitofautiana naye kimawazo aliwazika wakiwa hai ili kudumisha utawala wake. Aidha, katika kipindi chake cha utawala alitumia fedha nyingi na watu wengi kujijengea kaburi na kasri ya anasa ili awe na maisha ya furaha. Mfalme Qinshihuang alianza kujenga kaburi lake si muda mrefu baada ya kuunganisha China nzima. Watu laki 7 walilazimishwa kujenga kaburi hilo na mfalme alipofariki dunia miaka 40 baadaye walikuwa hawajamaliza kulijenga. Kaburi la mfalme huyo lenye eneo la kilomita za mraba 56.25 liko kwenye mlima Lishan katika kitongoji cha Mji wa Xi'an mkoani Shan'xi. Msingi wa kaburi ni wa mraba ambao una urefu wa mita 350 kutoka kusini hadi kaskazini, na mita 345 kutoka mashariki hadi magharibi, na kimo cha mita 76. Kutoka juu, kaburi hilo lina umbo la piramidi. Kutokana na utafiti wataalamu wa mambo ya kale wamegundua kwamba pembeni mwa kaburi hilo kuna mashimo na makaburi zaidi ya mia 5 ya vitu na makaburi ya wajenzi wa kaburi waliotumiwa kama kafara. Kwenye mashimo kulifukiwa sanamu za farasi na mikokoteni ya shaba nyeusi ambayo yanaeleza jinsi mfalme Qinshihuang alivyokuwa kwenye gari la farasi, pia zipo sanamu za vibanda vya farasi ndani ya kasri, kwenye shimo kubwa sanamu za askari na farasi ambazo zinaashiria jeshi shupavu katika enzi yake ya Qin zimefukiwa.

Sanamu za askari na farasi zinajulikana kama miujiza ya nane duniani na ugunduzi wake ni wa bahati tu. Mwaka 1974 wakulima wa sehemu hiyo walipochimba kisima walipata vigae vingi vya vyombo vya udongo, lakini hawakutilia maanani na walitaka kuvitupa. Kwa bahati nzuri wakati huo mtaalamu mmoja aliyekuwa huko, alivitazama na kuona kuwa pengine ni ugunduzi mkubwa. Alitoa taarifa kwenye idara ya mambo ya kale wilayani, hivyo sanamu za askari na farasi zikafukuliwa. Hadi leo sanamu 500 za askari, mikokoteni 18 ya vita ya mbao, na sanamu zaidi ya 100 za farasi zimegunduliwa. Sanamu za askari zina maumbile makubwa ambapo urefu ni wastani wa mita moja na sentimita 80, sura zao zilichongwa kama za halisi na hisia kwenye nyuso zao ni tofauti, ambapo zimeonyesha ustadi mkubwa wa uchongaji katika enzi ya Qin. Sanamu za askari na farasi zinawavutia sana wageni kutoka nchi mbalimbali, na wengi huja kuziangalia bila kujali umbali. Baadhi ya viongozi wakubwa wa serikali pia huomba kwenda huko kushuhudia wenyewe. Rais mstaafu wa Marekani Ronald Reagan alielezea sanamu hizo kuwa ni miujiza ya ajabu ya binadamu. Kutokana na uduni wa elimukale ya China, na kuhifadhi kaburi hilo lisiharibike hivi sasa serikali ya China haina mpango wa kuchimbua kaburi halisi la mfalme Qinshihuang. Katika miaka ya karibuni, vitu zaidi ya elfu 50 na baadhi ambavyo ni kama hohari adimu duniani viligunduliwa kutoka kwenye mashimo pembeni mwa kaburi la Qinshihuang. Mojawapo ni mkokoteni wa kuvutwa na farasi uliotengenezwa kwa shaba nyeusi na kupambwa kwa dhahabu na fedha. Mkokoteni huo uliotengenezwa kwa makini uligunduliwa mwaka 1980 ambapo ukubwa wake ni nusu ya mkokoteni halisi, ukionesha jinsi mfalme Qinshihuang alivyoendesha gari lake. Mwaka 1987 kaburi na sanamu za askari na farasi ziliorodheshwa na UNESCO kwenye kumbukumbu ya urithi wa utamaduni wa dunia.